Ndugu Wananchi;

Hatimaye imewadia ile siku ya kuuaga mwaka mmoja na kuukaribisha mwingine. Leo tunauaga mwaka 2008 na kuukaribisha mwaka 2009.

Kwanza kabisa, naomba sote tumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujaalia uhai na kutuwezesha kuiona siku hii adhimu salama. Ni wajibu wetu kumshukuru Muumba wetu kwani wapo wenzetu wengi hawakujaaliwa kuiona siku ya leo kwa vile wametangulia mbele ya haki. Wakati tukikumbushana wajibu wetu wa kumuomba Mwenyezi Mungu awape marehemu wetu hao mapumziko mema, tumuombe pia awape nafuu na kuwaponya wenzetu wote wanaougua maradhi mbalimbali ili wajumuike nasi katika shughuli za ujenzi wa taifa letu.

Ndugu Wananchi;
Mwaka wa 2008 tunaoumaliza leo ulikuwa mwaka wa aina yake kwa taifa letu na katika historia ya uongozi wangu. Ulikuwa ni mwaka ambao tumepata mafanikio mengi mazuri na mengine ya kihistoria katika nyanja mbalimbali za maisha ya wananchi wa Tanzania na taifa letu. Lakini, pia kulikuwepo na changamoto au matukio machache ambayo yalisababisha baadhi ya watu ndani na nje ya nchi yetu wapate shaka juu ya hatima ya umoja, amani na utulivu wa nchi yetu. Umoja, amani na utulivu ndiyo nguzo kuu na sifa kubwa inayoitofautisha na kutambulisha Tanzania miongoni mwa mataifa barani Afrika.

Ndugu Wananchi;
Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwamba tumeumaliza mwaka huu kwa usalama, amani na utulivu. Tuzidi kumuomba baraka na rehema zake, katika mwaka 2009, ili nchi yetu iendelee kuwa na amani, utulivu na watu wake waishi kwa upendo, umoja, masikilizano, mshikamano na ushirikiano kama ndugu wa taifa moja.

Pamoja na kumuomba Mwenyezi Mungu, hatuna budi kutambua kuwa dhamana ya kuhakikisha kuwa nchi yetu inaendelea kuwa tulivu na yenye amani na upendo miongoni mwa watu wake ni yetu wenyewe. Ni ukweli ulio wazi kuwa katika mwaka huu tunaoumaliza sasa baadhi yetu tumekuwa tunafanya vitendo au kutoa kauli ambazo zilikuwa zinalielekeza taifa kubaya. Tena tulikuwa tunafanya hivyo kwa ajili ya kuendeleza manufaa binafsi ya kisiasa. Ni matumaini yangu kuwa tutajiepusha na mambo hayo katika mwaka 2009. Nawasihi viongozi wenzangu wa kisiasa na wa kijamii tubadilike, tuweke mbele maslahi ya taifa ili tuiepushe nchi yetu na mabalaa ambayo baadhi ya wenzetu yaliwakuta.

Hali ya Uchumi wa Nchi na Dunia
Ndugu Wananchi;
Kwa jumla hali ya uchumi wa nchi yetu kwa mwaka 2008 ilikuwa ya kiwango cha kuridhisha. Lakini, hali ingekuwa bora zaidi kama uchumi wa dunia usingepata misukosuko iliyoupitia sasa. Kwa sababu ya matatizo makubwa yanayoukabili uchumi wa dunia, baadhi ya malengo tuliyojiwekea kuhusu ukuaji na mwenendo wa uchumi wetu yameathiriwa.

Mfumuko wa Bei
Ndugu Wananchi;
Bei kubwa za mafuta zilizokuwepo kwa karibu miaka miwili mfululizo na hasa katika miezi kumi ya mwanzo ya mwaka huu zilipokuwa juu sana, imekuwa kichocheo kikubwa cha kupanda sana kwa mfumuko wa bei na ukali wa maisha hapa nchini. Aidha, kupanda sana kwa bei za vyakula tunavyoagiza kutoka nje kama vile ngano, mchele na vinginevyo viliifanya hali ya mfumuko wa bei kuwa mbaya zaidi.

Tulikuwa tumejiwekea lengo, kwa mfano, katika bajeti iliyopita kuwa tutateremsha mfumuko wa bei hadi kuwa asilimia 4.5 mwezi Juni, 2008 kutoka asilimia 5.9 ya mwezi Juni, 2007. Badala yake mfumuko wa bei ukawa asilimia 9.3 mwezi Juni, 2008 na kupanda hadi asilimia 12.3 ilipofika mwezi Novemba, 2008. Hivi sasa bei za mafuta zimeshuka kuanzia Oktoba, 2008 na hivi leo zimefikia dola za Kimarekani 38.4. Hali kadhalika, bei za baadhi ya vyakula nazo zimeshuka. Lakini, itachukua muda mpaka manufaa ya hali hiyo kuonekana kwa uchumi wa nchi yetu na wananchi wake.

Ndugu Wananchi;
Wakati mwingine hali huwa hivyo kwa sababu ya ukaidi na tamaa ya wafanyabiashara. Nimekwishawaagiza Mawaziri wahusika kuzibana mamlaka husika kutimiza ipasavyo wajibu wao kwa mujibu wa mamlaka waliyopewa kisheria kuwalinda wananchi dhidi ya wafanyabiashara wa aina hiyo. Wakati huo huo narudia kuwataka wafanyabiashara watoe ushirikiano unaostahili kwa maslahi ya wateja wao na taifa kwa jumla. Aidha, nazitaka mamlaka husika kutokuchelewa wala kuchelea kuchukua hatua zipasazo kwa wafanyabiashara wakaidi.

Ndugu Wananchi;
Kutetereka kwa mfumo wa fedha wa kimataifa na kuanguka kwa masoko ya hisa katika mataifa yaliyoendelea kumesababisha uchumi wa nchi hizo kudhoofika. Hali hiyo imekuwa na athari za namna na viwango mbalimbali kwa uchumi wa nchi zinazoendelea kama Tanzania.

Nilikwishalieleza siku za nyuma na napenda kurudia kusema kuwa sekta ya fedha hapa nchini bado ni tulivu. Haijaathiriwa na misukusuko inayoikumba sekta ya fedha ya kimataifa. Zipo sababu kuu mbili.

Kwanza, kwamba, sekta yetu ya fedha na soko la mitaji havijaunganishwa na mfumo wa fedha wa kimataifa na masoko ya hisa ya kimataifa. Hivyo basi, hakuna athari za moja kwa moja zinazotukuta hapa nchini kwa sasa.

Pili, kuna usimamizi mzuri wa soko na sekta ya fedha unaofanywa na Benki Kuu. Mpaka sasa, juhudi hizo za Benki Kuu zimesaidia. Hata hivyo, tunatambua haja na hoja ya kuendelea kuwa makini. Inaelekea matatizo ya mfumo wa fedha na uchumi katika nchi zilizoendelea yatachukua muda mrefu kutengemaa. Hatujui siku za usoni mambo ya yatakuwaje.

Serikali itaendelea kushirikiana na Benki Kuu kuzuia athari za soko la fedha duniani zisitufikie au kama zitatufikia, basi makali yake yawe nafuu. Kwa sasa mfumo wa ufuatiliaji (surveilance) na ule wa kutoa tahadhari ya mapema (early warning system) vinafanya kazi ipasavyo. Tuko tayari kuchukua hatua zaidi kama hapana budi.

Ndugu Wananchi;
Athari za hiyo Tsunami ya uchumi wa dunia, kama ilivyoitwa na baadhi ya watu, kwa uchumi wetu tumeanza kuziona kwa baadhi ya sekta. Tuchukue kwa mfano, sekta ya utalii. Katika mapumziko yangu ya mwisho wa mwaka huu nilitembelea mbuga zetu za hifadhi ya wanyama za Tarangire, Ziwa Manyara, Ngorongoro na Serengeti ya Kusini. Katika mazungumzo yangu na viongozi wa hoteli, hifadhi hizo na wale wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) nimeelezwa jinsi idadi ya watalii ilivyopungua na mapato yao kushuka kwa kati ya asilimia 7 na 18.

Aidha, nimezungumza na baadhi ya wamiliki wa viwanda vya kuchambua pamba na viongozi wa Bodi ya Pamba. Wote wamenieleza tabu wanayoipata ya kuuza pamba yao nje. Pia wanaelezea jinsi bei ya pamba ilivyoshuka katika soko la dunia. Katika kipindi cha mwezi Machi hadi Julai, 2008 bei ya pamba ilikuwa senti 82 za dola za Kimarekani kwa paundi na kushuka hadi senti 45 kwa paundi kwa sasa.

Hali kwa zao la kahawa nayo siyo nzuri. Nimeambiwa kuwa kati ya mwezi Agosti, msimu wa kahawa ulipoanza, na tarehe 18 Disemba 2008, bei ya kahawa ya Arabica kwenye soko la dunia, imeshuka kutoka dola za Kimarekani 158 hadi 104 kwa gunia la kilo 50. Hii ni sawa na anguko la asilimia 34. Katika kipindi hicho hicho, bei ya kahawa ya robusta imeshuka kutoka wastani wa dola za Kimarekani 93.6 hadi dola 65.46 kwa gunia la kilo 50. Hii ni sawa na anguko la asilimia 30.

Ndugu Wananchi;
Hata kwa mazao mengine nayo kwa jumla, hali ni hiyo hiyo ya kupungua kwa mauzo nje na kushuka kwa bei. Matatizo tunayoyapata sisi kwa mazao yetu ndiyo yaliyoikuta bidhaa ya mafuta. Kwa sababu ya uchumi kutetereka katika nchi za Marekani, Ulaya Magharibi, Japan, China na India mahitaji ya mafuta yamepungua na bei ya mafuta imeanguka kupita kiasi.

Ndugu Wananchi;
Kupungua kwa mauzo nje na bei ya bidhaa zetu pamoja na kupungua kwa watalii kuna athari kwa uchumi wa nchi yetu. Mapato yetu ya fedha za kigeni yatapungua jambo ambalo litapunguza akiba yetu ya fedha za kigeni, hivyo kuathiri uwezo wetu wa kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje. Aidha, mapato ya Serikali kwa kodi zitokanazo na mauzo hayo yatapungua, hivyo kuathiri uwezo wa Serikali wa kutimiza majukumu yake ya kiutawala na kiuchumi. Isitoshe ajira chache zilizopo katika sekta husika zitapungua na kusababisha watu hao kuwa na hali mbaya kiuchumi.

Ndugu Wananchi;
Hali mbaya ya uchumi wa dunia inasababisha uwekezaji wa kutoka nje nao kuathirika. Baadhi ya wawekezaji walioonyesha nia ya kuwekeza nchini wameahirisha nia yao. Ukiacha hofu inayotokana na hali mbaya ya uchumi wa dunia, wengine wamekuwa wanapata ugumu wa kupata mikopo kutoka katika mabenki. Mabenki yamekuwa yanasita kukopesha na pale yanapokopesha masharti yake huwa magumu kiasi cha kuwakatisha tamaa wakopaji.

Ndugu Wananchi;
Nimezitaja baadhi tu ya athari za kuyumba kwa uchumi wa dunia kwa uchumi wa nchi yetu ili tutambue kuwa tupo kwenye mazingira magumu na hali ya baadae ni ya mashaka. Tunaweza kunusurika kwenye eneo moja lakini tukaathirika kwenye maeneo mengine kwa sababu uchumi wetu ni uchumi wa dunia ya utandawazi. Kutokana na athari hizo inakadiriwa kuwa hatutafikia malengo yetu ya kukua kwa uchumi mwaka huu 2008 na hata mwaka ujao wa 2009. Inakadiriwa kuwa uchumi utakua kwa asilimia 7.7 badala ya 7.8 mwaka huu na mwakani utakua kwa asilimia 7.3 badala ya asilimia 8 iliyokadiriwa.

Ndugu zangu;
Watanzania wenzangu;
Napenda sote tutambue kuwa kuna kila dalili kuwa mwaka 2009 huenda tutatumia muda mwingi na nguvu nyingi kukabili athari za machafuko ya uchumi wa dunia. Kwa ajili hiyo, hatuna budi kutambua hivyo mapema na kuwa tayari kusimama kidete kukabiliana na athari zake. Sisi katika Serikali tunafuatilia kwa karibu hali inavyoendelea duniani na hapa nchini na kuamua hatua za kuchukua. Tutaendelea kupashana habari. Maombi yangu kwenu wananchi wenzangu ni uelewa wenu na ushirikiano wenu. Umoja, mshikamano na ushirikiano wetu wakati huu ndivyo vitakavyotukinga na kutuvusha katika tatizo hili kubwa.

Ndugu Wananchi;
Yapo mambo kadhaa ambayo hatuna budi kufanya katika kukabiliana na hali hii tete hapa nchini. Miongoni mwa hayo lipo suala la kujenga uwezo wa ndani wa kujitegemea kwa mambo fulani fulani kama vile chakula na bidhaa muhimu kwa matumizi ya watu. Pili, linalolingana na hilo, ni suala la kukuza utalii wa ndani na kutafuta vyanzo vipya vya watalii kama vile Mashariki ya Kati na Asia. Tatu, kukuza masoko ya ndani kwa bidhaa zetu na masoko ya kanda kama vile SADC na EAC. Wakati mwigine tunahangaikia masoko ya mbali wakati soko lipo hapa ndani au nchi jirani.

Ndugu Wananchi;
Kwangu mimi kauli mbiu muafaka kwa mwaka 2009 ni “Mwaka wa Kuhami na Kukuza Uchumi wa Taifa”. Bahati nzuri kauli mbiu hii inawiana na mpango wangu wa kazi nilipoingia madarakani. Nilikuwa nimepanga kuwa, katika nusu ya kwanza ya kipindi changu cha uongozi tuelekeze nguvu zetu katika upatikanaji wa huduma za kiuchumi na kijamii, na nusu ya pili tushughulikie kukuza uchumi. Nafurahi kwamba, tumefanikiwa kuweka misingi madhubuti ya kisera na mipango ya uhakika ya utekelezaji kuhusu elimu, afya, barabara, maji na umeme vijijini. Utekelezaji wake unaendelea na changamoto yetu kubwa ni upatikanaji wa fedha za kutosha kutekeleza malengo tuliyojiwekea.

Nashukuru kwamba ufanisi mkubwa tulioupata katika ukusanyaji wa mapato ya ndani na misaada ya washirika wetu wa maendeleo tumeweza kupata mafanikio tuliyoyapata mpaka sasa. Hata hivyo mahitaji ya rasilimali bado ni makubwa. Ni wajibu wetu kuendelea kutafuta.

Ndugu Wananchi;
Kuanzia mwaka 2009 Serikali itaelekeza nguvu katika kukuza uchumi wa nchi kwa lengo la kuongeza mapato ya nchi na wananchi wake. Bahati mbaya au nzuri yanayotokea sasa duniani yanasisitiza haja na hoja ya kufanya hivyo. Pia, yameongeza jambo jipya la kufanya, nalo ni la kuhami uchumi usitetereke.

Kilimo Kipaumbele cha Kwanza
Ndugu Wananchi;
Katika agenda yetu ya kukuza uchumi, kilimo kimepewa kipaumbele cha kwanza. Tunafanya hivyo kwa sababu nzuri na za msingi kabisa. Kwanza, tunataka kuhakikisha kuwa tunajitosheleza kwa chakula na tunakuwa na ziada ya kutosha. Katika mazingira ya sasa ambapo bei za vyakula duniani ziko juu, kuwa na upungufu wa chakula na kulazimika kuagiza kutoka nje kutazua matatizo makubwa nchini. Mfumuko wa bei utatushinda kuudhibiti.

Pili, kilimo kitatupatia malighafi ya viwanda vya kusindika mazao ya kilimo na kuzalisha bidhaa kamili zinazotokana na mazao ya kilimo. Kuendeleza viwanda vya aina hii ni kipaumbele chetu cha pili katika agenda yetu ya kukuza uchumi wa taifa. Lazima tuanze safari ya kuuza nje mazao ya kilimo yakiwa yameongezewa thamani kuliko kuyauza yakiwa ghafi kama tufanyavyo sasa. Tutafanya kila liwezekanalo kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ili kufanikisha azma yetu hiyo.

Tatu, kilimo ni chanzo kikubwa cha mapato ya fedha za kigeni kwa nchi, mapato ya serikali kupitia kodi na ni tegemeo la watu wengi nchini kwa uhai wao. Asilimia 8.5 ya fedha za kigeni hutokana na mazao ya kilimo na asilimia 80 ya Watanzania wanaishi vijijini ambapo kilimo ndiyo shughuli yao kuu ya kuwapatia mapato na maisha yao.

Hali ya Chakula
Ndugu Wananchi;
Hali ya upatikanaji wa chakula nchini ni nzuri kwa miaka miwili mfululizo sasa, yaani 2007 na 2008, na tumekuwa tunapata ziada ingawaje ni kidogo. Napenda kuwahakikishia kuwa hakuna tishio la njaa nchini. Hata yale maeneo ambayo yamekuwa yanapata upungufu wa chakula tumeweza kuyahudumia kwa kutumia ziada hiyo na akiba kutoka katika Hifadhi ya Taifa ya Chakula (SGR).
Kwa mfano, tathmini iliyofanywa mwezi Septemba, 2008 inaonyesha kuwa watu 240,544 katika Wilaya 20 nchini watakabiliwa na upungufu wa chakula kati ya Desemba, 2008 na Januari, 2009. Watu hao watahitaji tani 7,182 za chakula ambacho tayari kimekwishatengwa kutoka Hifadhi ya Taifa ya Chakula. Hifadhi hiyo sasa ina akiba ya tani 127,420.

Ndugu Wananchi;
Mvua za vuli hazikuwa nzuri kwa mikoa ya Pwani, Dar es Salaam, Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara. Lakini, zimekuwa nzuri kwa mikoa ya Kagera, Mwanza na Mara. Hivyo basi mavuno ya vuli hayatakuwa mazuri katika mikoa iliyoathirika. Hali hiyo inaweza kuongeza iadi ya watu watakaohitaji msaada wa chakula. Hata hivyo, hakuna shaka yoyote tutaweza kuwahudumia. Matumaini yetu na sala zetu kwa mikoa hiyo ni kuwa mvua za masika zitakuwa nzuri. Ikiwa hivyo mzigo utapungua. Bahati nzuri mikoa mingine inayopata mvua moja hali ya mvua ni nzuri, hivyo inatutoa hofu ya upungufu mkubwa wa chakula nchini. Tuzidi kumuomba Mungu mvua zinyeshe kama kawaida katika mikoa hiyo nayo.

Ndugu Wananchi;
Dhamira yetu katika kuelekeza nguvu zetu katika kuendeleza kilimo ni kuongeza tija. Bahati mbaya kwa sasa tija iko chini sana jambo linaloelezea hofu za upungufu wa chakula, mazao ya biashara na hali duni ya maisha kwa wakulima wengi.
Kwa ajili hiyo Serikali imekusudia mwaka 2009 kutilia mkazo mambo matano:
a. Upatikanaji na matumizi ya mbegu bora;
b. Upatikanaji na matumizi ya mbolea;
c. Upatikanaji wa maafisa ugani;
d. Uendelezaji wa kilimo cha umwagiliaji pale inapowezekana; na
e. Upatikanaji na uimarishaji wa masoko ya mazao ya wakulima.

Ndugu Wananchi;
Mambo yote hayo na mengine ambayo sikuyataja si mapya. Tumekuwa tunayatekeleza katika miradi na programu mbalimbali za kuendeleza kilimo nchini kama vile DADP’s, PADEP na ASDP. Tunachokusudia kufanya mwaka ujao ni kutoa msukumo maalum wa kuendeleza kilimo kama tulivyofanya kwenye elimu na tunavyokusudia kufanya kwa upande wa afya.

Kuhusu upatikanaji wa mbegu, tumepanga kuimarisha vituo vyetu vya utafiti wa mbegu na kuongeza uwezo wetu wa kuzalisha mbegu hapa nchini. Kwa ajili hiyo nimewaagiza Jeshi la Kujenga Taifa na Jeshi la Magereza watumie sehemu ya mashamba yao kuzalisha mbegu.
Nafuraji kwamba viongozi wa idara zetu hizo tayari wameshaelewana na wenzao wa Wakala wa Mbegu nchini kufanikisha mpango huo muhimu. Kwa upande wa mbolea nafurahi kusema kuwa kauli yangu niliyotoa Bungeni tarehe 21 Agosti, 2008 kuhusu pesa za EPA imeshaanza kutekelezwa. Shilingi bilioni 30 zimetengwa kwa ajili ya mbolea ya ruzuku na bilioni 10 kwa ajili ya madawa ya mimea. Madawa ya mifugo yametengewa shilingi bilioni 10 na mikopo ya kilimo TIB shilingi bilioni 10.

Ndugu Wananchi;
Nafurahi pia kuwa dhamira yetu ya kuzalisha mbolea hapa nchini inatekelezwa vizuri. Kiwanda cha kuzalisha mbolea ya phosphate pale Minjingu, mkoani Manyara kimekamilika na kimeshaanza kazi. Wakati huo huo mchakato wa ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha mbolea ya NPK hapo Minjingu umeshaanza. Aidha, uamuzi wetu wa kujenga kiwanda cha mbolea ya urea na ammonia kule Mtwara umefikia hatua nzuri. Kampuni ya kuwekeza imekwishapatikana na shughuli za mchakato wa ujenzi wa kiwanda hicho ziko mbioni.

Hatua hizi zote zitakapokamilika, ndani ya miaka miwili ijayo, zitaiwezesha nchi yetu kuwa moja ya wazalishaji wakubwa wa mbolea katika kanda yetu ya SADC na Jumuiya ya Afrika Mashariki. Tutatosheleza mahitaji yetu na kuwa na ziada ya kuuza kwa wengine nchi za nje na kujipatia fedha za kigeni.

Mifugo
Ndugu Wananchi;
Juhudi za kuongeza tija katika kilimo zitaelekezwa pia kwenye mifugo. Nia yetu ni kuboresha ufugaji wetu ili tupate mifugo inayotoa nyama nyingi, maziwa mengi na ngozi zilizo bora. Juhudi hizo zitajumuisha kuboresha aina ya mifugo yetu kwa kutumia madume bora na uhamilishaji. Pia itahusisha upatikanaji wa huduma za kinga na tiba ya mifugo, majosho, malisho, maji, masoko ya mifugo na mazao ya mifugo. Suala la kuwa na viwanda vya kusindika mazao ya mifugo nalo tutalipa uzito unaostahili.

Uwekezaji
Ndugu Wananchi,
Katika mwaka 2009, tutaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi wa ndani na nje kuja kuwekeza nchini. Sifurahishwi na taarifa nizipatazo kuwa mazingira ya uwekezaji na kufanya biashara nchini bado hayajaboreka vya kutosha. Na, linalonisumbua zaidi ni kule kuanza kujengeka dhana kuwa Tanzania inaanza kupoteza sifa ya mahali rafiki kwa wawekezaji. Hii si dalili nzuri, lazima tuibadili haraka iwezekanavyo.

Ndugu Zangu;
Dunia nzima hata mataifa tajiri yanavutia wawekezaji seuze siye maskini? Uwekezaji ndiyo chachu ya kukua kwa uchumi. Bila ya uwekezaji uchumi haukui. Wote tunaowasifia kufanikiwa kiuchumi ni kutokana na uwekezaji. Hata China imeendelezwa na uwekezaji tena kutoka mataifa ya kibepari.
Tutayaainisha mambo yanayotufikisha hapo na kuyatafutia majawabu. Natambua kuwepo malalamiko kuhusu usumbufu na urasimu mkubwa katika kuwahudumia wawekezaji. Mlolongo na muda wa uamuzi ni mrefu, kuna usumbufu upande wa kodi na tuhuma za vitendo vya rushwa zinasikika. Wakati mwingine kauli za wanasiasa wetu zimekuwa zinawaogopesha wawekezaji. Yote haya na mengineyo ni mambo ambayo yapo kwenye uwezo wetu kuyarekebisha.

Tumedhamiria kuyakabili kwa dhati matatizo hayo ili tuifanye Tanzania kuwa nchi nzuri kuwekeza. Pamoja na kusimamia kwa karibu mradi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara Tanzania (BEST), nakusudia kuanzisha kitengo maalum cha kusikiliza malalamiko ya wawekezaji na kuyatafutia ufumbuzi (Investors Complaints Bureau). Kitengo hicho kitakuwa chini ya Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi na kazi yake itakuwa ni kutatua kwa haraka malalamiko ya wawekezaji.

Mikopo ya Wajasiriamali Wadogo na SACCOS
Ndugu Wananchi,
Miaka miwili iliyopita tulianzisha mpango wa mikopo kwa wajasiriamali wadogo wadogo ambao hawana sifa za kukopesheka katika mabenki kwa utaratibu wa kawaida. Tumefanya hivyo ili wanyonge nao wapate fursa ya kujiendeleza na kujikwamua. Kama tujuavyo, tulitenga shilingi bilioni moja kwa kila mkoa wa Tanzania Bara na shilingi milioni 100 kwa kila mkoa kwa mikoa minne ya Zanzibar na milioni 200 kwa mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.
Tulikubaliana kuwa mikopo hiyo itatolewa na Benki za CRDB na NMB na asasi ndogo za fedha kama vile Benki ya Posta, PRIDE, SELF n.k.
Taarifa zinaonyesha kuwa hadi Novemba 30, 2008 jumla ya shilingi bilioni 39 zimekopeshwa na NMB (16.1bn/=) na CRDB (22.9bn/=) na watu 48,339 wamenufaika pamoja na SACCOS 192 na vikundi 137. Benki na asasi nyingine 12 zimeshakopesha SACCOS 236 na shilingi 4.6 bilioni zimetumika katika wilaya 46 za Tanzania Bara.

Katika ziara zangu katika mikoa ya Bara nimepokea malalamiko ya watu kuhusu upatikanaji wa mikopo hiyo. Moja ya jambo nililojifunza ni kuwa, mahitaji ya mikopo ni makubwa na fedha zilizotolewa ni kidogo. Jawabu lake ni kuongeza fedha, jambo ambalo tuko tayari kufanya.
Jambo la pili nililojifunza ni kuwa fedha zilizolipwa na wakopaji wa awali hazijazungushwa. Jawabu lake ni kuzizungusha ili wengine nao wakope. Tunazungumza na mabenki juu ya jambo hilo. Ni dhamira yangu mwaka ujao wa 2009 tufanye tathmini ya kina ya mpango huu ili tubaini mapungufu yake na mbinu za kuyarekebisha ili tuongeze fedha na kunufaisha watu wengi zaidi wa kipato cha chini wainue hali zao za maisha.

Kwa nia ile ile ya kuwasaidia watu wasiokuwa na sifa za kukopesheka moja kwa moja na mabenki wapate mitaji ya kufanyia shughuli zao za kujipatia kipato, tuliwahimiza wananchi waanzishe Vyama vya Kuweka na Kukopa. Tulipoingia madarakani kulikuwa na SACCOS 1,875 na sasa zipo 4,780 kutokana na msukumo maalum tulioutoa kwa uanzishwaji wake.
Fedha nyingi za akiba zimewekwa na wanachama wa SACCOS hizo na mikopo mingi imetolewa kwa wanachama hao. Aidha, SACCOS kadhaa zimeweza kupata mikopo ya kawaida ya mabenki na kupitia mikopo ya wajasiriamali wadogo wadogo.

Pamoja na kujenga utamaduni mzuri wa watu kuweka akiba, SACCOS zimekuwa nyenzo muhimu ya kukuza uchumi na vyombo vya kutumainiwa na wananchi wa kawaida katika harakati zao dhidi ya umaskini. Napenda kuahidi kuwa ni makusudio yetu kuendeleza juhudi za kuimarisha na kuanzisha SACCOS nchini.
Huduma za Kiuchumi na Kijamii
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka ujao tutaendeleza jitihada za kuongeza na kuboresha upatikanaji wa huduma muhimu za kiuchumi na kijamii hususan elimu, afya, maji, umeme na barabara. Kazi kubwa imefanyika na watu wengi sasa wanapata huduma hizo, lakini bado hazijatosheleza mahitaji na viwango vya ubora.
Tunatambua wajibu wa Serikali wa kuongeza fedha katika bajeti za sekta hizo ili miradi mingi zaidi itekelezwe na kukidhi mahitaji ya wananchi. Hiyo ndiyo dhamira yetu kufanya katika mwaka 2009 na miaka ijayo. Sekta ya maji na umeme vijijini tutazipa kipaumbele stahiki.

Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa elimu ya sekondari napenda kwa mara nyingine tena kuwashukuru na kuwapongeza sana wananchi kwa moyo wao wa kujitolea na kujituma. Moyo wao huo na ushirikiano wao na Serikali ndiyo siri iliyotufanya tuendelee kupata mafanikio makubwa katika upanuzi wa elimu ya sekondari nchini.
Hivi sasa, nchini tunazo sekondari za Serikali 3,039 kutoka 1,202 mwaka 2005 na idadi ya wanafunzi imeongezeka kutoka 524,325 mwaka 2005 hadi 1,222,403 mwaka huu. Haya si mafanikio madogo katika kipindi kifupi hivi.

Naomba moyo huo wa kujitolea na ushirikiano viendelee kwa manufaa ya watoto wetu na wajukuu wetu waliopo sasa na wajao. Sisi katika Serikali tunaahidi kuendelea kutimiza wajibu wetu katika ushirikiano wetu huo. Tutaendelea kukabili changamoto za upatikanaji wa walimu, vitabu, vifaa vya kufundishia, maabara na nyumba za walimu. Tunatambua kuwa ni mzigo mkubwa lakini hatuna budi kuubeba kwa maslahi ya taifa letu.

Matokeo ya Darasa la Saba
Ndugu Wananchi;
Kwa miaka miwili mfululizo matokeo ya mitihani ya darasa la saba yamekuwa si mazuri. Mwaka wa jana kiwango cha kufaulu kilikuwa asilimia 54.2 na mwaka huu ni asilimia 51.2. Hali hii si nzuri na hatuwezi kuacha iendelee. Hatuna budi kujiuliza kulikoni na kutafuta majawabu muafaka. Nimeiagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini kasoro zilizopo na kupendekeza hatua za kuchukua. Aidha, nimemuagiza Waziri Mkuu kulisimamia suala hili kwa ukamilifu.

Barabara

Ndugu Wananchi;
Katika mwaka huu tunaoumaliza leo, tuliendelea kutoa kipaumbele cha juu kwa sekta ya miundombinu. Tumeongeza bajeti ya miundombinu na sasa ni ya pili kwa ukubwa baada ya elimu. Kiasi cha shilingi bilioni 973.3 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu nchini katika mwaka wa fedha 2008/09. Tumeendelea kujenga barabara mpya za lami, za changarawe na za udongo. Pia tumekarabati na kuimarisha barabara zilizopo.

Lengo letu la kuunganisha Makao Makuu ya Mikoa yote kwa barabara za lami sasa lina muelekeo mzuri. Mipango kwa kuunganisha mikoa ya Lindi, Mtwara, Rukwa na Ruvuma imefikia mahali pazuri.
Hivi sasa nguvu zetu tunazielekeza kwa mikoa ya Kigoma na Tabora ambapo naamini mpaka katikati ya mwaka 2009 sura kamili inaweza kuwa imejitokeza. Nafurahi hata hivyo kwamba, taratibu za ujenzi wa daraja la Mto Malagarasi zimefikia hatua za mwisho.

Tunasikitika kwamba misukosuko ya mfumo wa fedha wa kimataifa umetulazimisha kuahirisha kutekeleza mpango wetu wa kupata fedha kwa kutumia hati fungani (soverign bounds) kwa ajili ya kujenga kwa kiwango cha lami barabara zetu kuu nyingi hapa nchini. Ni matumaini yetu kuwa hali ikitengemaa tutautazama upya mpango huo.

Bandari, Reli na ATCL
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka 2009 tutaendelea kufuatilia na kusimamia kwa karibu hali katika mashirika ya reli, bandari na shirika la ndege. Hali ya huduma hizo muhimu hairidhishi hata kidogo. Yapo matatizo ya uendeshaji ambayo yamesababisha huduma zitolewazo kuwa za kiwango kisichoridhisha. Tutafanya kila tuwezavyo kurekebisha mambo ili huduma hizo ziboreke na kuwafanya watumiaji kufurahi.

Mapato ya Serikali

Ndugu Wananchi;
Kama ilivyo ada mwaka ujao tutaendeleza juhudi za kuhakikisha kuwa mapato ya Serikali yanaendelea kuongezeka. Tutaendelea kuimarisha Mamlaka ya Mapato na kuziba mianya inayopoteza mapato ya Serikali.

Napenda kutumia nafasi hii, kuwapongeza sana viongozi na watumishi wa TRA kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kukusanya mapato ya Serikali. Pamoja na matatizo ya hapa na pale hali ya mapato ya Serikali imeimarika.
Mara mbili katika mwaka huu wamevunja rekodi ya ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Mara ya kwanza ilikuwa mwezi wa Juni walipokusanya shilingi 346.7 bilioni na mara ya pili ilikuwa mwezi wa Septemba walipokusanya shilingi 420.8 bilioni. Tunatambua na kuthamini juhudi zao na nakusudia kuwatunza kwa mafanikio hayo mwishoni mwa mwaka huu wa fedha.

Nidhamu ya Matumizi
Ndugu Wananchi;
Sambamba na juhudi za kuongeza na kuimarisha mapato ya Serikali hatuna budi kuhakikisha kuwa kunakuwepo na nidhamu na uaminifu katika matumizi ya fedha na rasilimali za Serikali. Nimelisisitiza sana jambo hili na kuwataka viongozi wenzangu na watumishi wa Serikali kusoma na kuzingatia maoni na mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali yaliyomo katika taarifa zake za kila mwaka.
Nimeagiza Viongozi na Watendaji Wakuu wa Wizara, Idara, Mikoa, Wilaya na Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji kusimamia kwa karibu utekelezaji wa Sheria ya Fedha na mali za Serikali na Kanuni zake. Kuna dalili za mabadiliko chanya, lakini hali bado si ya kiwango cha kutufanya tufurahi sana. Mwaka ujao tutaendelea kubanana katika jambo hili ili tufikie ufanisi unaotakiwa.

Ndugu Wananchi;
Kuanzia mwaka ujao nitawaomba wakaguzi wa mahesabu ya Serikali kumkabidhi kwenye vyombo vya sheria mtumishi wa Serikali aliyehusika na wizi au ubadhirifu mara watakapougundua. Najua utaratibu wa sasa hauko hivyo. Nataka tuutazame upya utaratibu wetu wa sasa ili isaidie kujenga nidhamu hata kama ni ya woga wa kufungwa. Itasaidia kunusuru fedha nyingi za umma zinazotumiwa isivyo.

Ni matumaini yangu pia kwamba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ataendeleza kwa kasi na nguvu zaidi kazi waliyoianza ya ukaguzi wa thamani ya fedha zilizotumiwa na kulinganisha na kazi iliyofanyika (value for money audit). Ukaguzi wa asili umekuwa unahusu uandishi wa vitabu kwa mujibu wa kanuni za fedha. Lakini, inawezekana kabisa vitabu vya hesabu vikaandikwa vizuri lakini pesa zikatumika vibaya au hata kuibiwa. Tunataka ulinganifu sawia wa fedha zilizotumika na kazi iliyofanywa.

Ndugu Wananchi;
Nimewaelekeza wenzetu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kufanya kazi kwa karibu na ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kusaidia kupambana na wasiozingatia nidhamu ya matumizi ya fedha na mali za umma hususan wezi na wabadhirifu wa fedha za umma.
Bahati nzuri Sheria ya Mwaka 2007 iliyounda PCCB mpya imetoa mamlaka ya kufanya hivyo. Nimewataka wawe wakali kwa wala rushwa kama wafanyavyo sasa, lakini pia wawe wakali kwa wale wote wanaokiuka kanuni za fedha za Serikali. Vitendo hivyo siyo tu vinaitia hasara Serikali bali pia vinapunguza uwezo wa Serikali kuwahudumia wananchi walioiweka madarakani.
Nimewataka waitumie vyema sheria mpya na fursa waliyonayo ya kuwaongezea uwezo wa rasilimali tuliyowapa kwa kutumiza ipasavyo wajibu wao. Nimewasihi pia kwamba katika kufanya hivyo wasionee wala kupendelea watu bali watende haki.

Ulinzi na Usalama
Ndugu Wananchi,
Tunaumaliza mwaka wa 2008 hali ya ulinzi na usalama wa nchi ikiwa ya kuridhisha. Mipaka ya nchi yetu ni salama na nchi ni tulivu. Hatuna budi kutoa pongeza maalum kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa kazi nzuri waliyoifanya na wanayoendelea kuifanya. Uhalifu wa makosa makubwa ya jinai kama vile mauaji, unyang’anyi wa kutumia silaha na unyang’anyi wa kutumia nguvu umepungua.
Taarifa za Januari hadi Novemba, 2008 zinaonyesha kuwa kulikuwa na matukio ya aina hiyo 8,330 ukilinganisha na matukio 10,381 katika kipindi kama hicho mwaka 2007. Huu ni ushahidi kuwa Polisi wanafanikiwa kudhibiti uhalifu, hata hivyo bado juhudi ziongezwe ili matukio ya uhalifu yapungue zaidi. Nafurahi pia kwamba hata ajali za barabarani zimepungua mwaka huu ukilinganisha na mwaka wa jana.
Mwaka wa jana kulitokea ajali 16,196 kati ya Januari na Novemba, wakati mwaka huu zimetokea ajali 5,500. Hata idadi ya watu waliopoteza maisha imepungua kutoka 2,757 mwaka 2007 hadi 1,270 mwaka huu.

Ndugu Wananchi;
Wakati tunawapongeza wadau na Jeshi la Polisi kwa maendeleo hayo bado naamini kuwa ajali za barabarani pamoja na idadi ya watu wanaopoteza maisha au kujeruhiwa na mali kuharibiwa vinaweza kupungua zaidi. Ajali nyingi za barabarani husababishwa na makosa ya madereva kutokuheshimu sheria ya usalama barabarani.
Lakini, pia kuna mchango wa Jeshi la Polisi hasa wale wa usalama barabarani kutodhibiti ipasavyo madereva wazembe. Tatizo hili lipo kwenye uwezo wa Polisi na wadau kulidhibiti.

Madereva wakubali kuzingatia na kuheshimu sheria ya usalama barabarani. Wenye magari wahakikishe wanaajiri madereva wenye sifa nzuri. Aidha, madereva wa mabasi ya abiria watambue kuwa wanabeba binadamu wenzao ambao kwa kipindi chote cha safari usalama wao uko mikononi mwao.
Makosa madogo ya dereva yanaweza kuwapotezea watu uhai au kuwapa vilema vya maisha. Lazima watambue umuhimu wa wao kuwa waangalifu. Polisi nao lazima watimize ipasavyo wajibu wao.
Polisi lazima wawe wakali kuhakikisha sheria za usalama barabarani zinafuatwa. Naamini Polisi wakiwa wakali tofauti itaonekana.

Mauaji ya Albino
Ndugu Wananchi;
Suala la mauaji ya ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi, yaani albino nimekwishalisemea mara mbili tatu mwaka huu, na mara ya mwisho wakati wa Baraza la Idd tarehe 8 Desemba, 2008. Ni mauaji na mateso ambayo hayana sababu ya kutokea kwa sababu chanzo chake ni cha kipuuzi. Imani kwamba kiungo cha albino kinampa mtu utajiri ni jambo la kijinga. Nirudie kuwasihi wenzetu hawa wanaotafuta utajiri wa haraka haraka kuwa juhudi na maarifa yao ndiyo siri ya kufanikiwa kwao na si vinginevyo. Lakini, kwa vile wapo watu wanaoamini kuwa wakipata viungo vya albino watatajirika na wapo waganga na wauwaji, Serikali haina budi kuchukua hatua za kuwabana watu wote hao na kulitokomeza kabisa tatizo hili.

Tumeunda kikosi-kazi kinachojumuisha Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa cha kuendesha mapambano haya. Hivi sasa wanaendelea na uchunguzi wa kina nchi nzima kuwatambua wahalifu na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria. Mpaka sasa watu 91 wamekamatwa na kufikishwa mahakamani na mapambano yanaendelea.

Kwa nia ya kuongeza kasi na nguvu ya mapambano haya, mapema mwaka ujao tutaendesha zoezi la kura ya maoni nchi nzima. Tutawataka wananchi wawataje watu wanaowajua kuwa wanajihusisha na mauaji au kukata viungo vya albino. Wawataje waganga wanaohusika, wauawaji wa albino, wauzaji wa viungo vya albino na wafanyabiashara wanaotumia viungo hivyo.
Taarifa hizo zitasaidia kuwafuatilia na kuwakamata watu hawa waovu. Utaratibu kama huu ulitusaidia katika mapambano dhidi ya ujambazi nchini. Naamini utasaidia kwa hili. Tunafanya matayarisho ya zoezi hilo. Wakati utakapowadia watu wataarifiwa namna ya kushiriki. Naomba ushirikiano wa hali ya juu wa wananchi wakati huo. Jitokezeni kuwataja ili isaidie kukomesha aibu hii kwa taifa letu.

Hitimisho
Ndugu Wananchi,
Tunaumaliza mwaka nchi ikiwa na sifa kubwa katika medani ya kimataifa. Uhusiano wetu na mataifa yote duniani ni mzuri. Hatuna adui. Hali kadhalika uhusiano wetu na mashirika ya kimataifa ya kisiasa na kiuchumi ni mzuri.
Nchi yetu inaheshimika na kutumainiwa katika diplomasia ya kimataifa. Tumepokea wageni wengi mashuhuri na wengine ni wa kihistoria kama ziara ya siku nne ya Rais wa Marekani, Mheshimiwa George W. Bush. Tumekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika kwa mwaka huu.
Pamoja na ugumu wake lakini tumeifanya kazi hiyo vizuri na yapo mambo kadhaa mazuri ambayo nchi yetu itakumbukwa nayo. Miongoni mwa hayo ni amani ya Kenya, kurejesha umoja wa taifa la Comoro, kuongoza vyema mijadala kuhusu masuala magumu kama yale ya uundaji wa Serikali ya Umoja wa Afrika na kuyafikisha mahali pazuri.

Mwaka 2009 nchi yetu itakabidhi uongozi wa Umoja wa Afrika kwa heshima na upendo mkubwa kutoka kwa wanachama wenzetu na mataifa mengine duniani.
Ndugu Wananchi;
Tunaumaliza mwaka nchi ikiwa tulivu. Hii inathibitisha kuwa nchi inaweza kuwa tulivu isipokuwa pale ambapo baadhi yetu tutakapokuwa tumeamua kuwa isiwe hivyo. Naomba mwaka 2009 uwe tofauti.
Tuache vitendo vya kuchochea ghasia kwa kisingizio chochote kile. Vitendo hivyo havitavumiliwa hata kidogo. Ni vizuri tukaambiana mapema tusije tukalaumiana. Naomba Watanzania wenzangu wote na hasa wanasiasa wenzangu tuyatambue hayo na tujiepushe nayo.
Naomba makundi ya kijamii yatambue ukweli huo na waache kuwaendekeza wanasiasa hasidi.

Ndugu Wananchi;
Naomba nimalize kwa kuwakushukuru kwa mara nyingine tena Watanzania wenzangu wote kwa ushirikiano wenu na uelewa wenu na msaada wenu kwangu na kwa wenzangu wote serikalini katika kipindi chote cha mwaka huu tunaouaga leo. Tumepita vipindi vya raha na vigumu kwa pamoja na tunaumaliza mwaka tukiwa wamoja na watu wenye mshikamano.
Naomba tuingie mwaka mpya na moyo huo na tuendelee hivyo.

Nitakuwa mtovu wa fadhila kama sitamshukuru Mwenyezi Mungu kwa wema na upendo wake na kutuvusha salama mwaka 2008. Tuzidi kumuomba atuongoze na kutuvusha salama mwaka ujao na miaka ijayo.
Mimi si Sheikh na wala si mwanazuoni, mimi na mfuasi tu. Lipo wazo nimekuwa napewa mara kadhaa kuwa pengine si vibaya kila mwishoni au mwanzoni mwa mwaka tungekuwa na siku ya maombi ya pamoja watu wote wote wa dini tukiongozwa na viongozi wa dini zetu kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa mwaka tulioumaliza na kuliombea taifa mema kwa mwaka unaofuata.
Ni wazo linalovutia wengi lakini sidhani kuwa ni ni jambo la kufanywa kwa amri ya Serikali. Nawaachia viongozi wa dini zetu watuongoze.

Naomba tutakiane heri na fanaka tele katika mwaka mpya, 2009.

Mungu Ibariki Afrika
Mungu Ibariki Tanzania
Ahsanteni kwa kunisiliza.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 19 mpaka sasa

  1. Wow!! Namshukuru RAIS kwa hotuba na juhudi alizonazo kwa watanzania. Lakini kwanini tunakuwa na sifa za nje huku ndani tunajiozesha? Tunakuwa kama apple lililonawiri nje na kutamanisha huku likiwa limeoza nje? Najua hali ya sasa ni ngumu saana kuikabili na itachukua muda kuisawazisha maana uozo ni mwingi na hakuna anayetaka kukiri bila kushurutishwa. Kwa maana nyingine ni mwingi zaidi ya tuonavyo na tusikiavyo kwani mpaka wavumbuliwe ndio watakiri. Sijui ni wapi Rais ataanza kushughulikia na sijui ni nani wa kumsaidia maana walio na uwezo wa kumsaidia ndio waliosababisha tuhitaji msaada huo (ndio wafujaji). Ni kweli kuwa tumemaliza mwaka nchi ikiwa na sifa japo sina hakika kama ni kutoka kwa mwananchi. Tunauhusiano mzuri na mataifa ya mbali lakini twashindwa kujenga uhusiano mwema na wenye hali ya chini. Nchi inaheshimika kidiplomasia lakini ndani ya wananchi hawaoni kikomo cha ufisadi na ufujaji. Kuna mijadala mizuri na kuunganisha Afrika ilhali watanzania hawajaungana kiuchumi kutokana na uwazi mkubwa uliopo baina yetu.
    Kuna mengi, naamini anayaona na kuyashughulikia na naamini siku yaja ambayo wenye hatia watafikishwa kutakiwako.
    Ni mtazamo wangu na naendelea kutunza haki yangu ya kukosea na kukosoloewa.
    Blessings

    ReplyDelete
  2. MISUPU SIKU NYENGINE NI BORA USOME WEWE HAYA MANENO YOE MAREFU HUKU UNAJIRIKODI KISHA TUWEKEE TUSIKILIZE MAANA SISI WENGINE TUKISOMA SANA TUNAANZA KUONA NYOTA NYOTA

    ReplyDelete
  3. Mhishimiwa Raisi asante kwa Speech ndefu mno lakini sikulaumu mana hiyo ndio kazi yako. Anyway samahani sijaisoma yote for obvious reasons mana mimi ni mama wa nyumbani and I have family to take care of sina muda wa kukaa sana kwenye komputa. Nimepitia tuu vichwa vya habari na kusoma jambo ambalo linakera wengi sasa hivi la ubadhirifu wa mali ya Ummma. In short hizo measures ambazo unataka kuchukua za kupitia vitabuni could or could not work. Tanzania tunajua rushwa imejaa mpaka inanuka kama choo cha shimo, sasa tuna uhakika gani kama hiyo ofisi ya kuratibu vitabu vya Mashirika ya Umma sasa ndioitakuwa Rushwa zoote zinatokea hapo ? Hapo baba umewapa watu dili na hivi hata mimi ningekuwa bongo ningeanza kutafutia kazi usawa huo....catch my drift ? Swala ni kwamba Ubadhirifu wa Mali ya Umma haupo tuu kwenye washika pesa za serikali kwani mimi ukinipa nishike hiyo pesa nikitaka kuila nitatafuta jinsi ya kuandika kwenye vitabu vya mahesabu na vilevile kutafuta watu wa kula nao wanaohusika na kuratibu hiyo miradi na kukagua hayo matumizi. ILI RUSHWA IISHE TANZANIA LAZIMA VIONGOZI WA SERIKALI KUANZIA ZA MITAA YAANI MTU YEYOTE ALIYEKUBALI KUWA KIONGOZI WA UMMA AKUBALI KUONDOKANA NA HULKA YA UBWANA NA KUTAMBUA KUWA UONGOZI NI UTWANA AMA UTUMWA KWA UMMA. Viongozi wetu mkishakubali kuwa nyinyi sio mabwana wa kupita na Magari makubwa na kujenga tabia ya kunyenyekea WAnanchi na kutambua kwamba mko kwenye Uongozi kwa ajili ya kutumikia Nchi basi haya yooote yatapata ufumbuzi. CHEO NI DHAMANA kama si kwa Binaadamu basi kesho kwa MUNGU tutaonana. VIONGOZI KUWENI MFANO WA KUIGWA KWA MEMA NA SI KWA MAOVU.

    Swala la pili Mheshimiwa Raisi linalokereketa sana jamii sas hivi na ambalo hukuligusia katika Speech yako ni kuhusu huu UMOJA WA AFRICA MASHARIKI. Jamani mimi nilikuwa ndio nazalia Umoja huu ulipovunjika kwa mara ya kwanza hivyo sikuushuhudia but kutokana na kufuatilia hii Second round binafsi naona hili swala si la kulichukulia mzaha. Na kwa kusema hivyo napenda kukupongeza Mheshimiwa JK kwa jitihada zako zote ulizofanya soo far za kuwalinda watanzania na nchi yetu tukufu, lakini nasema ya kuwa kwa nini tuna stall kufikia uamuzi wa once and for all kuhusu hili swala. Tunajua ya wazi kuwa hawa jirani zetu woote wametuzunguuka wanaimezea mate ya uchu ardhi yetu na hili ndio lililo muhimu katika this whole fiasco WANATAKA UMOJA KWA AJILI YA ARDHI YETU. mimi ninaishi hapa Ukerewe kwa Uhakika nimeshakaa vchini na WAganda ambao tayari wamenunua mashamba makubwa sana kwenye vijiji vya Tanzania kupitia mlango wa nyuma na wanaomba kesho sheria yetu ya ardhi ibadilike waje kupitia mlango wa mbele.Na hawa watu wana pesa kuliko iliyoibiwa EPA kwa pamoja na si wao tuu wako wengi kam Wo katika hizi nchi za EA wanaosubiri kwa hamu ardhi ya Tanzania. Na uhakika Serikali inalitambua hili , sasa swala ni kwamba mkipitisha hata robo ya hii sheria ya Umiliki wa Ardhi basi ndio DEATH SENTENCE YA VIZAZI VYETU VIJAVYO and this is for sure. Mimi naona kusolve tuu hili suala badala ya kunegotiate kwa hili ni TANZANIA ikubali kupitisha sheria ya KWAMBA ARdhi ya Tanzania ni mali ya UMMA for as long as the COUNTRY EXISTS, full stop.

    Mimi binafsi huu umoja siufagilii kabisa kwa mengi mfano mdogo last summer nimekuja Bongo nikaenda Arusha kununua TANZANITE , nilipigwa na butwaa na uchungu wa hali ya juu ulinishika nilipoambiwa kuwa idadi ninayotaka nitaipata NAIROBI na SIYO ARUSHA ? hapo ndio utajaza mwenyewe . Na haya yanaendelea Nchini Mheshimiwa Raisi.

    MUNGU IBARIKI TANZANIA UWAPE VIONGOZI NA WANANCHI MOYO WA UZALENDO mwaka 2009, Amen.

    ReplyDelete
  4. Nimepitia haraka haraka hii hotuba ya JK, lakini sikuona chochote kuhusu EPA! Je kuna sababu za kimsingi kwa nini asizungumzie EPA? Historia itamjadili vipi JK kama kiongozi hyu atashindwa kudhibiti swala la EPA?

    ReplyDelete
  5. JK tunakushukuru kwa yote mema uliyojaliwa kulitenda taifa na mataifa. Hotuba hii ni ndefu sana ila imekosa kutuwekea mambo mawili/matatu muhimu bayana kwenye medani za kitaifa na kimataifa.Nitauliza machache:

    1. Uwekezaji: umeongele vivutio, lakini hujaongelea udhibiti wa mikataba mibovu, na kuzingatia maslahi ya taifa.

    Amin amin nakuambia, ni bora madini yetu yabaki ardhini kuliko mwendo uwe kama tulio nao sasa wa kufaidisha wengine huko tukikaribia deplation.

    Tunapoteza mabilioni ya shilingi kila uchao na kuporwa rasilimali zetu kwenda kufaidisha wengine nje. Hasira yetu iko juu ya madini zaidi. Wawekezaji waje kwenye kilimo, wapewe ardhi kwa mkataba wenye ukomo, wazalishe.

    Bado tulio wengi hatuna imani na jinsi madini yetu yanavyofaidisha taifa. Abadan! Bunge letu likabidhiwe jukumu la kupitia mikataba. Hizo 10% au % zozote zisiwe kikwazo na chanzo cha usiri.

    Kumbuka, kuna deplation! Haya madini yatoweka na tutabaki na mapango bila faida linganifu. Tunaibiwa JK.

    2. Mikopo na SACCOS: Elimu juu ya biashara ndogo ndogo na ujasiriamali iko chini ya kiwango mzee. Namna ya kuendesha SACCOS na hata maana yake kwa jamii mijini na vijijini bado ni kitendawili.

    3. Tanzania kimataifa: Kwa suala la Zimbabwe ambapo ndipo jicho la dunia kwetu lilipo tumeshindwa. Kwani yule jamaa wa Comoro alikuwa mbaya kuliko Mugabe? Nonviolence strategies have already failed in and for Zimbabwe, na kilichobaki ni kuwaumiza na kuwatesa raia wasio na hatia.

    Zimbabwe ungewezesha AU imtoa yule dikteta. Mataifa/Dunia iko tayari kugharamia na tungetumia wanajeshi wetu wakalambe dume pale kisayansi. Ni sifa kubwa ambayo wananchi WOTE wa Zimbabwe wangekukumbuka nayo daima.

    4. Shukrani: Mzee Dr. Jk nimesononeka sana kwa wewe kutotambu mchango wa vyombo vya habari na vyama vya upinzani katika vita dhidi ya ufisadi ambayo tumepambana nayo mwaka uliopita. Hivi huthubutu kuwashukuru wapinzani na wanahabari hadharani? Hata kwa hili lililo wazi Dr. JK?

    Sina wasiwasi kuwa huumizi kichwa kwa sababu ya ufisadi, ila ni kwa nini umetupa wasiwasi... hutambui mchango wao?

    5: Sala ya taifa: Hapa sawa kabisa. Wengi wetu (a.k.a most of us) ni wadini (religious). Wengi wetu pia kama sio wote tunaamini sala ni silaha muhimu, na pakusanyikapo wawili au watatu, Mungu huwa kati. Shime viongozi wa dini. Hii pia itazidi kuimarisha utaifa!

    Mungu akulinde JK. Akupe hekima, akili, shauri, nguvu, elimu, ibada na uchaji wake.

    Mungu ibariki Afrika
    Mungu ibariki Tanzania

    ReplyDelete
  6. Sasa mbona JK naye anajifanya anajua sana kiswahili, Kuhami uchumi ndo maanake nini wajameni?? Halafu kama ni mtaalam wa lugha sasa kwa nini anaendelea kutumia neno albino wakati kiswahili chake kipo, whyyyyyyyyyyyyyy??? kwa niniiiii????

    ReplyDelete
  7. Nampongeza Raisi kwa kuainisha vipaombele vya mwaka ujao, 2009, ingawa karibia vyote ni vile vile ninavyosikia tangu niwe na uwezo wa kutunza kumbukumbu. Naomba yeye kama mtu ambaye mwenye madaraka ya juu katika nchi yetu aonyeshe kwa vitendo katika kufuatialia hatua madhubuti zinachukuliwa kwa wafanyakazi wanaoiba pesa za umma kama alivyowagiza PCCB na ofisi ya ACG kufanya kazi hiyo. Kimsingi bila kuwa na matumizi mazuri ya pesa zetu, ni vigumu sana kutatua kero zetu kwani miradi mingi inayotekelezwa ni chini ya kiwango kutokana na wizi wa pesa huku nchi inaongeza madeni na wananchi wanazidi kuwa masikini. Natumaini ukiwa mtu wa matendo zaidi kuliko maneno utaleta mabadiliko makubwa sana katika nyanja zote kwani PESA nyingi za umma zinapotea mikononi mwa viongozi pamoja na wahasibu katika katika ngazi mbalimbali lakini mwisho wa siku mahesabu yakuwa mazuri kwenye vitabu lakini mradi uliotekelezwa ni feki.
    MUNGU AKUPE UJASIRI KTK KUWABANA WEZI

    ReplyDelete
  8. Unaejiita mdau wa ukerewe huna lolote!!! unajifanya huna muda wa kusoma hotuba ndefu huku wewe unaandika pumbaaaaaa ndefu. Ndiyo nyie mnaopenda kutoa maelekezo badala ya kufanya, kama unauchungu na nchi yako rudi kasaidie kuijenga na siyo kuwakatisha tamaa watu wanaofanya kazi ya kuijenga tena wakiwa kwenye mazingira magumu.

    ReplyDelete
  9. Hii no mojawapo ya speech nzuri sana ambayo imetolewa na Rais wa Tanzania. JK amegusia mambo mengi sana ynayoikabili nchi yetu.

    Kwa wale mnaopenda kulaumu bila sababu nawaomba msome hii hotuba. Kama mnaona ni ndefu basi ni bora mnyamaze tu. Kumbuka hata Plato alishwahi kusema “Wise men speak because they have something to say; Fools because they have to say something.”

    Jangili

    ReplyDelete
  10. IS TOO LONG BLA BLA WE AS NORMAL TANZANIANS WE NEED TANGIBLE REAL CHANGE, WE NEED OUR LIVES TO BE CHANGE IN REAL TERMS NOT NOMINAL AND GENERALISED ONES. WE WANNA SEE INDIVIDUAL PEOPLE CHANGE THEIR PREVAILING HELL LIVES. TUNATAKA UFANYE KWELI BADILISHA MAISHA YA WATANZANIA KAMA UNATAKA KURA ZETU 2010. MICHUZI KAMA SWAHIBA WAKO JK HANA HABARI NA BLOG HII TAFADHALI MPE INAWEZA KUMSAIDIA SANA KATIKA UTENDAJI WAKE, KWANI HUMU WATU WANASEMA YA KWELI.

    ReplyDelete
  11. kiukweli watanzania itakuwa ngumu kufikia malengo kwa sababu haiwezekani kila mwaka kuna vipaumbele vitatu na zaidi. serikali ingeweka kipaumbele kimoja kila mwaka wa budget na kuhakikisha kinasimamiwa ipasavyo lakini tumekuwa kama tunatapatapa na mwishowe hatufanikiwi vyote....
    kwahiyo hiyo hotuba ya JK haina jipya na hakuna kitachofanyika.
    kitu kingine nilichonotice ni kuwa takwimu za maendeleo anazotoa utafikiri anaongea na donors sio wananchi wa kawaida, ifike mahali kuwa kuna lugha fasaha za kuongea na wananchi na sio kujibu kisayansi sana anatoa asilimia kadhaa mwananchi anataka kujua direct au indirect effect za huo ukuaji uchumi na maendeleo kulingana na mazingira yanayomkabili sasa akisema uchumi mwaka huu umepanda kwa asilimia 7.8 sio kama mwaka jana ambayo ilikuwa asilimia 7.6 inamsaidia nini mwanachi wa kawaida ambaye bado anasota na bills? hizo asilimia akaongee na donors sio sisi. Nways hongera kutimiza wajibu tu hamna unachofanya wala hatutegemei jipya toka kwako, tumechoka.

    ReplyDelete
  12. Rais anasimamia utawala bora? Mbona anawatisha wanasiasa na wanaharakati? JK acha vitisho kwa taifa nchi iongozwe kwa mujibu wa sheria zilizopo sio kwa vitisho. Usitutishe, tutasema tu na hatutafunga midomo hadi kieleweke. The regime belong to Tanzanians; the government is the agent of citizens!

    ReplyDelete
  13. VIPI RAISI HAUONI KUNA KASORO KATIKA WANANCHI KUTOKUPENDA KUFANYA KAZI ZA KUZALISHA BADALA YAKE MAKUSANYO YA KODI KUTOKANA NA BIDHAA ZINAZOINGIZWA NCHINI NDIYO KIPIMO CHA MAFANIKIO KATIKA UCHUMI WETU! HIVI WATANZANIA TUNAZALISHA NINI TUNACHOWEZA KUPELEKA NJE? WAWEKEZAJI HAWAZALISHI CHOCHOTE SANA NI UWEKEZAJI WA HUDUMA, HATUONI UWEKEZAJI WA KUJENGA VIWANDA VIKUBWA, NI WIZI MTUPU.

    ReplyDelete
  14. Wewe Anon wa 11:00 unaeniambia mimi naongea pumba , heri ya pumba zangu kuliko uozo wako. The whole point ya Michuzi kuweka maoni ni kuandika opinions zetu na kila mtu yuko entitled kwa opinion yake so don't you dare kuniambia mimi naongea pumba. And FYI kama huo Uzalendo wa U-Tz usikute mimi ninao kuliko wewe tena siku nyingine usirudie kabisa kukosa adabu kama huna cha kusema na ninahisi huna cha muhimu cha kuchangia ndio mana unaona wenzako wanaongea pumba basi na wewe weka hizo nafaka zako tuzione huna lolote. Hapa mimi naona ni mawili kama uko nje ya nchi ina maana hata hufuatilii kinaochoendelea nyumbani labda wewe mwenzetu umeukana UTanzania kwa hiyo wewe kila kitu kiko sawa kwako. na kama uko Tz na hujawahi kutoka then sikulaumu kwani upeo wako wa kuona mbali kupitia yanatendeka nchi za nje ni mdogo. Mimi nina haki ya kuyasema niliyoyasema kama Mtanzania halisi na vilevile nimebahatika kuishi nje ya nchi hivyo I can see the picture from outside. ni mzalendo ninayeipenda nchi yangu hivyo kuwa nje sio hoja na si sababu ya wewe kunitukana kwani napenda kufuatilia yanayojiri nyumbani. Na usitake kunibabaisha kuhusu kurudi Bongo nitarudi anytime for good na kusaidia kujenga Taifa nililo na uchungu nalo sana tena kukupita wewe. Kwa ufupi ni kutokana na kuishi kwangu huku Ukerewe na kuangalia muundo wa Uongozi wa hapa ndio umenisaidia kugundua kuwa Viongozi wetu walio wengi wa Tanzania (sio wote ) lakini asilimia kubwa once wakipata cheo wanafikiri wako pale kula pesa za nchi na kuitwa "Mzee" na "Mheshimiwa" na kuogopewa yaani mtu asiwaguse wanakuwa untouchables na kusahau kuwa wao ni WATWANA na si MABWANA wa UMMA. Hii hulka ni mbaya na haipo nchi zilizoendelea. Hapa Ukerewe kwa mfano kama ni Mbunge mpaka siku anaondoka madarakani ni anatumikia wananchi tena kwa kunyenyekea kama umempelekea malalamiko atakutafuta yeye prsonally mpaka ahakikishe kapatia ufumbuzi shida yako sijui mayb ni kwa sababu hawaitwi Mzee au Mheshimiwa huku ni mambo ya first name tuu but still heshima yao iko pale pale na hawaogopwi na kwangu mimi hii ndio Demokrasia ya kweli.Tanzania hata ukiongea na "Mheshimiwa" ukasema kitu kwa bahati mbaya vibaya basi unaweza ukajikuta lupango kwa masaa kadhaa na hii ni udikteta na heshima ya woga ambayo ndio inawapa power viongozi kusahau kuwa kura za wananchi ndio ziliwaweka pale na hivyo wana dhamana ya wananchi.

    Na kuhusu hilo swala la EA Community tuulize sisi tunaoishi ndani ya Uingereza ya sasa na ya zamani kabla ya European Union jinsi Maisha ya mwananchi wa kawaida yalivyobadilika.Natoa mfano tuu hapa kwani Eu na EA ni kitu kimoja muungano wa nchi tofauti zenye lengo moja ingawa Eu ni kubwa sana. Anyway Kabla ya EU Mzawa wa Ukerewe alikuwa anatuona sisi watu weusi woote hatuna mpango lakini sas hivi sisi ndio tumekuwa marafiki zao na wanawaona hao wa eastern europe mbao ni wazungu wenzao walioingizwa na EU ni wabaya kwa jinsi huu wananchi wa nchi za Europe walivyoharibu maisha ya mwananchi wa kawaida, hamna kazi , wizi umezidi, gangs kila kona, priorities zote serikalini za nyumba wanapewa wao n.k. mambo ambayo yamebadilika baada ya kujiunga na Umoja wa nchi tofauti.

    Mimi sikuwa nawakandia Viongozi I was simply voicing my opinion which I have a right to kama Mdau wa Blogu hii and you as well are entitled to yours so next time kabla hujayaita mawazo yangu pumba toa nafaka zako kwanza ndio uongee pumba weeeeeeee

    ReplyDelete
  15. Salamu muafaka kutoka kwa mkuu wa nchi. Inafurahisha kusikia kwamba Rais anatukumbusha kale kawimbo ketu ka toka miaka ya sitini kwamba 'kilimo ndio uti wa mgongo wa uchumi wetu' na kwa hiyo kinapewa kipaumbele cha kwanza!!!! ningemwamini rais wetu mpendwa kuwa anayosema si usanii kama angaa ningesikia anatamka bayana mkakati wa huo ukipaumbele. Kwa mfano ningesikia kuwa katika mwaka 2009 serikali itasitisha kwa muda uagizaji wa mashangingi, na badala yake fedha za kununua mashangingi zitaelekezwa kununua matrekta ambayo yatakopeshwa kwa vyama vya ushirika au ofisi za wilaya, ili yatumike kuleta mageuzi katika kilimo, yaani tuanze na hatua za kuondokana na kilimo cha jembe la mkono, kifaa kilichogunduliwa hata kabla ya Yesu kuzaliwa na leo hii kimeendelea kuwa ndio zana kuu ya 'uti wa mgongo wa uchumi wa bongo'!!!!! Vinginevyo hii hotuba ni sawa na salamu zile zile tunazosikia kila mwaka: "HAPPY NEW YEAR!!!"

    ReplyDelete
  16. Mimi nimeifurahia Hotuba hii kwa kuwa inagusa na kuainisha maeneo muhimu na ambayo inabidi yafanyiwe kazi.

    Tatizo ninaloliona hapa ni kuwa Rais hajaainisha viwango vyovyote vya malengo(Targets) katika maeneo hayo ili mwakani tuweze kuyapima kwa takwimu na sio maneno. Kwa mfano kwenye elimu angesema ni kwa kiwango gani anataka vijana wafaulu sema 70% na katika kilimo pia angetaja kabisa yeye anataka uzalishaji uongezeke kiasi gani, au tupunguze kununua chakula kutoka nje kwa kiasi gani.

    Nasema hivi kwa kuwa sijaona kama anao mawaziri wenye fikra na kwa kuwa hajasema viwango basi na wao wataendeleza maneno ilimradi bora liende kama ilivyozoeleka. Tumekuwa na tatizo kubwa la kifikra miongoni mwa viongozi wetu wa juu hawa na wengi wamekuwa wakisubiri Rais aseme ndio waanze kupiga debe sijawahi hata siku moja kumsikia Waziri anaainisha mawazo yake binafsi(muono wake-vision) na jinsi anavyokusudia kutekeleza sera ili aweze kufikia malengo(policy speech).
    Kwa mfano kuna Waziri alipewaga kazi ya Ardhi na Maendeleo mjini yeye akawa kila siku anapiga kelele kuhusu viwanja na Shirika la Nyumba?!! Akatolewa akapewa nyingine sasa sijui atapiga kelele kuhusu majosho??!!

    Bwana JMK inabidi awape maelekezo kamili mawaziri wake yenye malengo maalumu na yenye viwango ili wakishindwa kutekeleza kieleweke maana wakati wa kuzunguka na mashangingi yetu bila utekelezaji wa kazi uishe.
    Bwana Raisi pia hakugusa maswala kadhaa:
    1. ELIMU YA JUU
    2. UBORA WA ELIMU
    3. MAKAZI NA MIPANGO MIJI
    4. MAKTABA ZA UMMA WILAYANI-Kujisomea(Nilishtuka sana juzijuzi kuona kuwa maktaba moja ya bure katika Kata moja hapa Uingereza ilianzishwa mwaka 1880)

    Haya ni maeneo yanayoturudisha nyuma sana na inabidi yaangaliwe kwa undani.
    Ila kwa ujumla hotuba ni nzuri ila watekelezaji wako wapi??? Raisi naona kwa hili aanzishe Perfomance Contract kwa wakubwa wote anaowateua.

    Mungu Ibariki Tanzania,
    Mungu Iokoe Tanzania,
    Mzawa

    ReplyDelete
  17. KWA KWELI HII HOTUBA IMENIGUSA KWENYE PATO LA SERIKALI AMBALO JUNI NI 346.7 BILLIONI NA SEPTEMBA 420.8 BILLIONI,SWALI LANGU JEE KAMA KUNA PATO KAMA HILI KWA NINI BADO TANZANIA TUNA MATATIZO YA MAJI NA KWA NINI BADO SEHEMU KAMA MANZESE WANATUMIA VYOO VYA SHIMO???? NCHI INA PESA NA MVUA ZIKINYESHA WATU WANAKUFA NA KIPINDUPINDU??? AU HILO PATO WANAWEKA BOT ILI WAKUBWA NA WAJANJA WACHUKUE BADALA YA PATO LA SERIKALI KUNUFAISHA WANANCHI.
    TANZANIA BADO HAIJABADILIKA KWENYE SUALA LA KUJALI WANANCHI WAKE!!!HII INAONESHA WAZI KUTOKANA NA MASIKINI KUWA WENGI NA MATAJIRI KIDOGO.SHAME.
    MUNGU INUSURU TANZANIA NA KIPINDUPINDU!!MAANA KIKITOKEA KULE KWENY VYOO VYA SHIMO, WAGONJWA WAKIENDA HOSPITALI WATAAMBIWA DAWA HAKUNA NA ZILIZOKUWEPO NI DAWA FEKI AMBAZO ZITAWAUWA. SO AS TANZANIAN AM I SUPPOSE TO BE PROUD OF THIS SPEECH.HELL NO.NAJUA HILO PATO LA SERIKALI LITAISHIA KULIWA NA WACHACHE BADALA YA KUNUFAISHA MASIKINI WALIO WENGI.
    MUNGU IBARIKI TANZANIA.

    ReplyDelete
  18. wee unaejiita mdau wa ukerewe unatutia kichefuchefu na comments zako ndefu bwana hadi na sie wengine tukwambie ndio ujue kuwa unaboa hapa eti mwenyewe unasema kabisa hukuisoma hotuba yote kwavile huna muda sasa umeupatia wapi huo muda wa kuandika mgazeti wote huo au ulitaka wadau wakusome wewe wasimsome jk?IF U DON HAVE SOMETHIN 2SAY IS BETTER TO LISTEN THAN KUROPOKWA KAMA ULIEKUNYWA MAJI YA CHOONI VILE. :NB mdau hapo juu u made my day kuwa JEMBE LA MKONO TANGIA ENZI ZA YESU LILISHAKUWEPO DUH lol

    ReplyDelete
  19. EAST AFRICA NA ARDHI YETU WATANZANIA,,,,yan ni ivi ardhi ni ya umma wa Tz na no kubadilisha sheria hii kwa yoyote tulompa dhaman ya kutuwakilisha huko,,,patakua hapatoshi apa bongoland mkiiuza ardhi yetu kwa jiranizzz,,,hapa tu ndo pananikera na sipataki kbs,,acha tuungane bt no ardhi na ajira

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...