Jukwaa kuu huwa hapatoshi wakati wa tamasha
Mtanange wa sita wa tamasha la Sauti za Busara ambalo hufanyika Zanzibar kila mwaka itakuwa ni kuanzia tarehe 12 hadi 17 Februari 2009; hakutakuwa na kiingilio kwa watakaoingia kabla ya machweo.

Sauti za Busara ni tamasha la kimataifa ambalo linautambulisha na kuutangaza muziki wa Afrika Mashariki, na ambalo hufanyika katika kila wiki ya pili ya mwezi wa Februari kila mwaka kisiwani Zanzibar.

Likionyesha wasanii maarufu na wanaochipukia na waliofanyiwa uteuzi makini zaidi ya 400 (vikundi 40 kwa jumla), Sauti za Busara imeweza kuthibitisha kuwa ni tukio kubwa na bora zaidi la muziki hapa Afrika mashariki, ni tukio linalowaunganisha watu katika mazingira ya kusherehekea.

gwaride la ufunguzi likipita mitaa ya mji mkongwe wa mawe

Wasanii watakaoshiriki
Samba Mapangala & Orchestre Virunga (DRC / Kenya), Natacha Atlas (Egypt / UK), Msondo Ngoma Band (Tanzania), Oudaden (Morocco), Nawal (Comoros / France), Joh Makini (Tanzania), TY (UK), Jagwa Music (Tanzania), Segere Original (Tanzania), Katapila ‘Sangula’ Ngoma (Tanzania), Culture Musical Club (Zanzibar), Khethi with Kibo Sounds (South Africa / Tanzania), The Moreira Project (South Africa), Elemotho (Namibia), Mamillion (South Africa), Comrade Fatso and Chabvondoka (Zimbabwe), Mohamed Ilyas & Nyota Zameremeta (Zanzibar), Bi Kidude (Zanzibar), Wahapahapa Band (Tanzania), Carola Kinasha & Shada (Tanzania), Mutinda (Kenya), Sansa Troupe (Uganda), Best of WaPi (Pan Africa), Swahili Encounters Group (Various), Iddi Achien'g (Kenya), Rachel Magoola (Uganda), Omega Bugembe Okello (Uganda / USA), Safar (Zanzibar), Kiumbizi (Pemba), Zinduka Ngoma (Zanzibar), Jang’ombe Nursery School (Zanzibar), Tarbia (Zanzibar), Zimamoto (Zanzibar), DJ Side (Zanzibar), DJ Yusuf (UK / Zanzibar), na wengineo wengi.

Tunasikia fahari kutangaza kwamba Samba Mapangala (pichani) amethibitisha kushiriki akiambatana na bendi yake ya Orchestre Virunga. Kwa hakika yeye ni mmoja wa wasanii mahiri na wanaopendwa sana hapa Afrika Mashariki. Katika muda wa miaka 25 ameweza kutamba na vibao mbalimbali, vikiwemo Virunga, Ahmed Sabit, Vunja Mifupa, Sungura, Vidonge, Dunia Tunapita na Nyama Choma.

Burudani kutoka Afrika chini ya anga

Kuanzia siku ya Alhamisi mpaka Jumapili, kutakuwa na burudani ya vikundi kumi kila siku. Wasanii wakubwa wataonyeshana kazi na wale wanaochipukia. Kwa pamoja tuna mseto wa vikundi thelathini kutoka Zanzibar, Tanzania bara na Afrika Mashariki. Vikundi hivi ni mchanganyiko wa vile vya muziki wa asili, vionjo mchanganyiko na ule wa kileo. Vilevile kuna vikundi vingine kumi kutoka Komoro, Zimbabwe, Afrika Kusini, Namibia, DRC, Morocco, Misri, Nigeria na Uingereza.
Mtiririko wa maonyesho ya muziki ni wa “Bandika Bandua” yaani ni onyesho moja baada ya lingine. Maonyesho yote huanza wakati wa jioni, muda ambao joto la jua linapoanza kupungua, mara nyingi kundi la mwisho hupanda stejini nyakati za saa sita ya usiku.


Jukwaa kuu
Jukwaa kuu la burudani lipo eneo la Mji Mkongwe, ndani ya ukumbi wa kihistoria wa Ngome Kongwe (upande wenye majani) na juu upo wazi. Kipindi cha tamasha ukumbi huu hupambwa kwa rangi mbalimbali, na pia kunakuwa na vibanda ishirini kwa ajili ya huduma za vinywaji, chakula, uuzaji wa nguo, bidhaa za kisanii, pamoja na kanda na CD za wanamuziki mbalimbali.
Pirika pirika ni nyingi kila siku ya tamasha ndani ya ukumbi huu, wenyeji na wageni wa rika, tamaduni na jinsia mbalimbali hujazana kwa wingi. Muda wa jioni kunakuwa na watoto na familia nyingi katika hali ya furaha na bashasha, wadau mbalimbali wa sanaa na utamaduni kutoka kona mbalimbali hubadilishana mawazo. Giza linapoingia wapenda muziki nao hujifaragua na kujirusha kutokana na mirindimo ya muziki na burudani mahiri.


Kila mtu anakubali kwamba kipindi nyoyo ya kila mhudhuriaji hukongwa kutokana na mandhari ya tamasha, na Sauti za Busara huthibitisha kuwa ni “tamasha rafiki zaidi duniani!”
Tiketi na viingilio
Kiingilio ni bure kila siku kuanzia saa kumi jioni hadi machweo. Baada ya hapo utahitajika kuwa na
tiketi au pasi maalum ya kuingilia. Bei zinatofautiana baina ya wageni, wakaazi na. Kwa wanaopendelea kukaa kwenye viti kuna tiketi maalum za VIP.
Sherehe ya kumalizia tamasha
Siku ya mwisho wafanyakazi wa tamasha, baadhi ya wasanii na wale wote wanaopenda kwa pamoja tutaelekea katika moja ya fukwe murua Zanzibar. Huko kutakuwa na ma-DJ, wacheza sarakasi, vikundi mbalimbali vya muziki na hivi ndivyo tutakavyohitimisha karamu yetu kwa mwaka 2009.
Shughuli hii imepangwa kufanyika siku ya Jumanne tarehe 17 Februari,
Kendwa Rocks.
Kumbuka kuwa, siyo sisi pekee. Zanzibar ina maeneo mengine mengi ambako matukio kedekede hufanyika kwa mfano katika mahoteli, migahawa na kumbi mbalimbalii. Hii tumeibatiza jina la “Busara Xtra” na tutafanya kila jitihada kukufahamisha yale yote yatakayojiri.
KWA HABARI KAMILI
NA




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. Hi kaka michuzi, mi nauliza ni kwa nini hii habari imetoa majina ya vikundi vitakavyoshiriki, na kwenye mabano imetofautisha Tanzania na Zanzibar mfano Carol Kinasha (Tanzania) bi kidude (Zanzibar) naona kama si sahihi maana Tanzania inainclude Zanzibar. si bora waseme Tanzania Bara na Tanzania Visiwani? inaonyesha kama zanzibar si Tanzania, kumbukeni kuwa jina la Tanzania limetokana na Tanganyika (TAN) na Zanzibar (ZAN) then ikaongezewa IA..Asante ni maoni tu

    ReplyDelete
  2. yeah zanzibar sio Tanzania...umesema mwenyeo Tanzania ni TAN ZAN na NIA sasa kweli zanzibar = TAN ZAN NIA?
    na kwa nini kuitwe tanzania visiwani wakati jina lake lipo na linajulikana kua ni zanzibar...haijalishi kama kuna tanzania or tanzania bara or tanganyika or whatever zanzibar ni zanzibar musituchanganye na siasa zenu za 1 + 1 = 1..

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...