washtakiwa watatu walioachiwa huru wakitoka Mahakama Kuu leo
story kamili nenda http://www.dailynews.co.tz/
umati wa watu ukiondoka mahakama kuu baada ya Abdalah Zombe na wenzie 9 kurejeshwa rumande baad ya kuonekana wana kesi ya kujibu.
Washtakiwa watatu katika kesi ya mauaji inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Abdalah Zombe na wenzake 12 wameachiwa huru mchana huu baaada ya kuonekana hawana kesi ya kujibu.

Washtakiwa hao ambao waliondoka mahakama kuu wakiwa watu huru ni mshtakiwa namba 4 Konstebo Noel Leonard, mshtakiwa namba 6 Koplo Nyengelera Morris na mshtakiwa namba 8 Koplo Felix Cedrick.
Kesi imeahirishwa hadi kesho ambapo washtakiwa wataanza utetezi baada ya kula kiapo kilichoshindikana kuliwa leo. Akitoka mahakamani na kupanda karandinga, Zombe alisikika akisema mambo yote kesho na kwamba nchi inaendeshwa kwa utawala wa sheria.
Wiki iliyopita, mawakili wa pande zote walijenga hoja kuishawishi mahakama kukubaliana na maoni yao, baada ya upande wa mashitaka kumaliza kutoa ushahidi wao.
Wakati upande wa mashitaka unasisitiza kuwa Zombe na wenzake wana kesi ya kujibu, upande wa utetezi unadai hakuna ushahidi mzito unaowafanya washitakiwa hao wasimame kizimbani kujitetea.

Zombe na wenzake wanashitakiwa kwa mauaji ya Wafanyabiashara wanne ambao ni Ephrahim Chigumbi, Sabinus Chigumbi ‘Jongo’, Mathias Lunkombe na Juma Ndugu, ambaye alikuwa dereva wa teksi iliyokuwa ikitumiwa na wafanyabiashara hao katika shughuli zao.

Washitakiwa wengine katika kesi hiyo namba 26/2006 ni Mrakibu wa Polisi Christopher Bageni, Mrakibu Msaidizi wa Polisi Ahmed Makele, WP. 4593 Konstebo Jane Andrew na D. 1406 Koplo Emmanuel Mabula.

Wengine ni D. 8289 Konstebo Michael Shonza, D. 2300 Koplo Abeneth Saro, D 9321 D/C. Rashid Lema, D. 4656 D/Koplo Rajab Bakari na D. 1367 D/Koplo Festus Gwabisabi.
Wanadaiwa kutenda kosa hilo Januari 14, 2006 katika msitu wa Pande nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam. Washitakiwa walikana mashitaka hayo na wameendelea kuwa rumande tangu kesi hiyo ifikishwe mahakamani kwa mara ya kwanza Juni, 2006.
Inadaiwa kuwa siku wanayotuhumiwa kufanya mauaji hayo, washitakiwa waliwakamata wafanyabiashara hao na dereva bila vikwazo vyovyote katika maeneo ya Sinza Palestina.

Kwa mujibu wa upande wa mashitaka, askari hao walidai kuwa marehemu hao walikuwa majambazi, wakati haikuwa kweli. Upande wa mashitaka unadai watu hao walikuja jijini kutafuta soko la madini waliyokuwa nayo.
Wakati wanakamatwa, wafanyabiashara hao walikuwa na kiwango kikubwa cha madini na fedha nyingi baada ya kuuza baadhi ya madini kwa mfanyabiashara mwingine Arusha ambako walikwenda kupeleka watoto wao shuleni.

Inadaiwa kuwa washitakiwa wote kwa pamoja, walipanga mauaji hayo na baadaye kuhusisha tukio hilo na matukio mengine ya wizi wa kutumia silaha kwenye Kampuni ya Bidco na Al-Mar Jewellers Kariakoo ili kujaribu kujipatia madini na fedha za wafanyabiashara hao.

Upande wa mashitaka unadai pia kuwa askari walitekeleza mauaji hayo kwa kupokea amri kutoka kwa Zombe kwa usimamizi wa karibu wa Bageni na Makele.
Inadaiwa pia kuwa washitakiwa (isipokuwa Zombe) waliwachukua marehemu hao hadi kwenye msitu wa Pande na kuwapiga risasi huku wakiwa wamewalaza kifudifudi. Baada ya mauaji hayo, washitakiwa wanadaiwa kukutana katika Kituo cha Polisi cha Urafiki ambapo waligawana pesa na vitu vingine wanavyodaiwa kuchukua kutoka kwa wafanyabiashara waliouawa.

Kesi hiyo ilianza kusikilizwa Mei 27 mwaka jana na upande wa mashitaka katika kuthibitisha makosa ya mauaji yanayowakabili washitakiwa hao ulipeleka mashahidi 37.

Ushahidi wao ndiyo unaufanya upande wa mashitaka kuishawishi mahakama ione kuwa washitakiwa wote wana kesi ya kujibu kwa vile ndiyo walioshiriki kuwakamata washitakiwa na baadaye wakapatikana wameuawa.

Suala la marehemu kuuawa kwa risasi halina ubishi, ila swali la msingi ambalo mahakama inalazimika kujiuliza kabla ya kutoa uamuzi wake ni kama washitakiwa ndiyo walioshiriki kuwaua marehemu hao.

Jambo lingine la kujiuliza katika kesi hiyo ni kama mauaji hayo yalifanywa wakati washitakiwa wote wakiwa na nia moja ovu ya kuua au walifanya hivyo kwa bahati mbaya.

Katika kujenga kesi yao, upande wa mashitaka unadai ushahidi kadhaa unaonyesha kuwa washitakiwa ndiyo walioshiriki kuwaua wafanyabiashara hao kwani waliwakamata bila mapigano yoyote Sinza.

Upande wa mashitaka unadai kuwa washitakiwa walikuwa na nia ovu ya kuwaua washitakiwa hao kwani baada ya kutimiza kitendo hicho, waligawana fedha ambazo walikutwa nazo marehemu hao.

Lakini upande wa utetezi unadai hakuna shahidi aliyeshuhudia kama washitakiwa ndiyo waliofyatua risasi kuwaua marehemu, ila ushahidi wote ni wa kimazingira na wa kusikia.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Toka 2006 mpaka 2009 bado ushahidi, Nahisi ata UFISADI utaishia hivyo hivyo ,ushaidi autoshi

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...