UTAPELI WA VIWANJA NA MASHAMBA BAGAMOYO

Tafadhali kuwa mwangalifu hii habari ni ya kweli chukua tahadhari!


Mzee aliyejitambulisha kwa jina la Mzee Mohamed Said mkazi wa Tegeta jijini Dar es salaam, alikiri kushiriki kwenye zoezi la kutapeli mashamba ya Bagamoyo na hali yeye si mkazi wa huko. Hapo alikuwa kwenye Ofisi ya Serikali ya Kijiji, Kijiji cha Kiharaka, Wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani.


Michuzi tunaomba uturushie hii ili watu wawe makini wanapotaka kununua viwanja na mashamba huko Bagamoyo - Mkoa wa Pwani.

Serikali kwa sasa imekabidhi madaraka ya ugawaji wa ardhi na umilikishwaji ardhi kwenye jamii ya sehemu ambazo ardhi hizo zipo. Zoezi hili hufanywa na serikali ya kijiji ambayo hukagua maeneo ya mapori ambayo ni salama kwa shughuli za binadamu na kugawa kwa wanavijij kwa ajili ya kilimo au kama vitega uchumi. Hicho ni kitendo cha kiungwana kabisa lakini kuna watu ambao sio waaminifu wanataka kutia dosari zoezi hilo.

Hivi majuzi tulitembelea maeneo ya Mbweni Dar e salaam tukiwa tunatafuta eneo la kujenga shule ya bweni. Tuliambiwa kwamba pia huko Bagamoyo kuna maeneo yanauzwa na wanavijiji kwa ajili ya kuleta maendeleo kama shule n.k. na hakuna usumbufu kabisa hivyo tujaribu pia huko.
Tulijikusanya na tukafunga safari hadi nje kidogo ya Mbweni kuingia Bagamoyo. Hapo tulitambulishwa kwa kijana anayejulikana kwa jina moja tu na Hussein anayedai kuwa yeye ni mwenyeji wa hayo maeneo na anawafahamu watu wengi sana wa huko.
Kijana huyo alitueleza ya kwamba yeye na vijana wenzake wa Kijiji cha Kiharaka, wameji-organize na wameamua kuuza kwa pamoja baadhi ya eneo la ardhi (pori) waliyopewa na serikali ya kijiji. Hivyo basi kila kijana ana sehemu yake. Na wao kwa pamoja wameamua kutenga heka 15 na wanauza heka shs 200,000 Hivyo tutauziwa heka 15 kwa 3m.
Eneo hili lilikuwa zuri na lilituvutia watu wote tuliofika hapo. Tulikubaliana kwamba tutafanya maamuzi baada ya kujadiliana na wenzetu (wa kikundi chetu na wanasheria wetu) na tutawajulisha kwa njia ya simu kama tutakuja kununua au vipi. Tulifurahi sana kwa "ofa" hiyo na kuahidi kurudi tena baada ya wiki moja kwa majadiliano zaidi na wahusika.

Tulirudi mjini na kushauriana kwenye kikundi chetu na kugawana majukumu. Mmoja alishughulikia kuhakiki ofa tuliyopewa, mwingine alifuatilia taratibu za kununua maeneo kama hayo kutoka kwenye serikali ya kijiji, na wengine walifuatilia sheria ya kujenga maeneo ya pwani kule makao makuu ya wizara ya ardhi.
Woga wetu ilikuwa ni kutapeliwa na kuuziwa sehemu ambayo haijatengwa kwa makazi n.k. Tulishauriwa kuwa tukitaka kununua eneo hilo tuwaone watu wafuatao: kamati ya ardhi ya kijiji, serikali ya kijiji, mwenyekiti na katibu, mtendaji wa kijiji(anakuwa ameajiriwa na serikali), au afisa ardhi wa wilalya

Lakini muhimu pia tuliambiwa tukiwa tunaenda kufanya manunuizi tuwaone pia hao wenye hivyo vipande na makaratasi yao yawe yanatambulika wizarani. Tulimuomba kijana aitwaye Simon ambaye ni mjumbe wa kamati ya kiiji cha Kiharaka Wilayani Bagamoyo aende Mchanga wa Hela kutafuta hili pori ambalo vijana hawa "hodari" walikuwa wanataka kutuuzia kwa ajili ya shule.
Huyo Simon alitueleza kwamba hawafahamu sana watu wa maeneo ya Mchanga wa Hela ila yuko kwenye kamati ya kijiji na atawauliza wenzie pia. Baadae alituambiwa kwa simu kwamba maeneo kama hayo yapo lakini hili haswa hana hakika nalo na hata wenzake pia hawakuwa na taarifa nalo. Alishauri kwamba siku ya kuonana na wamiliki na mwakilishi wao Mzee Mohamed, tukutane Ofisi ya Serikali y aKiji na hapo watakuwepo watu kuwatambua kweli kama hawa ni wahusika halali au la.

Tulifanya utafiti wote huu kwa muda wa wiki moja na wakati huu wote tulisumbuliwa sana na simu za yule kijana (dalali) Hussein ambaye wakati huo alitu-introduce kwa Mzee Mohamed Said aliyedai kuwa yeye ndio Mzee wao, na pia anatambulika na serikali ya Kijiji.
Mzee huyo alikuwa akimpigia simu mmoja wetu kila siku na kumlazimisha aje kutoa hela maana kuna watu wengine wanataka kununua kwa laki tatu kwa heka, na sisi ni wa laki 2 kwa heka. Kwa kweli zile simu zilimfanya mmoja wetu kutaka kufanya maamuzi ya haraka, kwamba atatoa hela yake mfukoni anunue ili kuishika hiyo ofa wakati sisi kama kikundi tukifuatilia process ya kuthibitisha. Lakini Mungu alisaidia na hakufikia uamuzi huo japo ni wazo alikuwa nalo baada ya kuona simu zinamsumbua.

Wiki moja baadae tulijipanga upya na kurudi Bagamoyo. Tulienda na wawakilishi wengine ambao hawakupata nafasi ya kuliona shamba wiki ya kwanza. Ni mahali pazuri sana na tulifanya maamuzi tukatoe hela benki na kununua. Eneo hilo liko karibu na bahari, na ni dakika 15-20 kutoka barabara kubwa ya Bagamoyo, kuna maji ila umeme hakuna. Hapo karibu kuna shule ya Mapinga, Kanisa la pentecostal na huduma nyingine kadhaa.

Tulipompigia simu Hussein kwamba tuko njiani, alidai ya kuwa tuendelee tu na Mzee Mohamed Said kwani yeye alikuwa anaenda shambani kwa bibi yake kulima. Tulianza kuingiwa hofu kwani kijana huyu tuko nae kila siku, na tulimwambia kama tutakuja ili awatayaarishe wale vijana wenzie wote kama wamiliki halali wa shamba hilo. Sasa yeye anatuambia anaenda kulima siku ambayo "muhimu" kukamilisha manunuzi. Basi tukawasiliana na Mzee Mohamed naye akawa nasi kwenye gari tukielekea shambani.

Huku nyuma Simon tuliyemtuma (bila Mzee Mohamed wala kijana Husein kujua) alitueleza kwamba tusifanye manunuzi yoyote hadi twende na huyo muuzaji kwenye ofisi ya serikali ya kijiji. Tulimpigia simu na kumwambia tuko na Mzee Mohamed na hivyo yeye aje ofisini tukutane hapo. Tulichoshangaa ni kwamba Mzee Mohamed alitupoteza sana.
Tulizunguka kwa masaa mawili tukitafuta shamba ambalo mwanzoni alisema yeye analijua sana. Hakutaka tuende serikali ya kijiji kabisa na badala yake alikuwa anatupeleka kwa baadhi ya watu palepale kijijini akidai ya kwamba wanamjua sana yeye lakini walikuwa kwenye baraza la zamani.

Hatimaye alitupeleka kwa kijana aitwaye Doto. Doto alikiri kweli kuna pori ambalo wameahidiwa kupewa lakini sio kwa kuuza, na hata kama ni kuuza sio kwa bei hiyo ndogo ya Hussein na Mzee Mohamed Said. Pia hawana karatasi zozote za kumilikishwa, isitoshe hamfahamu mzee yule. Ndipo tulipomuomba Doto atufikishe katika hiyo ofisi ya kijiji tukiwa na Mzee Mohamed.
Tulipofika ofisini tulilakiwa na mtendaji, mjumbe Simon (ambaye alishajua ni utapeli na akawaarifu polisi na mpelelezi) na polisi. Baada ya kuwaeleza yaliyojiri walimkamata huyo mzee na kumuweka chini ya ulinzi. Na hapo mtendaji alituambia hivi karibuni kuna prof wa sheria chuo kikuu mlimani ametapeliwa milioni kumi na tano kwa kuuziwa shamba na matapeli na walishangaa kwa nini sisi mpaka tunafika hapo ofisini tulikuwa hatujalizwa bado!
Pia alieleza matapeli hao wanatumia ushirikina sana,na mpaka sasa kuna kesi nyingi zipo mahakamani...kwa kifupi shamba halikuwepo, lile eneo tuliloonyeshwa tukalipenda sana na kudanganywa heka 15 ni za vijana ni mali ya KIJICO na eneo ni kubwa sana na ndio maana mara zote mbili tulizotembelea huko hatukuwakuta vijana (waodaiwa kuwa wenye eneo) kwenye eneo hilo.
Shamba la KIJICO liko maeneo ya Mchango wa hela kijijini hapo. Baada ya Shmba hilo ambalo kuna vibao mwanzo na mwisho vinavyosema KIJICO, kuna barabara ambayo inatokezea mapinga. Japo vibao vilikuwepo lakini kama sio mwenyeji wa kule si rahisi kujua shamba hilo mwanzo wake wala mwisho wake. Na madalali hawa matapeli hutumia njia za vichochoro na kuzunguka ili kupoteza muda na lengo msielewe mnapoenda wala mlikotoka.

Pale ofisini hatukumkuta Mwneyekiti wala Katibu, ila Mtendaji Rajabu Mbega alikuwepo na alitupa ushirikiano mkubwa mno, tunamshukuru sana Bwana Rajabu ambaye alitushauri nini cha kufanya. Akiwa chini ya ulinzi Mzee Mohamed alikiri ya kuwa yeye alikuwa anajitafutia riziki tu, hivyo tumsamehe bure. Lakini pia alieleza yeye ni mwenyeji wa Tegeta na wala si wa kijijini hapo. Mzee Mohamed( pichani) anatumiwa na matapeli wa huko kwa sababu ya umri wake huwezi kudhania ni tapeli.
Ana simu modern kabisa Nokia Nseries sijui ni yangapi, na kauli zake ni za hekima huwezi kufikiria ni tapeli kabisa. Tulimuacha mikononi mwa vyombo vya usalama, tukaondoka kijijini hapo kurudi majumbani kwetu.

Jihadhari sana, siku nyingine itakuwa
kwako na pengine hautakuwa na bahati ya kunusurika.
habari ndiyo hiyo!!

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 6 mpaka sasa

  1. duh hii kali sasa.kama huyo mzee kakamatwa mpelekeni kune vyombo vya sheria sio kukaa mnamaindi simu au mazagaza ya watuhumiwa.au mshamuibia kiserula chake mdingi wa watu jamani.wajinga na washamba mtaendelea kulizwa tu hadi kieleweke .bongo raha sanaa yaani.

    faza mithupu bongo lini au umependa vekesheni twa kusubiria kwa hamu sana ndani ya jiji

    ReplyDelete
  2. Michuzi, hii imekaaje. Naomba uulize wadau hasa serikalini!...Huu uwanja kama unajengwa upande wa Kenya, ndio mabao ya utalii yanaendelea...Bado najiuliza, hii jumuia ya afrika mashariki ina manufaa makubwa kwa tanzania ukilinganisha na wenzetu??

    ******************

    Uwanja wa ndege wa kisasa unatarajiwa kujengwa mpakani mwa Tanzania na Kenya katika maeneo ya Holili na Taveta kama njia ya kuimarisha utalii na kukuza biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki.

    Balozi wa Kenya nchini, Mutinda Mutiso, alisema hayo wakati juzi akizungumza na wawekezaji na wadau mbalimbali mjini hapa juzi usiku.

    Mutiso alisema uwanja huo utajengwa kilomita saba kutoka Holili kuelekea Taveta nchini Kenya.



    “Zabuni imekwishatolewa kwa Serikali ya Kenya ili kumpata mkandarasi mahiri atakayejenga uwanja huo,” alisema.

    Alisema uwanja huo ambao umepangwa kugharimu Sh. bilioni 10 za Kenya, utafungua milango na kuvuta watalii wengi katika ukanda huo.

    Aliongeza kuwa awamu ya kwanza ya mradi wa ujenzi wa kiwanja hicho, inatazamiwa kumalizika miaka miwili ijayo na ya pili itachukua muda wa miaka mitatu.



    Balozi huyo, alisema mikoa mitano ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Manyara na Singida itanufaika kutokana na ujenzi wa uwanja huo.

    Kwa mujibu wa Mutiso, ndege zitakazokuwa zinabeba watalii kutoka Amerika na Ulaya zitaruka moja kwa moja hadi katika uwanja huo ili kujionea vivutio vya utalii kama vile Mlima Kilimanjaro na mbuga za taifa za wanyama.



    Alisema lengo la kujenga uwanja huo ni kuinua hadhi ya vivutio vya utalii katika Hifadhi ya Mkomazi kwa upande wa Tanzania na mbuga za wanyama za Tsavo na Amboseli nchini Kenya.

    ReplyDelete
  3. Ukitaka kununua maeneo kijijini pitieni ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya mkishirikiana na Uongozi rasmi wa kijiji. Hakikisha hao ndiyo viongozi waliochaguliwa. Kumbukumbu zao ziko kwa DC. La sivyo mtalizwa jamani. Kwa mfano leo watu wa Kipawa wana ugomvi na watu wa Pugu kwa sababu hayo maeneo ambayo walikuwa wapewe watu wa Kipawa yaliuzwa kitapeli kwa watu wengine.

    ReplyDelete
  4. KAMA UKITAPELIWA NA MTU ALIYECHOKA HIVI (KWENYE PICHA) BASI NI HAKI YAKO KUTAPELIWA.....UTAMPAJE MTU KAMA HUYU SHILINGI ELFU KUMI NA TANO???

    ReplyDelete
  5. Hao ndio wanatuaribia sifa za mji wetu japo wako lkn wanauma na kupuliza sio kama hivi,
    Pili
    Kwa kuwa mlikuwa wengi ndio maana chanel haikukamata vzr matokeo ilimkamata mmoja wenu.msijali si mnataka eneo bado hakijaaribika kitu Nitafuteni mm nina eneo na liko sehemu nzuri nalimiliki kisheria Mtajenga shule hadi kule

    Mdau Mangesani mkabara na Gongoni

    ReplyDelete
  6. Kuna mzee mmoja marehemu sasa alienda kwa sir God mwaka jana anaitwa JALALA Mfaume. Yeye alikuwa ndo mwenyekiti kabisa wa kijiji kimoja visiga ndanindani huko. na mihuri na mashihidi analeta. How can you doubt mwenyekiti wa kijiji ambae still ana practise?

    kumbe jamaa alijua anandanji kwa gonjwa letu hili hatari akaamua kufurahia mapene ya watu. 2.4 m zilienda naye alikuwa akipiga piga simu hvo hvo. nlikwenda na lawyer teh..hata akugundua tunanyukwa!

    Babu alikuwa na ndumba sijui yule unaona bustani ya getsemani hiyooo but hata hushtuki.

    Nenda kwa dc kwanza never kwa wenykiti wa vijiji.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...