Align CenterJAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAHAKAMA YA TANZANIA

TAARIFA KWA UMMA


Taarifa hii ya uongozi wa Mahakama ya Tanzania ni kutokana na yaliyojitokeza leo siku ya tarehe 13 Oktoba 2010 nje ya jengo la Mahakama Kuu mara baada ya kesi Na. 95 ya Mwaka 2003 kuahirishwa. Uamuzi huo wa Mahakama ulipokelewa kwa hisia tofauti.Taarifa hii inakusudia kutoa ufafanuzi sahihi wa suala zima ili kuepuka tafsiri potofu inayoweza kujitokeza.

Ieleweke kuwa shauri la msingi lilikwisha Mahakamani kwa kutolewa hukumu ambayo ilitoa ushindi kwa Wazee wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao ni Karata Ernest na Wenzake dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Kwa mujibu wa sheria, ukazaji wa hukumu dhidi ya Serikali una matakwa yanayotakiwa kukidhiwa, ikiwa ni pamoja na kuwasilisha maombi Mahakamani kwa ajili ya kuomba Hati (Certificate).

Hati hiyo huwasilishwa kwa Mlipaji Mkuu wa Serikali (Paymaster General) kwa ajili ya taratibu za malipo (Kifungu cha 16 cha Government Proceedings Act Sura ya 5 ya Sheria kama zilivyorejewa mwaka 2002).

Washindi, pamoja na mambo mengine wamekuwa na mitazamo miwili tofauti kuhusiana na tuzo, idadi ya wanaodai na idadi ya wanaostahili kulipwa. Hii ni sababu kuu iliyochelewesha suala hili kufikia tamati. Hili ndio lililopelekea Mahakama kutoa amri tarehe 27 Julai 2010.

Tarehe 27 Julai 2010, Mahakama ilitoa amri kwa washindi kuwasilisha maombi ya pamoja baada ya kubaini kuwepo makundi hayo mawili yanayopingana miongoni mwao. Zaidi, tarehe hiyo Mahakama ilipanga kusikiliza maombi haya tarehe 27 mwezi Septemba 2010 baada ya kupokea nyaraka zote muhimu.

Kwa bahati mbaya, tarehe hiyo iliyopangwa maombi hayo hayakuweza kusikilizwa sababu Mh. Jaji N. M. Mwaikugile alikuwa katika likizo fupi. Lakini hata kama angekuwepo bado yasingeweza kusikilizwa sababu hakukuwa na Kiapo cha pamoja kwa Washindi (Joint Affidavit by the Decree Holders).

Hii ni kutokana na mawakili wanaowakilisha makundi haya mawili walihitaji muda zaidi wa kuhakiki orodha ndefu ya Wadai ili kuandaa kiapo hicho cha pamoja. Mawakili walikuwa na ombi la kuomba kuongezewa muda ili waweze kuwasilisha kiapo hicho.

Hii ilipelekea shauri hili kupangwa tarehe ya leo (13 Oktoba 2010) ambapo wangewasilisha maombi yao mbele ya Mh. Jaji anaesikiliza shauri hili.

Tarehe ya leo Mh. Jaji, ameamua kujitoa kuendelea na shauri hili ili haki itendeke na kuonekana imetendeka kwa mujibu wa taratibu na kanuni za kimaadili zinavyoelekeza.

Jalada liliwasilishwa mbele ya Mh. Jaji Kiongozi ambae alimpangia Mh. Jaji Utamwa. Leo hii, mawakili wa makundi yote mawili pamoja na Wakili wa Serikali wamewasilisha hoja zao mbele ya Mh. Jaji J.H.K. Utamwa kuomba kuongezewa muda wa kuwasilisha nyaraka muhimu. Mh Jaji amelikubali ombi hilo kwa kuwataka wahusika wawasilishe nyaraka hizo kabla au siku ya tarehe 15 Oktoba 2010 saa tano asubuhi. Shauri limepangwa kutajwa tarehe hiyo hiyo kwa ajili ya amri stahili.

Huu ndio ukweli wa suala hili na si vinginevyo. Ieleweke pia kuwa kama isingekuwa kutoelewana kwa washindi, suala hili lingekuwa limeshafikia tamati siku nyingi.


F.S.K. MUTUNGI

MSAJILI MAHAKAMA YA RUFAA

13 Oktoba 2010

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 7 mpaka sasa

  1. Kulikuwa na haja ya Msajili wa Mahakama ya Rufaa kutoa ufafanuzi huu kuhusu mambo yaliyotokea "Mahakamani" au hizi kampeni za uchaguzi mkuu zinamfanya kila mtu awe mbumbavu na mvivu wa kufikiri??!!

    Mdau
    Reading, UK.

    ReplyDelete
  2. Mwenyekiti naomba uwakumbushe wabongo kumpigia kura Mwisho huko Big Brother, asante.

    ReplyDelete
  3. Communication is a serious problem to many people - and whoever wrote this is no exception. To most readers, this could have been a case of anything - wagoni, wachawi, vibaka etc...

    ReplyDelete
  4. Scandal!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!
    No need for explanation. We better! hatudanganyiki!

    ReplyDelete
  5. Huu ulikuwa ni uzembe wa hali ya juu wa serikali ya TZ.
    Mimi nikiwa mmoja wa walionyimwa haki hii ya mafao toka 1977 ilipokufa East African Community, ninaona uchungu mno. Na hasa ukiona kwa wenzetu Kenya na hata Uganda (amabao walikuwa hawana hata serikali ijulikanayo kwa mda mrefu tu) wamelipwa bila matatizo mafao yao yote punde baada ya serikali zao kupokea malipo. Serikali ya TZ ilikiri wazi bungeni kuwa pesa zetu walizitumia toka 1980s kwa mashughuli mengine kabisa bila ridhaa yetu.

    Haki yetu ni yetu, and we are fed up of having to literally beg for it now. Tanzania Govt. Please do the right thing TULIPENI PESA ZETU IMMEDIATELY ....... Tumechoka!
    Justice delayed is justice denied.

    ReplyDelete
  6. Jaji anasubiri kujitoa hadi siku ya mwisho??! Alikuwa wapi siku zote au ninterest kwenye kesi imeonekana leo? Mara ya kwanza mahakama ilisema eti hawataisikiliza kesi hadi watakapokaa na kuamua na wastaafu wanede watajulishwa lakini baada ya kuamua kufia pale barabarani eti ndio mahakama ikakaa kikao cha dharura na kuamua kuteua jaji mwingine na kusikiliza ijumaa hii!! Huu ni nini kama sio kutokuwa na huruma na mwananchi anayelipa mishahara yao?!!

    ReplyDelete
  7. Mimi huliangalia suala hili kwa mtizamo tofauti. Lakini nasema, wazee wetu walipwe haki yao. Ni haki yao, nasema tena ni haki yao. Serikali yetu kwa makusudi kabisa na bila kujali maslahi ya watu wake iliamua kutumia fedha zao. kwa kipindi kile pengine, waliweza kujibalaguza, lakini nadhani it is too much. Let this matter be closed na tuangalie mambo mengine. Mtindo wa kuahirisha mambo hautatui tatizo, litaendelea kuwapo, na kwa kuwa nchi zetu zinakabiliwa na mlolongo wa matatizo, basi kila siku huzaliwa mengine.
    Lakini ninachoweza kuishauri serikali ni vyema ikalimaliza hili. Wajue wazee hawa wanaendelea kupata wahurumiaji, and the more wahurumiaji wanapoongezeka, suala nalo linaendelea kuwa kubwa na kuwa linaweza kuwa cheche ya tatizo kubwa baadaye. Sidhani yuko polisi ataweza kupambana na wazee wa miaka 70 nakuendelea! hayupo.
    Malizeni hili tatizo. Ni aibu kwetu.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...