MWANDISHI WETU

TIMU ya taifa ya Kenya imegoma kuendelea na michuano ya Chalenji inayoendelea hapa nchini kwa madai ya kutolipwa posho zao kwa siku 19 tangu waingie kambini kujiandaa na michuano hiyo inayofanyika kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es Salaaam.

Hata hivyo Kenya ilianza vibaya kwenye michuano hiyo iliyoandaliwa na Baraza la Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), kwa kukubali kichapo cha mabao 3-2 kutoka kwa Malawi kabla ya kupokea kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Ethiopia.

Jumapili Kenya ilikuwa ishuke dimbani kumenyana na mahasimu wao wa jadi Uganda katika mchezo wa kumaliza raundi ya kwanza ya makundi, ambapo Kenya hata ikifanikiwa kushinda haitaweza kusonga mbele,kwani utakuwa ni mchezo wa kukamilisha ratiba.

Lakini jana nahodha wa timu hiyo Steven Situma alisema kuwa wameamua kugoma si kwa sababu ya matokeo mabovu ila ni kwa sababu viongozi wa Shirikisho la Soka la Kenya 'FKL' wamekuwa wakiwadanganya na kuwageuza watoto wadogo kila mara na wameamua kuchukua hatua hiyo ili kuwa fundisho kwa viongozi hao.

"Mwanzo walituambia watatulipa pesa zetu siku ya Jumanne lakini hawakufanya hivyo, wakatuahidi tena watatupa Alhamis ambayo ni jana lakini hawakufanya hivyo, sasa sisi hatutacheza mechi ya Jumapili na tupo tayari kurudi Kenya hata sasa hivi"alisema Situma hata hivyo hakutaka kuweka wazi kiasi wanachodai zaidi ya kusema ni maelfu ya pesa za Kenya.

Naye Kocha wa timu hiyo Jacob 'Ghost' Mulee alisema amejitahidi kuwashawishi wachezaji hao wasigomee mashindano lakini imeshindikana kwani hata jana asubuhi waligoma kwenda kwenye mazoezi.

"Naweza kusema hata hivyo wachezaji wa Kenya wana nidhamu ya hali ya juu, wao kilichowakera zaidi ni ile hali ya kudanganywa kama watoto wadogo wakati wao ni watu wazima, hela wanazodai ni nyingi hata sisi tunadai benchi zima la ufundi hatujalipwa, na viongozi wetu wamekuwa wakituahidi uongo.....

"Wachezaji wapo kwenye hali mbaya sana hata mechi yetu na Ethiopia ilikuwa kazi kubwa kuwashawishi wacheze walikuwa wameshagomea kazi ilikuwa kwenye chumba cha kubadilishia walikataa kabisa kuingia uwanjani lakini tulijitaidi kuwashawishi hadi wakakubali lakini leo imeshindikana kabisa.

"alisema Ghost ambaye pia amedai hatishwi na viongozi wa FKL ambao wana desturi ya kumtimua kila mara timu inapofanya vibaya kwani hiyo ni sehemu ya kazi yake
Ghost ambaye alishatimulia zaidi ya mara tatu kunoa timu hiyo ya Kenya kabla ya kurejeshwa tena safari hii kwa ajili ya kuandaa timu kwa ajili ya michuano ya Chalenji aliyasema hayo alipoulizwa iwapo haofii kibarua chake kuota nyasi kutokana na kitendo hicho ikiwa ni pamoja na matokeo mabaya.

"Ni desturi yetu kufukuzwa timu inapofanya vibaya, mimi sijali hii ni kazi yangu, Ghost ni lazima aende na kurudi hawezi kukaa milele, na mimi siwezi kujiuzulu wakati nadai pesa yangu kama watataka kunifukuza sawa tu."alisema.

Naye Makamu mwenyekiti wa FKL ambaye ni kiongozi wa msafara wa timu hiyo, Erastus Okulu alisema "Nitazungumza nao na kuwatatulia suala lao nimeshazungumza na wenzangu wanashugulikia malipo yao siku yoyote kuanzia sasa lazima tuwape pesa zao, tunajua mpira ni hela hivyo wawe na subra tutawatatulia na kuondoa aibu hii."alisema Okulu.

Wakati Okulu akisema hayo, Katibu mkuu wa CECAFA Nicholaus Musonye alisema "Najua tatizo lao, ni lazima watacheza watake wasitake wamalizie ratiba, lazima wacheze."alisisitiza Musonye ambaye pia ni raia wa nchini humo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. Situma kama Evra!

    ReplyDelete
  2. KFL ilipeleka timu Tanzania ikiwa imefanya makubaliano nao,bahati mbaya watani zetu hao wamepoteza mechi zote 2 za awali ya mwisho ambayo hata kama watashinda wangekuwa nje ni dhidi ya Uganda ambayo kiukweli ni Uganda siku zote ni wakali so kwa kuogopa aibu wanaamua kujitoa,sikatai labda wana madai ya msingi ila kwa nini hawakufanya hivyo dhidi ya Ethiopia au mechi yao ya kwanza?haya ndio matatizo ya ukanda wa afrika mashariki kutopeleka timu wedi kapu na haitatokea kuwa hivyo kwani hakuna mpira zaidi ni utapeli tu timu zinagoma kuingia viwanjani kwa kutopata maslahi yao,imetokea hivyo kwa Yanga dhidi ya Simba watu wanagomea kwa sababu za kis...mara Kenya wanafanya hivyo jamani kuna mpira kweli hapo?haya na huyu ndugu yetu Mulee kiukweli ni kocha mzuri sana na mvumilivu kwani ashatimuliwa kimkizengwe na kurudishwa zaidi ya mara 3 na amekuwa mvumilivu KFL waache madhalilisho hayo.

    Ushauri tu ni kwamba hiyo team iingie uwanjani na ili kuikomesha KFL wachezaji wachukue hatua za msingi kudai madai yao na si kuogopa kichapo kwa Uganda.

    ZAUNUNU-AMSTERDAM

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...