Makamu wa Rais,Dr. Mohamed Ghalib Bilal

Na. Penzi Nyamungumi – Mwanza

Makamu wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal amesisitiza ushirikiano baina ya vyama vya siasa nchini kwa ajili ya kuendeleza amani na utulivu uliopo.

Dk. Bilal ameyasema hayo kwa nyakati tofauti wakati alipokuwa akizungumza na wananchi katika mikutano yake jana (Alhamisi) wilayani Sengerema akiwa katika ziara yake ya kikazi ya kukagua na kuona shughuli za maendeleo mkoani Mwanza.

Dk. Bilal ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM alisema uchaguzi umekwisha na wananchi wamefanya vizuri kuchagua viongozi wao kwa amani, kilichopo sasa ni kuimarisha ushirikiano baina ya vyama vya siasa kwa ajili ya kudumisha amani ambayo ni adimu kupatikana katika nchi nyingi za ukanda wa Afrika.

“Chama Cha Mapinduzi (CCM) iko tayari kushirikiana na vyama vingine kuifanya nchi yetu iendelee kuwa ya amani na utulivu ukilinganisha na nchi nyingine za ukanda huu wa Afrika,” alisema Makamu wa Rais na kuongeza

“Tumejipatia sifa ya kuwa wachapakazi wazuri. Hivyo, pamoja na matatizo, uchumi wetu unakua, kwa asilimia isiyopungua sita kwa mwaka. Hatutetereki, tunaongeza nguvu zaidi kupambana na matatizo tuliyonayo,” alieleza.

Katika mikutano hiyo katika kata ya Bupandwa na mjini Sengerema iliyohudhuriwa na viongozi wa wilaya wa Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi Dk. Bilal alisema kuwepo kwa matatizo ni sehemu ya maisha katika ulimwengu lakini lengo kuu ni kutaka kushirikiana kwa pamoja ili kutafuta njia ya kuondokana na matatizo hayo.

“Mwezi ujao tutakuwa na muswada Bungeni wa kushughulikia mabadiliko ya Katiba. Haikuwepo kwenye Ilani ya CCM. Lakini wapinzani wamesema, serikali imewasikiliza na kuyafanyia kazi madai yao. Hiyo ni dalili tosha ya ushirikiano,” alibainisha.

Aliwahakikishia wananchi wa Sengerema kuwa serikali itayatafutia ufumbuzi matatizo yanayoikabili wilaya hiyo yakiwamo ya kivuko na kusema tayari makisio yanafanywa kuikarabati MV Geita ili iwafikishe katika visiwa vilivyoko wilayani kwa usalama.

Kuhusu pembejeo Makamu wa Rais alisema mikakati inaandaliwa ya kuhakikisha pembejeo zinawafikia wakulima wengi zaidi kwani lengo ni kuzalisha kwa tija ili nchi iweze kujitosheleza kwa chakula na kuuza ziada kwa nchi jirani.

Akiwa kijijini Bupandwa Dk. Bilal aliweka jiwe la msingi jengo la vyumba vitatu vya madarasa ya shule ya sekondari Budapwa na akatoa shilingi milioni tatu kwa ajili ya kusaidia ujenzi unaoendelea wa shule hiyo.

Dk. Bilal leo ataendelea na ziara yake katika wilaya ya Magu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...