Aliyekuwa Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Abdallah Zombe, amewasilisha majibu yake dhidi ya hoja za serikali ambapo ameiomba Mahakama kutoa hukumu yake katika malalamiko aliyowasilisha dhidi ya serikali na kutupilia mbali ombi la mdaiwa la kutaka shauri hilo kufutiliwa mbali kwa madai kuwa halina hoja za msingi kisheria.
Zombe alifungua kesi hiyo namba 35 ya mwaka 2011, katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, akiiomba iiamuru serikali imlipe Sh bilioni tano.
Katika majibu yake dhidi ya hoja za serikali aliyowasilisha mahakamani hapo juzi, Zombe amedai kuwa kulingana na mwenendo wa kesi hiyo haihusiani na rufaa iliyopo katika Mahakama ya Rufaa na kwamba mdaiwa
anapaswa kuwasilisha vielelezo vya kutosha kuthibibitisha madai ya hoja zake.
Anadai kuwa kulingana na maudhui ya maelezo ya utetezi Zombe amedai kuwa anao ushahidi wa kutosha dhidi ya mdaiwa na kwamba kinacholalamikiwa ni mwenendo uliotokea kabla ya mashitaka hayajawasilishwa dhidi yake.
Amedai pia kuwa hoja ya serikali kwamba shauri hilo lifutwe kwa kuwa kuna rufaa iliyokatwa dhidi yake katika Mahakama ya Rufani hayana msingi kwani shauri hilo la madai linaweza kuendelea bila kuathiri
rufaa hiyo.
Zombe amepinga madai kwamba aliitwa na kujieleza akidai ukweli ni kwamba hakuulizwa chochote kabla ya kupelekwa mahakamani na hatimaye gerezani.
Amedai kuwa anapinga madai kuwa alipewa nafasi ya kujieleza na kwamba polisi walitekeleza wajibu wao ipasavyo, ukweli ni kwamba hakupewa nafasi ya kujieleza ambapo pia amemtaka mdaiwa kuthibitisha madai hayo
kwani Polisi walishindwa kutekeleza wajibu wao kwa kumshtaki bila ushahidi na kumuunganisha katika tuhuma hizo.
Kupitia kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), serikali iliwasilisha majibu ya hoja ya kwenye hati ya madai ya Zombe ilizowasilishwa mahakamani hapo na Wakili wake Richard Rweyongeza, Machi mwaka huu.
Shauri hilo lilitajwa kwa mara ya kwanza Mei 16, mwaka huu mahakamani hapo mbele ya Jaji Upendo Msuya.
Katika shauri hilo Jaji Msuya aliutaka upande wa mdaiwa (Zombe) ambaye anawakilishwa na Wakili Rweyongeza, kuwasilisha majibu ya serikali Mei 23, mwaka huu kwa njia ya maandishi, na shauri hilo limepangwa kutajwa
Juni 20, mwaka huu.
Mwanasheria Mkuu, aliiomba Mahakama kufutilia mbali madai ya Zombe kwa
madai kuwa hayana hoja za msingi za kisheria. Alidai kuwa Zombe alipelekwa mahakamani kujibu mashitaka hayo halafu akapelekwa jela Ukonga ni sahihi lakini si kweli kwamba Mahakama pamoja na Magereza zilikuwa zimetayarishwa kwa ajili yake, ukiachilia mbali dai la kwamba hakukuwa na hati ya kuitwa shaurini ambapo amemtaka kuthibitisha madai hayo.
Aidha, madai ya kwamba serikali ilivunja sheria kwa kumnyima haki ya kusikilizwa si kweli kwani aliitwa na kuhojiwa na tume hiyo kabla ya kupelekwa gerezani Ukonga, na kwamba kutiwa mbaroni kwa mdai
hakukutokana na kushindwa kwa Polisi kufanya kazi yao ya kisheria na mdai anatakiwa athibitishe madai hayo ya kwamba Polisi walishindwa kutekeleza wajibu wao kwa kumshtaki bila ushahidi wa kumuunganisha
katika tuhuma hizo.
‘‘Mdai hana madai yoyote dhidi ya serikali na anatakiwa kuthibitisha hivyo, kwa kuongezea kuna rufani ambayo haijasikilizwa katika Mahakama ya Rufani Tanzania, kwa msingi huo mdaiwa anaomba Mahakama itupilie
mbali madai hayo na mdai alipie gharama za kesi hiyo,’’ inadai sehemu ya hati hiyo ya majibu ya serikali.
Zombe aliachiwa huru pamoja na askari wengine waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva wa teksi.
Kwa kupitia hati yake ya madai, Zombe anadai alishitakiwa kimakosa katika kesi ya mauji ya wafanyabiashara watatu wa madini wa Mahenge, Morogoro na dereva wa teksi. Zombe anadai kiasi hicho cha fedha ikiwa ni fidia kwa adhabu ya kumweka ndani wakati kesi hiyo ilipokua ikiendelea, riba na gharama za kesi.
Zombe anadai alipwe fidia hiyo kwa madhara aliyoyapata katika kesi hiyo ikiwa ni kukamatwa na kushitakiwa kwa tuhuma hizo akidai ni ukiukwaji wa sheria. Pia anaiomba mahakama itamke alikamatwa na kushitakiwa kinyume
cha sheria, akidai kabla ya kukamatwa, alikuwamehamishiwa katika Mkoa wa Rukwa, alirejeshwa Makao Makuu ya Polisi siku 14 baada ya kuripoti kituo kipya cha kazi.
Anadai siku hiyo kabla ya kukamatwa na kupandishwa kizimbani, aliitwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) aliyemjulisha anatakiwa kuunganishwa na washitakiwa wengine waliokuwa wamekwishapandishwa kizimbani kwa
tuhuma hizo. Anadai alichukuliwa ghafla na kupelekwa mahakamani ambapo baada ya kusomewa mashitaka yake, alipelekwa Gereza la Ukonga, mahali ambako kila kitu kilikuwa kimeandaliwa kwa ajili ya kumpokea.
Aidha, analalamika kuwa baada ya kukamatwa, polisi walikuwa na wajibu wa kumuuliza kama alikuwa na jambo lolote la kusema ikiwamo kuweka kumbukumbu kuhusu ushiriki wake katika tuhuma hizo. Anadai aliwasilisha malalamiko kwa Waziri wa Sheria jinsi alivyotendewa na hakujibiwa.
Anailalamikia pia Polisi kushindwa kutekeleza wajibu wao kwa kumshtaki bila ushahidi wa kumuunganisha katika tuhuma hizo na kwamba matokeo yake, aliathirika kiakili, alifedheshwa na kupata usumbufu kutokana na
mashitaka. Katika kesi hiyo ya mauaji, Zombe alipandishwa kizimbani Juni 9, 2006 na kuunganishwa na askari wenzake wengine ambao jumla yao walikuwa 13.
Agosti 17, 2009, mahakama ilimuachia huru yeye na wenzake baada ya kuwaona hawana hatia katika makosa yaliyokuwa yakiwakabili. Zombe na wenzake walikuwa wakituhumiwa kuhusika na mauaji ya wafanyabiashara wa madini Sabinus Chigumbi (Jongo), Ephrahim Chigumbi, Mathias Lunkombe na dereva wateksi Juma Ndugu, Januari 14, 2006
katika msitu wa Pande nje kidogo ya Dar es Salaam.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...