KATIKA kumuenzi aliyekuwa mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Rungwe John Mwankenja baraza la mdiwani wa halmashauri hiyo wamenuia kujenga shule ya sekondari itakayopewa jina la kiongozi huyo aliyeuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiofahamika Mei 19 saa 2:30 usiku.
Waziri wa Maji Prof. Mark Mwandosya akiongea msibani
Mwandishi wa mtandao www.francisgodwin.blogspot.com Joachim Nyambo anaripoti kutoka Rungwe kuwa wazo hilo pia linakwenda sambamba na mabadiliko ya jina la ukumbi uliopo katika ofisi za halmashauri hiyo ambao sasa utaitwa ukumbi wa Mwankenja.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Bw. Adolf Wilhelm alisema hayo katika mazishi ya Marehemu Mwankenja yaliyoofanyika nyumbani kwake katika kitongoji cha Mpandapanda kijiji cha Kiwira na kumtaja marehemu kuwa miongoni mwa watu waliokuwa na mchango mkubwa katika kuiletea maendeleo halmashauri hivyo anapaswa kukumbukwa.

Bw. Wilhelm alisema shule hiyo haitaendeshwa katika mfumo wa shule za kata bali itatumiwa na wanafunzi kutoka maeneo yote ya wilaya ya Rungwe ili wananchi wa pande zote za wilaya hiyo waendelee kuwa na kumbukumbu ya kiongozi wao.

Naye Naibu Waziri Elimu ofisi ya waziri mkuu Tawala za mikoa na serikali za mitaa TAMISEMI Mh. Kassim Majaliwa aliunga mkono wazo hilo na kusema kutokana na mchango mkubwa wa marehemu serikali itachangia sehemu ya gharama za ujenzi wa shule hiyo ili ukamilike kwa haraka.

“Bahati Mbaya ni majuzi tu tukiwa Dar es salaam kwenye kikao, HAyati Mwankenja alitafuta muda na kukaa nami faragha.Katika mambo aliyonieleza ni pamoja na hali ya elimu katika halmashauri yake.

"Kutokana nay ale aliyonieleza nikakubaliana naye tupange ziara wilayani kwake kumbe
ziara yenyewe ni kumkuta yuko kwenye jeneza.Lazima serikali iweke mkono wake katika ujenzi wa shule ya kumbukumbu yake” alisema Naibu Waziri.

Mh. Majaliwa aliwahakikishia wananchi kuwa serikali inalifanyia kazi kwa makini suala hilo na kuziagiza kamati za ulinzi na usalama za wilaya na mkoa kuhakikisha zinafanya kila linalowezekana huku wananchi kwa upande wao wakitakiwa kutoa ushirikiano ili wauaji waweze kupatikana.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Mbeya Mh. John Mwakipesile alisema atahakikisha anasimamia ujenzi wa shule ya Mwankenja ili ukamilike kwa haraka kwa kuwa mkoa umeguswa na kifo chake huku akiwataka wananchi kutosita kutoa taarifa za watu wanaohisi kuhusika na tukio la mauaji ya Mwankenja aliyekuwa pia mwenyekiti wa CCM wilayani hapa.

Mh. Mwakipesile alisema kwa vyovyote wauaji hawakutokea mbali hivyo ushiriki wa wananchi utaezesha kukamatwa kwao kama ilivyotokea miaka ya nyuma kwa wahusika wa matukio ya ubakaji na mauaji ya watoto wadogo yaliyoitikisa wilaya hiyo miaka michache iliyopita.

“Kama unaogopa kwenda polisi njoo unione ofisini kwangu ama nenda kwa mkuu wa wilaya.Ukiona huko kote una mashaka nako muone kiongozi yeyote unayemwamini ili mradi tu utoe taarifa zitakazotusaidia kufanyia kazi juu ya tukio hili.” Alisema

Waziri wa Maji Profesa Mark Mwandosya alisema tukio hilo limeshusha heshima ya wilaya ya Rungwe na wakazi kwa ujumla kwakuwa kwa muda mrefu ilikuwa ikisifika kama wilaya yenye amani na iliyotoa wasomi na walio na nyadhifa za kuheshimika serikalini.

Marehemu Mwankenja aliyezaliwa Novemba 27 mwaka 1959 aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa ndani ya gari baada ya kuwasili kutoka safari jijini Mbeya alikokwenda kumjulia hali mkewe aliyekuwa amelazwa katika hospitali ya wazazi ya Meta na amemwacha mjane pekee.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...