![]() |
Dk. Ali Mohamed Shein |
Na Idara ya Habari (Maelezo),Zanzibar.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa serikali anayoiongoza imedhamiria kuimarisha sekta ya kilimo kwa kutambua kuwa ndio dawa ya mfumko wa bei hapa nchini.
Dk. Shein aliyasema hayo jana kwa nyakati tofauti akiwa katika ukumbi wa Benjamin Mkapa, Wete Pemba na ukumbi wa skuli ya Micheweni wakati alipokuwa akizungumza na viongozi wa CCM wa Wilaya ya Wete na Wilaya ya Micheweni ikiwa ni mfululizo wa ziara zake za kuzungumza na viongozi wa CCM wa Wilaya zote za Unguja na Pemba.
Kutokana na hatua hiyo alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar tayari imeshaanza mikakati madhubuti ya kuiimarisha sekta hiyo ya kilimo ikiwa ni pamoja na kuendeleza kilimo cha mpunga hasa cha umwagiliaji maji kwa kutambua kuwa hatua hiyo pia, itasaidia katika kufikia lengo la kujitosheleza kwa chakula na kupambana na mfumuko wa bei.
Dk. Shein ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alisisitiza kuwa tatizo la mfumko wa bei ni tatizo la nchini zote katika bara la Afrika pamoja na dunia nzima kwa jumla na sio kwa Zanzibar pekee na kueleza kuwa kila panapokuwa na maendeleo changamoto haziepukiki.
Amesema kuwa katika kipindi kifupi cha uongozi wa awamu ya saba serikali imefanya mambo mengi, ambayo ameyashuhudia wakati wa ziara yake ya kutembelea mikoa yote mitano ya Unguja na Pemba na kuyaona na kuona ipo haja ya kuwaeleza wanaCCM.
Dk.Shein pia, alieleza utekelezaji wa Ilani ya CCM imekuwa ikitekelezwa kwa kasi kubwa ikiwa ni pamoja na uendelezaji wa ujenzi wa skuli mpya za Sekondari Unguja na Pemba na kueleza kuwa ujenzi huo umegharimu fedha nyingi ambazo ni mkopo kutoka benki ya dunia unatarajiwa kumaliza mwezi wa Septemba mwaka huu.
“Tumepitisha sheria mpya ya uhifadhi wa chakula, ni lazima tuwe la chakula cha kutosheleza na ndio adhma ya serikali”, alisema Dk Shein.
Katika maelezo yake, Dk. Shein alisema kuwa tayari Sheria na Sera mpya zimeshapata baraka za Baraza la Wawakilishi na serikali itahakikisha inalisimamia kikamilifu ikiwa ni miongoni mwa adhma ya kuhifadhi chakula.
Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar inaungana na nchi nyengine duniani katika kutekeleza ushauri wa kuandaa maeneo maalum ya kuhifadhi chakula ili shida ikitokea kuwepo akiba ya kutosha ya chakula nchini.
Aidha, Dk. Shein aliwataka viongozi hao kuwa karibu na wanachama wa CCM hasawale wa ngazi za chini wakiwemo kutoka Matawini ili kutekeleza vizuri ilani ya CCM.
Alisema kuwa kuna umuhimu kwa viongozi hao kuwa karibu na wanachama hao kwani walipokuwa wakitafuta nafasi hizo za uongozi walikuwa nao kwa karibu sana hivyo kuna kila sababu ya kuendeleza utamaduni huo.
Kwa upande wa sekta ya ajira Dk. Shein alisema kuwa katika kipindi kifupi ndani ya miezi sita mafanikio makubwa yameweza kupatika katika uimarishaji wa sekta za elimu, afya, miundombinu ya barabara, kilimo na nyenginezo.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM, alisisitiza kuwa ajira zitaongezwa na pale patakapo kuwa na ajira za serikali vijana nao wataajiriwa na pale patakapotokea fursa ya kusaidiwa ili wajiajiri wenyewe watasaidiwa kwani suala la ajira limezungumzwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Katika maelezo yake pia, alieleza kuwa mshikamano ni jambo la lazima na kusisitiza haja ya kuendeleza amani na utulivu.
Alisema kuwa ahadi ya kuwasaidia vijana kwa lengo la kukuza ajira lipo pale pale ambapo vijana wataweza kujikusanya pamoja kwenye vikundi na kupewa vifaa zikiwemo boti kwa ajili ya kujishughjlisha na uvuvi.
Kwa upande wa maslahi ya wafanyakazi wa sekta ya Umma, Dk. Shein alisema kuwa tayari taratibu zimepangwa katika kuhaikisha wafanyakazi za serikali wanafanyiwa makerekebisho katika mishahara yao sambamba na kuangaliwa suala zima la pencheni.
Dk. Shein alisema kuwa kwa upande wa serikali iliyopo madarakani mashirikiano makubwa yamekuwepo kwa viongozi wa serikali ambao wote kwa pamoja wamekuwa wakifanya kazi kwa lengo la kuiletea maendeleo nchi yao.
Huko Micheweni Dk. Shein alisisitiza azma ya serikali ya kuliimarisha eneo la maeneo huru lilopo Micheweni ambapo tayari kuna baadhi ya waekezaji wameahidi kuja kuekeza katika maeneo hayo pamoja na maeneo mengine hapa Zanzibar.
Nao viongozi wa CCM Wilaya hizo walimpongeza Dk. Shein kwa kazi kubwa anayoifanya ya kutoa matumaini kwa wananchi na wanaCCM wa Zanzibar, ziara zake zinawakumbusha kumbukumbu za ziara zake za kampeni na kueleza kuridhika kwao na hatua yake hiyo na kusisitiza kuwa viongozi wote hao wapo pamoja naye.
Viongozi hao waliahidi kuendelea kukiunga mkono chama hicho pamoja na kumuunga mkono yeye Dk. Shein katika kukiimarisha chama hicho .
yadhamilia ndio kiswahili gani jamani?
ReplyDelete