Freddy Macha akiendesha moja ya warsha zake za muziki katika maktaba ya Queens Crescent, London, kuadhimisha mwezi wa watu weusi, Oktoba 2010. Picha na Deanna Smith
Lilian Nabora, mwasisi na mwendeshaji wa kituo cha Fasdo anayesomea utawala Ubelgiji.
Vijana wa Fasdo wakijifunza na kufanya mazoezi ya kuimba na muziki.
Picha na Lilian Nabora
Mafunzo ya utengenezaji wa sabuni, Fasdo.
Picha na Lilian Nabora
Freddy Macha akiwa na wanafunzi wa Sekondari, Mwandege, mkoa wa Pwani, mwaka 2009 baada ya warsha shuleni hapo iliyoangalia vipengele mbalimbali vya elimu, sanaa, lugha na afya. Picha na Innocent Swai
Macha akionyesha zoezi la Yoga, Nyumba ya Sanaa, Mei 2009.
Picha na Innocent Swai
Moja kwa moja toka London; mwanamuziki na mwandishi Mtanzania atafanya semina ukumbi wa Fasdo, Tandika, Dar es Salaam, Jumanne tarehe 11 na Jumatano 12, Oktoba, 2011.
Fasdo (Faru Arts Development Organisation) ilianzishwa mwaka 2009 kwa jitihada za Lilian Nabora anayesomea mambo ya utawala na maendeleo katika chuo cha Utafiti wa nchi za Ulaya, Ubeljiji.
Mada zitakazoangaliwa ndani ya warsha hizi ni :
1.Je, utafanikishaje afya yako? Ulaji, mazoezi na mambo mengine kibao.
2.Je, unawezaje kutoka kwao kuishi ughaibuni na ukafanikiwa? Mambo ya msingi unayohitaji kuelewa. Yalete maswali na mambo yanayokusumbua kuhusu suala hili.
3. Je, unataka kuwa mwanamuziki? Kwenu nyinyi wote wasanii wa leo na kesho, njooni mpokee vidokezo na ushauri.
4. Je, unataka kuwa mwandishi msanii au mwanafasihi? Siri za kukufanya uwe bora zaidi ya wengine! Ongeza kipato chako kupitia uandishi wa kimataifa.
5. Kukua na maendeleo ya lugha ya Kiswahili na Kiingereza
6. Ukumbi wa Maswali na Majibu
Habari zaidi : Chande Nabora: Simu 0713-310755
Nasibb: 0713-261011
Tovuti: http://www.fasdotz.com/
Mhusika
Freddy Macha ni mwalimu, mwandishi wa insha na habari, mwanafasihi, mtunzi wa vitabu, mkalimani, mwanamichezo, msingaji, mwanablogu na mwanamuziki. Hapa Tanzania anajulikana zaidi kama mwanasafu, aliyeanzia kazi magazeti ya Uhuru na Mzalendo, 1976-1978; akajenga jina na safu ya kila jumapili Cultural Images gazeti la Kiingereza, Sunday News 1981-84. Kuanzia 2003 amekuwa akiandika kolamu kadhaa nchini ikiwemo : Kalamu Toka London kila jumapili gazeti la Mwananchi na Chat from London gazeti la Kiingereza, The Citizen kila Ijumaa.
Anazo blogu kadhaa ; na hufanya kazi za usingaji, muziki, mtafiti na mtangazaji wa runinga mbalimbali za mtandaoni mathalan Urban Pulse Creative Media na Global Fusion Music and Arts, Greenwich, London.
Baadhi ya kazi kuu alizozitoa:-
2006, kitabu cha Mpe Maneno Yake, hadithi fupi fupi za Kiswahili alizokusanya miaka 30 katika nchi nyingi alizoishi na kuchapishwa na E & D Limited, Dar es Salaam.
2001, Wimbo wa “Kilimanjaro” na bendi ya Kitoto, London.
2000, CD ya muziki na fasihi –Constipation- iliyotolewa na kusifiwa na majarida kadhaa Ulaya.
1996, hadithi yake “Nilipomuua Nyoka” (When I Killed a Snake) kwa Kiingereza ilichukua nafasi ya pili katika Tuzo la Jumuiya ya Madola, London.
1995, alitoa CD ya muziki na fasihi– Kitoto- Quebec, Canada.
1986 alichapisha mwenyewe mashairi ya Kiingereza na Kijerumani (Papers! Papers! Papers! ) Cologne, Ujerumani.
1985, alichapisha kitabu cha maisha ya mwanamuziki Remmy Ongala.
1984, mkusanyiko wake wa hadithi fupi za Kiswahili : Twenzetu Ulaya (Gap, Dar es Salaam).
1981, mashairi yake ya Kiingereza yalishinda tuzo la BBC.
1979, alisaidiana na wenzake kuanzisha jarida la Wimbi lakini kutokana na sababu mbalimbali hawakufanikiwa.
Maisha Ughaibuni
Alitoka Tanzania mwaka 1984 na bendi ya Sayari iliyochanganya muziki, dansi, ngoma, mashairi ya maonyesho na tamthiliya wakazuru nchi za Scandinavia (Sweden, Norway, Denmark). Baada ya miaka michache Ulaya alienda zake kusomea muziki, Brazil huku akipigia bendi kadhaa hadi 1994 alipohamia Canada na hatimaye Uingereza.
Habari zaidi na video zake tembelea : www.freddymacha.com
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...