Walinzi wa Amani wa Umoja wa Mataifa wakiwa katika moja ya utekelezaji wa majukumu yao huko Darfur ya Kaskazini.  Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa hasa  zile zinazochangia wanajeshi wake katika Operesheni za Kulinda amani za Umoja wa Mataifa kwa wiki zima wamekuwa katika mkutano ambao pamoja na masuala mengine, wamekuwa wakipigania nyongeza ya  malipo kwa askari na vifaa ambavyo nchi zinapeleka katika Operesheni hizo.  wajumbe hao pia wamekuwa wakisisitiza tafsri sahihi ya majukumu mbalimbali ya walinzi hao, usalama wao, matatizo ya upungufa wa  vifaa kama vile Helkopta na wametaka pia  nchi nyingi zaidi zijitokeze kuchangia   wanajeshi wao.

Na Mwandishi Maalum,
New York

Tanzania imeitaka Idara ya Umoja wa Mataifa inayohusika na masuala ya ulinzi wa amani (UNDPKO), kutoendekeza dhana inayotaka kuota mizizi ya kuwa, kuna nchi ambazo jukumu lake  ni kutoa walinzi wa amani kwa upande mmoja, na kuna nchi ambazo jukumu lake ni kutoa raslimali fedha na vifaa kwa upande mwingine.

Kauli hiyo imetolewa na Balozi wa Tanzania  katika Umoja wa Mataifa,   Ombeni Sefue, wakati wa mkutano wa Kamati Maalum ya 34 ya Opereshani za Ulinzi wa Amani (C34).  kamati  hiyo  ni sehemu ya   Kamati  ya Nne ya Baraza Kuu la 66 la Umoja wa Mataifa. Mkutano huo ulikuwa ukijadili   ajenda namba 54 inayohusu dhana nzima ya ulinzi wa amani.

Kamati ya nne ni kati ya kamati sita za Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kamati hiyo inahusika   pamoja na mambo mengine, masuala ya siasa na umalizaji ukoloni  na operesheni za ulinzi wa amani na vilevile masuala ya Habari.

 Balozi Sefue amesema, kuna   kila dalili ndani  Umoja wa Mataifa, za kutaka  kujengeka kwa mazingira ya  kubaguana kati ya nchi  zile zinazojiita wachangiaji wakubwa wa askari na zile zinazojiita wachangia wakubwa wa raslimali zikwamo fedha.
“Ningependa kusisitiza mambo kadhaa, ambayo ujumbe wangu unaamini ni ya msingi  na yanatakiwa kuzingatiwa. Kwanza tunahitaji kupanua wigo wa kuchangia   walinzi wa amani. Na tuachane na dhana inayotaka kujengekea ya kwamba kuna nchi ambazo jukumu lao ni kuchangia askari,kwa upande na wengine  jukumu lao ni kuchangia raslimali.  Hii ni dhana potofu na si sahihi.   Jukumu hili adhimu ni  wajibu wetu sote”, akasisitiza Balozi Ombeni Sefue.

Takwimu zinaonyesha kuna walinzi wa amani  120.000 wanaume na wanawake, wanaotekeleza majukumu  yao katika misheni mbalimbali. Idadi kubwa ya wanajeshi hao wakiwamo askari polisi wanatoka katika   nchi za Afrika ,  Asia na baadhi ya nchi za   Mashariki ya Kati.

 Tanzania   inashika nafasi  ishirini  miongoni mwa katika kundi la nchi zinazotambuliwa kama wachangiaji wakubwa. Aidha Naibu Kamanda wa vikosi vya kulinda amani huko Darfur ni Mtanzania, Meja Jenerali Wynejones Kisamba. 
Aidha  Balozi Ombeni Sefue ameitaka pia  Idara hiyo ,  kutoa tafsiri sahihi kuhusu baadhi ya majukumu  wanayopewa  walinzi wa amani.

Akatoa mfano kwa kusema,  jukumu lijulikanayo kama ya Robust Peacekeeping ni moja ya  jukumu jipya  ambalo  licha ya kwamba utekelezaji wake ni tata lakini hata  tafsri yake yaijaeleweka miongoni  mwa walinzi wa amani.

Akasema   kama hapatolewa tafsiri sahihi  ya jukumu hilo na namna ya kulitekeza, inaweza kujenga mazingira ya mkanganyiko na hivyo kuhatarisha mfumo mzima wa utekelezaji wa  amri  na udhibiti katika eneo la  husika. “ kwa kweli hili ni jambo la mwisho  kutarajiwa na walinzi wa amani na makanda wao  ” akasisitiza Balozi.

Suala lingine ambalo Tanzania imetaka lipewe umuhimu ni usalama wa walinzi wa amani. Akasema   usalama wa walinzi hao   ambao wanatekeleza majukumu yako katika mazingira magumu na hatari, unatakiwa kuratibiwa ipasavyo.

“ Lazima tuhakikishe walinzi wetu wa amani kwanza,  wanakuwa salama wao wenyewe ,wanapewa vifaa  zikiwamo Helkopta. Na kwamba  majukumu yako yanatambulika na  yameratibiwa vizuri ” akasitiza Sefue.

Taarifa kutoka Idara hiyo ya Operesheni za Ulinzi wa Amani, zinaonyesha kwamba jumla ya walinzi wa amani  86 wamepoteza maisha kwa mwaka huu peke yake  na  kati  hao  29 ni raia.

Kuhusu marejesho ya malipo kwa nchi zinazochangia walinzi wa amani pamoja na vifaa, Balozi Ombeni Sefue amesema, Tanzania  inakaribisha wazo la kuundwa kwa Jopo la washauri ambao watalifanyia kazi suala la marejesho ya malipo.
Hata hivyo akasema ni matarajio ya Tanzania kwamba, ushauri wowote utakaotolewa na  Jopo hilo utakuwa jumuishi.

Suala jingine ambalo pia lilichangiwa na wazungumzaji wengi. Lilihusu jukumu la kulinda raia wakati wa machafuko  (Protection of Civilians).
Akiizungumzia jukumu hilo,   Balozi wa Zimbabwe katika Umoja wa Mataifa,Chitsaka Chipaziwa. Amesema kama iliyokuwa kwa  jukumu la Robust Peacekeeping.  Jukumu ulinzi  wa rais pia bado lina utata na utekelezaji wake pia .
“ Hivi tunapozungumzia jukumu la ulinzi wa raia,  je ni kweli walinzi wetu wanaelewa vema namna ya utekelezaji wake?. Ni wiki iliyopita tu tulionyeshwa hapa namna gani jukumu hilo linatakiwa kuingizwa katika mitaala ya ufundishaji. Lakini tayari walinzi wetu walishaanza kulitekeleza jukumu hili.  Kwa hiyo ni nini kinachoanza, mafunzo kwanza au utekelezaji kwanza mafunzo baadaye", akahoji Balozi wa Zimbabwe.

Akafafanua zaidi kwa kusema pale ambapo jukumu hilo la kulinda raia lisipotekelezwa ipasavyo wanaolaumiwa ni nchi zinazochangia walinzi wake . Ili hali hapakuwa na muda wa kutosha kwa walinzi wetu kujifunza na kulielewa vema jukumu hilo. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...