Basi la abiria la kampuni ya Taqwa linalofanya safari zake kati ya Dar-Kigali nchini Rwanda limeanguka katika eneo la Mikese, Morogoro wakati likiwa njiani kuja jijini Dar na kujeruhi watu kadhaa waliokuwepo kwenye basi hilo.Chanzo cha ajali ni lori la mizigo lililokuwa limeegeshwa barabarani kutokana na ubovu, pia mwendokasi wa mabasi,kwa mujibu wa mashuhuda wa ajali hiyo.wakati huo huo Basi la Morobesti limenusurika kuanguka japo liliacha njia kutokana na chanzo hicho hicho cha Lori lililoharikiba na kusimama barabarani. 
Msururu wa magari katika eneo la ajali.

Baadhi ya wananchi wa Mikese, Wilaya ya Morogoro, wakiangalia basi la Moro Best lililopinduka katika Barabara kuu ya Morogoro- Dar es Salaam, na kusabaisha majeruhi kwa abiria 24, Basi hilo lilokuwa likitokea Wilayani Kilosa kwenda Dar es Salaam.
Basi la kampuni ya Morobesti likiwa limeacha njia na kutoka nje ya Barabara kama linavyoonekana pichani hapa likifanyiwa mpango wa kuvutwa na Break Down inayoonekana hapa katika eneo la ajali.
Baadhi ya Majeruhi katika ajali hizo wakiwa katika hospitali ya mkoa wa Morogogo.

Na John Nditi, Morogoro

JINAMIZI la ajali za mabasi limeanza kuukumba Mkoa wa Morogoro baada ya kutokea ajali nyingine mbili tofauti na kusababisha abiria 51 kujeruhiwa na baadhi yao wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.

Ajali hizo za mabasi zilitokea kwa muda na nyakati tofauti Januari 5,mwaka huu katika eneo la Mikese,Wilaya ya Morogoro katika Barabara kuu ya Morogoro- Dar es Salaam , hata hivyo hazikusababisha vifo vyovyote.

Ajali hizo zimetokea siku mbili tu baada ya kutokea kwa ajali nyingine Januari 3, mwaka huu ya Basi la Upendo ilipoteza maisha ya abiria wawili na kujeruhi wengine 29 ,katika eneo la Kijiji cha Doma,Wilaya ya Mvomero kwenye barabara kuu ya Morogoro- Iringa.

Akizungunza kuhusiana na ajali hizo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Adolfina Chialo, alisema ajali ya kwanza iliyotokea majira ya saa moja asubuhi ya Januari 5, mwaka huu kwa kulihusisha Basi la Taqwa Coach lenye namba T 478 BBJ lilolokuwa likiendeshwa na Nicolaus Mroma Mohamed (31) likitokea nchi ya Burundi kwenda Dar es Salaaam.

Kwa mujibu wa Kamanda huyo, ajali hiyo ilisababisha abiria 27 kujeruhiwa na kati ya hao wanne waliumia ambapo derava wake alijaribu kukwepa kugongana uso kwa uso na gari jingine na alipojaribu kukwepa basi lilitumbukia bondeni.

Kuhusu ajali ya pili ilitokea saa tatu asubuhi ya Januari 5, mwaka huu katika eneo hilo la Mikese, Barabara kuu ya Morogoro- Dar es Salaam,kwa kulihusisha basi la Moro Best lenye namba T 846 BCU aina ya Scania lilolokuwa likiendeshwa na Amini Mzigira (43) ambapo limesababisha majeruhi 24 baada ya kupinduka.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda huyo alisema , Basi hilo lilikuwa likitokea Mjini Kilosa kwenda Dar es Salaamna lilipofika eneo la Mikese nalo lilipoata ajali wakati derava wake alipojaribu kulikwepa gari jingine lilolokuwa likija mbele yake na kutoka nje ya barabara.

Hata hivyo alisema, abiria 24 walijeruhiwa ambapo mmoja amelazwa Hospitalini kutokana na kupata majeraha makubwa aliyoyapata.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa , chanzo cha ajali hizo ni uzembe wa dareva Lori aliyekuwa akijaribu akilipita lori njingine bovu ililiengeshwa kando ya Barabara wakati Basi hilo likipita upande wake.

Hata hivyo Kamanda wa Polisi wa Mkoa huyo, alisema Dereva wa Lori Scania lenye namba T 612 BTL ,Daniel Amos (37) mkazi wa Sinsa , Jijini Dar es Salaam, ametiwa mbaroni na Polisi kutokana na kuwa chanzo cha ajali hizo.

Nao baadhi ya majeruhi wa Basi la Moro Best waliopokelewa Hospitalini hapo kwa ajili ya matibabu , kwa nyakati tofauti walidai kuwa ajali hiyo ilitokana na dereva wa basi kulikwepa Lori hilo.

Miongini mwao ni Halima Maulidi (32) mkazi wa Kilosa, aliyekuwa na watoto wake Hadija Kulongwa (17) na Juma Kulongwa (13) alisema kuwa wanamshukuru mungu kuwanusuri kifo licha ya kupatwa na majeraha madogo.

Baadhi ya majeruhi waliopokelewa kutokana na ajali ya Basi la Moro Best ni Anna Robert na mumewe Matayo Lucas ambao ni wakazi wa Kinondoni , Mkoa wa Dar es Salaam.

Naye Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Dk Frida Mokiti, akizungumzia ajali hizo, alisema walikuwa wamepokea majeruhi wengi kutokana na ajali mbili hizo na kwamba baadhi walitibiwa na kuruhusiwa na wachache wamelazwa.

Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, waliolazwa kwenye wodi za majeruhi kwa upande wa wanawake na wanaume walikuwa wamefikia saba.

“ Tumepokea majeruhi wengi wa ajali za mabasi mawili moja na baadhi tumewatibu na kuruhusiwa na wachache wamelazwa nab ado tunachukua majina na rekodi zao…na pia majeruhi wawili wanafanyiwa upasuaji kufuatia kuumia vibaya akiwemo mtoto mdogo “ alisema Dk Mokiti.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 20 mpaka sasa

  1. Tatizo kubwa ktk sababu za Wimbi la ajali za barabarani ni kuwa matajiri wengi wa kampuni za mabasi wanaendesha mambo kwa Kiswahili sana, kutumia rushwa,hawazingatii mafunzo ya mara kwa mara kwa madereva kama wanavyofanya kampuni ya BP na kutofuata taratibu.

    Hebu tujiulize mji au inchi lilipoanzia safari hilo basi Kigali-Rwanda,je kule ajali kama huku zinasikika?, umewahi fungua Radio au TV ukasikia wimbi la ajali za barabarani huko?, wao hawana magari wanatumia Punda tu?

    Unakuta wanaajiri madereva kiholela tu, bila kujali sifa na uzoefu ,huku wakizingatia kujuana pekee, na wanataka madereva rahisi rahisi tu!

    ReplyDelete
  2. Poleni na ajali, Mungu awajalie afya njema haraka wote waliohumia.
    Serikali boresheni miundo mbinu ya RELI hayo malori yapungue barabarani. Ndo chanzo kikubwa cha ajali pia. Wanapaki ovyo, hawaweki halama za kutosha.

    ReplyDelete
  3. Lilikuwa linatoka Bujumbura-Burundi sio Kigali, ndugu yangu ni mmoja wa majeruhi nawaombea nafuu ya haraka majeruhi.

    ReplyDelete
  4. michuzi mbona huleti habari ya ujambazi migodini Geita, fuatilia utujuze.

    ReplyDelete
  5. mabasi hayana viwango vya kutosha ili kutumika kusafirishia watu isipokuwa kinachotumika ni rushwa kuyapitisha kwenye viwango.

    ReplyDelete
  6. Pasinga wenyewe ndio wanaosababisha ajali kwa ushabiki wa kuchochea spidi ili kufika mapema, maana basi linalokwenda taratibu linaonekana bovu au dereva hafai, abiria wana majukumu ya usalama wao. Nimewahi kusikia wakifagilia basi linalofika mapema, na tajiri afanye nini wakati anataka pesa.

    ReplyDelete
  7. Michuzi mimi nashangaa sana ajari zingine hasa za hapa town hazitangazwi na ni mbaya kwa uzembe wa Drivers.

    jana kuna daladala ya Kimara to Posta ilipita njia za panya kukimbia fokeni asubuhi. driver alishika njia ya kwenda mwenge kutokea ubonge kukwepa foleni. alipofika mataa ya kuingia sinza makaburini karibu na mlimani city shopping center akakuta taa nyekundu zinawaka basi yeye akakata comer bila kujali kama taa hazimruhusu kupita basi aligongangana na saloon car ikapinduka mara tatu na kupoteza maisha ya mpenzi wetu Frida...

    cha ajabu hata redio, magazeti, TV na hata wewe hujasema chochote kuhusu tukio hili la kizembe wa ukiukwaji wa sheria unaofanya na wazembe wachache.

    imeniuma sana na nahisi landa gari ina mkono wa kibosile na ndo maana issue imemaliza kimnywa hivyo bila kujali pendo aliloliacha Mpendwa wetu Frida kwa mwnae wa pekee, mama,baba na wadogo zake.

    R.I.P. FRiDA NGALOWOkA

    ReplyDelete
  8. Nyie matrafiki, mnafanya uzembe na kwa makusudi mnapelekea ajali kila leo. Kisha watu wakishaumia mnawakawiza kupatiwa huduma za haraka kisa mnataka wawape stori za namna ajali ilivyotokea. Mbona mpo dhidi yetu sana, hata aibu hamuoni??? Waziri, ndivyo inavyopaswa kuwa namna hii???

    ReplyDelete
  9. Poleni sana ndugu zetu mungu awafanyie wepesi mpone haraka. Lakini pia Bongo ajali zikitokea watu hubebwa hovyo hovyo hatujali kaumia wapi ndo maana watu wanapoteza maisha au kupata vilema vya maisha. Mtu hujui kaumia wapi sisi tunafika tunabeba tu Jamani!! mungu tusaidie.

    ReplyDelete
  10. Hizi ajali ni nyingi na husababishwa na mengi.KWANZA kabisa barabara nadhani zinahitaji kuongezwa upana na zitenganishwe.Upande mmoja uwe na njia tatu pamoja na sehemu za kusimamisha gari iwapo kutakuwa na dharura.Na vilevile malori na mabasi yaruhusiwe upande wa kushoto tu au kama inataka kumpita mwenzake ndio anaweza kutumia njia ya katikati.
    PILI..Madereva wanahitaji kwenda kusomea uendeshaji na kila kampuni wanatakiwa wawape kisomo cha kujikumbusha udereva na jinsi ya kukabiliana na matatizo ya barabarani kwa kuwa makini kila baada ya miezi sita ili walazimishwe kufuata sheria barabarani.
    TATU...Madereva wengine naamini wanakunywa pombe safarini au wanakuwa wamekunywa siku iliyopita na hatimae kuamka na "hengover"hili pia ni tatizo kubwa sana kwa kumfanya dereva kutokuwa makini au kujiona yupo zaidi ya umakini"over confidence" na hatimae kusababisha ajali.Hii nadhani Polisi wangepewa vyombo vya kuwaangalia madereva njiani vyombo vya kukagua kama mtu amekunywa pombe.
    NNE...Madereva wengi vilevile hupenda kutumia simu huku wakiendesha gari.Ningeomba abiria washirikiane na Polisi kwa hili kwani ni hatari sana hata kama dereva ni mjuzi vipi lakini umakini wa barabarani hautakiwi kuingiliana na chochote kile ambacho kitamtoa mawazo ya dereva ktk barabara na kumuingiza ktk jambo lingine tofauti.
    TANO...Madereva wengine hawapumziki vya kutosha kwa kujiandaa na safari.Kwani kuendesha gari ukiwa umechoka pia ni hatari inasababisha kupoteza umakini ktk barabara hasa kama dereva hajalala usingizi wa kumtosha na pengine alienda kujirusha usiku kucha.
    SITA..Kama serikali itapanua reli na kuweka usafiri huu ktk mikoa kwa kweli mambo yatakuwa ni mazuri sana na hatimae barabara zitapumzika na ajali hizi maana kama zingekuwa zinasema na kuhesabu vifo basi sijui ingekuwaje.

    ReplyDelete
  11. kuna haja gani ya kuwa na kiongozi anayeshughulikia maswala haya?
    Labda mpaka janga limkute na yeye ndiyo ataanzakufanya kazi?
    Ajali nyingi za barabarani Tanzania zinasabishwa na uzembe ...
    Kuna haja gani ya kukimbiza basi kama basi linafanya safarizake kwa kuzingatia mda?
    Kuna haja gani ya kuwa na magari kama watumiaji hawajuwi jinsi ya kutumia?
    Wenzetu walivyoanzisha utumiaji wa magari mengi barabarani walitoa elimu ya jinsi ya kuepuka ajili za kiuzembe za barabarani.
    Tanzania imekuwa na ajali nyingi za barabarani ukilinganisha na nchi nyingi za Afrika mashariki.
    Muhusika fanya kazi au Wizara ifutwe kwa uzembe wako...

    ReplyDelete
  12. Duh,Poleni kwa wote walio poteza ndugu na jamaa katika ajali.Na tunaomba mungua awape nafuu na kupona majeruhi wote waendelee na shughuli zao
    Nchi yetu Tz imesha kwisha na sasa hizi ni dalili za kufikia ukingoni.Kila sekta,kitengo or wizara ni kubovu na kunanuka.Hakuna kwenye nafuu.Ni sawa na mtu mwenye matatizo kibao ila akiwa amevaa shati,suruali na kiatu uwezi mjua.Hii ndo Tz na utawala wake tangu enzi na enzi.Hakuna uboreshaji bali hali ina kuwa mbaya siku hadi siku.Twamuomba mungu atuongoze kwani sisi Raiya hatuna la kufanya ila hao Viongozi ndo wametumaliza na wanaendelea kutumaliza.
    Mwisho wake sijui ni nini?.Watu watashindwa vumilia na kuamua ku muuwa yule anaye fanya uzembe e.g Drivers wazembe,Mafisadi nk.
    Mifano nchi za watu tunaziona.
    Jk tunaomba uingilie kati na uokoe nchi ilipo fika ni pabaya.
    Yes we can

    ReplyDelete
  13. Wala si swala la madreve. Matajiri wa mabasi wako kishirikina zaidi

    ReplyDelete
  14. POLENI SANA.
    ILA MAGAUNI HAYO NI WAGONJWA SIO WATOA HUDUMA JAMANI .

    ReplyDelete
  15. Duh! matajiri wa mabasi wanaroga mpaka mabasi!? basi wakaaalee! waambie waroge maendeleo ya nchi tuendelee chapchap!!

    ReplyDelete
  16. HAKUNA USHIRIKINA WALA NINI TATIZO NI UZEMBE AJALI NYINGI ZINASABABISHWA NA UZEMBE,HIYO USHIRIKINA INAFANANA NA ZILE IMANI ZA KUSEMA MWISHO WA MWAKA AJALI ZINAKUWA NYINGI KITU AMBACHO SI KWELI BALI NI UZEMBE

    ReplyDelete
  17. Madereva wapimwe uwendawazimu vichwa

    ReplyDelete
  18. Mimi naomba kuuliza hawa wakuu wa usalama wa barabara kazi yao ni nini kukaa kwenye ofisi na kupokea mishahara ya bure hizi ajali za barabarani haswa za mabasi wenye abiria zimezidi hii ni aibu sana na hamna hata hatua zinachukuliwa kutataua hili tatizo wanatakiwa kuamka hawa watu wanaopata ajali ni binadamu inaonekana hawajali kwa sababu hakuna ndugu zao wanapopata ajali wanatakiwa kuyafungia kidede haya maswala haswa hao madereva wanaharibikiwa barabarani na hao madereva wenye leseni za mlango wa nyuma mnatumalizia jamaa zetu acheni hayo.Polisi wa usalama barabarani mnatakiwa kuyafungia hayo mabasi na madereva kuchukuliwa hatua kali

    ReplyDelete
  19. kwanza naona tuwekane sawa,hilo basi la moro best sio scania ni yutong mabasi ya kichina,pili tatizo la hizi ajali limekuwa sugu,matrafiki wanajaribu kuvinzia madereva wanaoenda mwendo kasi sana sana kwenye makazi,wanakuwa na speed gater(tochi)lakini bado sio dawa ya kuwafanya madereva waenende mwendo unaotakiwa,mara nyingi ukiwa barabarani ndio unaona madereva wanavyopeana ishara kwamba trafik wapo wapi na wapunguze mwendo,wakati mwingine madereva wa mabasi wanapigiana simu kwamba trafik wapo wapi,sasa kwa mtindo tutafika kweli jamani??tatizo jeshi polisi kitengo cha usalama barabarani wanafanya kazi kwa kubahatisha sijui,ila manually zaidi.

    ReplyDelete
  20. Jamani ankal ajali nyingi ni uzembe wa madereva, kwani unaweza kumbambia rubani wa ndege au meli kimbia tuwahi. Dereva ndio yuko kwenye usukani. Serikali haithamini maisha ya watanzania. Tunaomba waziri wa hii idara aangali kwa makini. Wakubwa wako kwenye magari yao hawana habari na wadogo.
    Mungu ibariki Tanzania.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...