MAMLAKA ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), imepandisha bei ya mafuta ya Petroli kwa Sh72 zaidi ya ile ya awali. Mbali na Petroli Ewura imepandisha bei ya mafuta ya Taa kwa Sh5 huku bei ya Dizeli ikibaki kama ilivyo.

Awali bei ya Petroli iliuzwa Sh1882 na kuanzia leo inatarajia kuuzwa Sh1954 kwa lita, mafuta ya Taa yaliyouzwa kwa Sh1958 yatauzwa Sh1963 lakini Dizeli itaendelea kuuzwa Sh1976 kwa lita .

Bei hiyo mpya inayotarajia kuanza kutumika leo kote nchini imekwenda sambamba na kuanza upya kwa matumizi ya kanuni ya ukokotoaji wa bei za mafuta.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ewura kwa vyombo vya bahari, kanuni hiyo mpya inakwenda sambamba na kuanza kutumika kwa kanuni mpya za mfumo wa ukokotoaji wa bei ya mafuta.

“Kanuni hii itaanza kutumika Jumatano ya Januari 4 mwaka huu,(leo) kwa Tanzania Bara na itakuwa ikirekebishwa kila baada ya mwezi mmoja” inasema sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa ilifafanua kuwa gharama za mafuta zinatokana na ongezeko la tozo inayotozwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania (Wharfage) ambayo imeongezeka kutoka dola8.30 za Marekani kwa ujazo wa tani moja hadi dola 10 za Marekani. Kiasi hicho ni kwa ujazo wa tani moja, pamoja na ongezeko la Thamani (VAT).

Taarifa hiyo ilifafanua kuwa ongezeko hilo limelenga kuiwezesha (TPA) kuendeleza miradi mbalimbali inayohusu biashara ya mafuta, ikiwamo ujenzi wa gati mpya ya kupakua mafuta (SPM) na Ukarabati wa mifumo ya miundombinu ya Kurasini Oil Jetty (KOJ).

Ilitaja miradi mingine inayotekelezwa na TPA kuwa ni ujenzi wa maghala mapya na eneo la upokeaji mafuta (manifold) na kwamba miradi itakapokamilika itaboresha kazi ya kupokea mafuta na pia itapunguza gharama za mafuta kumalizika kwa miradi hiyo.

Kutokana na bei hiyo mpya Petroli kwa jiji la Dar es Salaam itauzwa 1956,mafuta Dizeli Sh1977 na mafuta ya Taa Sh1963, Mwanza Petroli itauzwa kwa Sh2106,Dizeli Sh2127 na mafuta ya taa Sh2112.

Katika jiji la Arusha Petroli itauzwa kwa bei ya Sh2040, Dizeli Sh2061 na mafuta ya taa Sh2047, Mbeya Petroli itauzwa kwa Sh2063, Dizeli Sh2084 na mafuta ya Taa Sh2069.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. muschi b.c.January 05, 2012

    Mbona wenye vituo vya kuuza mafuta hawajagoma kuuza mafuta kwa bei hizi mpya tena za juu sana!au mafuta huadimika bei ikishushwa! EURA you have a long distance to go!!

    ReplyDelete
  2. EWURA munatababisha kila wakati humuna msimamo!!!

    ReplyDelete
  3. Ewura acheni nguvu ya soko ifanye kazi kuliko ubabaishaji wa kila siku. Nyie tulieni muendelee kuiba kama kawaida yenu kwenye mafuta, kwenye luku, na kila kitu. Mkishusha mnatangaza kwa mbwembwe... mkipandisha mnafanya kimya kimya? kulikoni? kila mwenye akili anatambu wauiza mafuta nchi hii ni watawala wetu ambao ndiyo waliokuteua wewe Masebu! Pamoja na usomi wako lakini huna hata jeuri ya kujiuzulu!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...