TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Bara la Afrika linakabiliwa na changamoto nyingi katika kuleta mageuzi katika kilimo chake lakini ni muhimu changamoto hizo zinaweza kutatuliwa kwa pamoja kati ya Serikali na Sekta Binafsi.

Rais Kikwete ameeleza hayo katika mkutano wa wadau wa Uchumi wanaokutana mjini Davos-Switzerland, kuzungumzia mageuzi na changamoto za uchumi na fedha zinazoikabili dunia kwa sasa.

Katika Mada inayohusu mtazamo na muelekeo mpya wa Kilimo na hatua zinazoweza kuchukuliwa, Rais kikwete amesema, sekta ya kilimo barani Afrika inahitaji mageuzi makubwa ya kukifanya kiwe cha kisasa na chenye tija na hatimaye kuweza kuzalisha chakula kwa ajili ya matumizi ya watu wake na ziada kwa ajili ya kuuza nje ya bara hilo.

“Ukizungumzia mageuzi ya kilimo unazungumzia kilimo kinachotegemea sayansi na teknolojia ya kisasa itakayotufanya tutumie mbolea, mbegu bora, zana bora za kisasa ili kilimo hiki kiwe na tija”. Rais amesema na kuongeza kuwa kwa kufanya hivyo, bara la Afrika litakuwa limewatoa wananchi wake kwenye umaskini mkubwa lakini pia kuongeza ajira na kuvutia maendeleo zaidi Barani Afrika.

Rais amewaeleza wajumbe wa mkutano huo unaojumuisha Viongozi wa Serikali, Wakuu wa Makampuni na Mashirika ya Kibiashara, Kifedha na Wataalamu mbalimbali wa Fedha na Uchumi duniani.

“Kilimo barani Afrika pia kimekuwa na changamoto nyingi kutokana na kuwa kinaendeshwa na serikali, mara nyingi serikali zimekuwa zinakabiliwa na upungufu wa fedha hivyo kutenga fedha chache na zisizotosheleza katika kufanya shughuli za utafiti na kuboresha kilimo kwa ujumla”. Rais amesema na kutoa mwito kwa nchi tajiri, wafanyabiashara wakubwa na wadau wa maendeleo kutoa kipaumbele na kuanza kutilia maanani sekta hii ya kilimo barani Afrika.

“Tunaweza kushirikisha sekta binafsi ili kuchangia nguvu na mchango wa serikali, kwa pamoja tutaweza kukuza kilimo cha Afrika na kukifanya kiwe na tija zaidi kwa wakulima na wadau wote kwa ujumla”.

Amesema na kutoa mfano wa mkakati wa kukuza kilimo Kusini mwa Tanzania unaohusisha mikoa mitano, iliyo katika ukanda wa Tazara maarufu kama Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania (SAGCOT).

Mpango ambao unajumuisha juhudi za Serikali, Sekta Binafsi na Makampuni Binafsi ya nje na ndani ya Tanzania.

Lengo kubwa la mpango huu ni kuzalisha chakula kwa wingi hasa mahindi katika Mikoa ya Iringa, Ruvuma, Mbeya, Rukwa na Morogoro, kwa ajili ya matumizi ya ndani na nje ya Tanzania.

Rais Kikwete ametoa mfano huu wa SAGCOT na kutoa changamoto kwa wadau na washiriki wa Mkutano wa mwaka huu wa Uchumi Duniani, maarufu kama World Economic Forum (WEF), kutumia mpango huu kama mfano wa kuigwa na kutumika katika nchi zingine za Afrika, ili kuboresha na kuleta mabadiliko katika Kilimo barani Afrika na hatimaye, kuchangia katika kukuza uchumi na maendeleo ya bara la Afrika na dunia kwa ujumla.

Rais Kikwete ameondoka leo tarehe 28 Januari 2012, kuelekea Addis Ababa, Ethiopia kuhudhuria kikao cha Wakuu wa Nchi cha kila mwaka.

Mwisho.

Imetolewa na Premi Kibanga,

Mwandishi wa Habari Msaidizi wa Rais,
Davos-Switzerland.
28 Januari, 2012

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 6 mpaka sasa

  1. porojo nyingii

    ReplyDelete
  2. Rais wetu anazungumzia kuhusu green revolution ambayo nchi zilizoendelea zinatafuta njia mbadala ya green revolution movement ambayo imeleta madhara makubwa katika mazingira na afya.
    Nia yake kubwa ni kuwa uwekezaji mkubwa wa katika nchi yetu lakini vipi kuhusu athari za kimazingira nafikiri inabidi tujiunge katika Dunia ya leo na kuzunguzia multifuctional agriculture kilimo ambacho ni bora kwa mazingira, jamii na uchumi wa nchi.

    ReplyDelete
  3. acheni kutuzingua, the thing is western powers hawana sehemu ya kutengenezea chakula their population. Hii ndo ishu ya food security inayowasumbua ndo maana wanakuja kwa kasi Afrika na hasa nchi zenye rutuba kama Tanzania kujidai wanawekeza na kutuletea kampuni kama AgriSol Energy. Ubaya zaidi viongozi wetu mnatufanya kama wapumbavu hatuwezi kujua vitu kama ivi. Tunajua mnapoomba misaada mnapewa masharti ya kuruhusu kampuni kama Agrisol kupewa hekari kibaao kwa bei za kutupa na kufukuza wenyeji. Chonde chonde viongozi wetu, hamna tofauti na kina Chief Mangunga waliouza nchi kwa kupewa vioo watazame sura zao. Kumbukeni uongozi ni kujitolea na wito, sio biashara. Na pia "One Day the Poor Will Have Nothing Left to Eat but You the Rich."

    ReplyDelete
  4. Tutaudhuria mikutano mingi sana ulaya lakini maendeleo ya nchi hayaletwi na watu wa nje bali ni watanzania kwa kushirikiana na wataalamu wake wa ndani mikutano hii mingi ni ya kupoteza muda. tunazo resources za kutosha na wataalmau wa kutosha tuwatumie tujilitee maendeleo

    ReplyDelete
  5. mwanadamu mgumu sana. ikiwa kweli wanamtizamo na wana nia nzuri juu ya kilimo kwanza wawasaidie wakulima wadogodogo.Vile vile watumie pesa wanazochukua kwa ajili ya misafara ya raisi na kutokununua mashangingi wainvest kwenye kilimo. Hakuna cha urahisi.unapomnunulia changudoa wako gari au kumjengea nyumba kwa kutumia nguvu za wananchi unategemea nini.

    ReplyDelete
  6. kwa nyongeza kwa anonymous wa 06.36 Jan 28: Uliyosema ni kweli, zaidi wanachotaka 'wazungu' ni mahali pa kufanyia majaribio ya GMO na kuuzia mbolea. Mimea wanayoiita ya kisasa 'GMO's' haioti kwenye udongo ulio na rutuba ya asili bila kutumia mbolea zao kali na ambazo ni sumu. Mkulima atadanganywa anapewa mbegu eti inazaa sana ili aache kutumia mbegu asili (kwa kisingizio cha kutotoa mazao ya kutosha) baada ya kupanda lazima aweke mbolea 'ya kununua'. Udongo baadaye unakuwa tegemezi - bila mbolea ya kununua huoteshi kitu bali uharibifu wa mazingira na kukithiri kwa umaskini
    Africa(target ni maeneo yenye rutuba eg Mbeya, Morogoro - ili wadidimize ukulima wa asili na kuhalalisha GMOs kama mkombozi)Tunabaki kushangilia Bill Gates/Kofi Annan wametutembelea - kalagabaho... At the same time, wao ardhi yao wamerudi kwenye 'organic farming for sustainable environment...' Viongozi wetu kuweni makini jamani!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...