Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Mstaafu Joseph Warioba akiongea na waandishi wa habari ofisi za Tume leo (Alhamisi, Agosti 9, 2012) kuhusu tathmini ya kazi ya Tume ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya. Kulia ni Katibu wa Tume Bw. Assaa Rashid na kushoto ni Naibu katibu Bw. Casmir Kyuki.
Mwandishi wa Habari wa Radio Deutch Welle Bi. Hawra Shamte akiuliza swali katika mkutano kati ya waandishi wa habari na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Mstaafu Joseph Warioba. Mkutano huo ulifanyika ofisi za Tume jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Mstaafu Joseph Warioba avitaka vyama vya siasa, asasi za kidini na wanaharakati kuacha kuwaelekeza wananchi aina ya maoni wanayopaswa kutoa kuhusu Katiba Mpya.

Jaji Warioba ameyasema hayo leo (Alhamisi, Agosti 9, 2012) katika mkutano wake na waandishi wa habari kuzungumzia tathmini ya mikutano ya awamu ya kwanza ya ukusanyaji wa maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya katika mikoa minane ya Pwani, Dodoma, Manyara, Kagera, Shinyanga, Tanga, Kusini Unguja na Kusini Pemba.

“Sio wanasiasa tu, watu wote wakiwemo viongozi wa kidini, wanaharakati na taasisi zisizo za kiserikali ziache kuwalazimisha wananchi watoe maoni wanayotaka wao. Wananchi wawe huru kutoa maoni yao,” alisema na kuongeza kuwa vyama vya siasa, asasi zisizo za kiserikali ziatapata muda wa kuwasilisha maoni yao Tume.

“Mwananchi akitoa maoni yake binafsi, anakuwa ‘very articulate’ (anajieleza kwa ufasaha), lakini akielekezwa cha kusema, na ukamuomba ufafanuzi, anashindwa hata kueleza,” alisema Jaji Warioba katika mkutano huo uliohudhuriwa na pia na Katibu wa Tume hiyo, Bw. Assaa Rashid na Naibu Katibu Bw. Casmir Kyuki.

Kuhusu idadi ya mikutano iliyofanyika katika awamu ya kwanza, Mwenyekiti huyo amesema Tume yake imefanya mikutano 386 katika mikoa minane ya awamu ya kwanza kwa muda wa mwezi mmoja.

“Wastani wa wananchi 188,679 walihudhuria mikutano hiyo ya Tume. Hii ikiwa ni wastani wa watu 489 walifika kwenye kila Mkutano,” alisema na kuongeza kuwa Tume inaridhika na idadi hii na inaonesha wananchi wana mwamko wa kutoa maoni yao.

Kati ya waliohudhuria, Jaji Warioba alisema, wananchi 17,440 walitoa maoni yao kwa njia ya kuzungumza kwenye mikutano hiyo na jumla ya wananchi 29,180 walitoa maoni yao kwa njia ya maandishi na kuyawasilisha kwenye Mikutano ya Tume.

Jaji Warioba aliongeza kuwa Tume ilipokea maombi na kufanya mikutano nane na makundi maalum yakiwemo Taasisi za Dini na Vyombo vya Ulinzi na Usalama katika awamu ya kwanza. 

“Kimsingi, Tume imeridhika na kazi ya ukusanyaji wa maoni katika awamu ya kwanza kwani mikutano yote iliyopangwa na Tume imefanyika na imefanyika kwa amani na utulivu na wananchi walivumiliana katika kutoa maoni yao,” alisema.

Akizungumzia changamoto, Mwenyekiti huyo alisema katika mikutano ya Tume, wanawake bado hawajitokezi kwa wingi kutoa maoni yao mbele ya Tume ingawa wanahudhuria mikutano hiyo na kusisitiza kuwa Tume itaendelea kuwahamasisha kutoa maoni yao kwa uhuru na uwazi.

Kuhusu kuanza kwa awamu ya pili ya mikutano ya kukusanya maoni, Jaji Warioba alisema kazi ya kukusanya maoni kwa awamu ya pili inatarajiwa kuanza rasmi tarehe 27 Agosti, 2012 na ratiba ya mikutano hiyo itatolewa na Tume hivi karibuni.

Akiongea katika mkutano huo, Naibu Katibu wa Tume hiyo, Bw. Kyuki alisema kuwa awamu ya pili ya kazi ya ukusanyaji maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya itafanyika katika mikoa saba ambayo ni Mbeya, Morogoro, Lindi, Ruvuma, Kigoma, Katavi na Mwanza.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. BONGO BONGO KAONA JAMAA WAMEMKOMALIA KICHWA SASA ANASEMA WASILAZIMISWE HE HE HE KAZI IPO KAREGEZA KAMBA YAKE BWANA MKUUU HA HA HA

    hatutasita au kuchoka mpaka kieleweke

    ReplyDelete
  2. Ili zoezi la kukusanya maoni ya Katiba Mpya yafanikiwe Tume ya kukusanya maoni ifanye kazi yake kwa uwazi zaidi(transparency),nikiwa na maana kwamba,kila wanapomaliza hatua fulani ya zoezi,"watoe taarifa ya nini kilichokusanywa kutoka kwa watanzania waliotoa maoni yao kupitia vyombo vya habari yakiwemo magazeti",ili kutoa fursa zaidi kwa wale ambao hawajafikiwa na tume waweze kutoa maoni ya kina zaidi na mbadala kwa kuziba mapengo pale palipokosekana na kuliongezea tija zaidi zoezi zima.Badala ya kusubiri hadi hatua ya mwisho ndipo watoe ripoti ya maoni itakayo rejeshwa kwa wananchi waweze kuidurusu tena na kutoa mapendekezo yao ya mwisho.Hili ni pendekezo tu ambalo linaweza kufanyiwa kazi.Vinginevyo,watanzania wapo gizani hawajui nini kinachoendelea,na wapi wanakolazimika kuziba mapengo ya mawazo.Zimebakia kauli za viongozi tu kwamba,"tumefikia pazuri,zoezi linaendelea bila ya tatizo,nk".Misimamo iliyotolewa na baadhi ya vyama vya siasa,mathalani,kutaka Muungano wa Serikali Mbili au Serikali Tatu,sio jambo sahihi katika hatua iliyopo sasa ya kutoa maoni.Walipaswa kusubiri hadi hatua za mwisho.Kila mtanzania achunge akili zake.Zoezi kama hili litakuja tokea tena pengine baada ya miaka Hamsini mingine kupita.Kwa hiyo chunga sana!

    ReplyDelete
  3. Michuzi naomba utujulishe website ambayo tuntukatoa mchango wetu sisi ambao hatukukutana na tume

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...