Juu na chini anaonekana Rais Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini ya Kikristo Ikulu jijini Dar es salaam leo ambapo amekuwa na mazungumzo nao ikiwa ni mojawapo ya jitihada za Rais Kikwete kutafuta muafaka na kutafuta utatuzi wa hali ya sintofahamu ambayo inanyemelea nchi yetu katika kipindi hiki.

 Rais Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika mazungumzo na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini ya Kikristo Ikulu jijini Dar es salaam leo
Rais Dkt Jakaya Mrisho Kikwete katika picha ya pamoja na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini ya Kikristo Ikulu jijini Dar es salaam leo. Kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano) Mhe Steven Wassira.
----

Viongozi wa dini wamewataka waumini kote nchini kulinda amani na  umoja uliopo  ili nchi isije ikaingia kwenye mgawanyiko wa kidini na kuleta machafuko hapa Tanzania.

Wito huo umetolewa na viongozi wa dini leo Ikulu ya Dar-Es-Salaam mara baada ya kikao cha pamoja baina ya viongozi wa dini na Rais Jakaya Kikwete.

Viongozi hao wa dini wamefika leo wakiongozwa na Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).

Viongozi wengine wametokea Baraza la Kikristo Tanzania (CCT) Seventh Day Advertist (SDA) na Baraza la Pentekoste Tanzania (PCT).

Mkutano huo umeanza kwa Askofu Ngalalekumtwa kusoma tamko lao la pamoja kwa Rais Kikwete ambalo ndilo limetoa muongozo wa mazungumzo hayo ya leo ambayo yamehusu Amani na Usalama wa Taifa na migogoro ya kidini ndani ya jamii.

Mkutano wa viongozi wa dini ya Kikristo Tanzania ni mojawapo ya jitihada za Rais Kikwete kutafuta muafaka na kutafuta utatuzi wa hali ya sintofahamu ambayo inanyemelea nchi yetu katika kipindi hiki.

“Nataka tuzungumze ni namna gani tunaweza kutoka kwenye hali hii na tunakwendaje mbele zaidi na kuhakikisha nchi yetu bado inakua ya  amani na umoja kama ilivyozoeleka” Rais amesema na kutoa nafasi kwa viongozi wa dini kutoa maoni yao.
Viongozi hao wa dini wamemueleza Rais Kikwete kuwa wanaunga mkono jitihada zake za kutafuta amani na kwa pamoja wamekubaliana uandaliwe mkutano wa pamoja baina ya viongozi wa dini zote ambapo masuala ya amani na umoja wa nchi utajadiliwa kwa kirefu.

Katika kikao cha leo pande zote zimekubaliana kuwa kuna changamoto zilizoko sasa zinahitaji kutatuliwa haraka iwezekanavyo ili kuepusha nchi kutumbukia katika mgogoro mkubwa zaidi, na pia kukubaliana kuwa pande zote, kwa maana ya serikali na taasisi za dini, zinawajibu mkubwa wa kuhakikisha amani inadumu.

Kabla ya kikao cha leo , Rais amewahi kukutana na viongozi wa dini ya kiislamu na kikristo mmoja mmoja ambapo alikua akitafuta maoni na ushauri wa pande zote kabla ya pande zote hazijakaa pamoja na kuwa na msimamo wa pamoja.

Kikao cha leo kimehitimisha jitihada hizo na kinachofuata ni mkutano mmoja ambapo Rais Kikwete atakutana na viongozi wa dini zote kwa pamoja hivi karibuni.

………...”MWISHO”……..

Imetolewa na:
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi,
Ikulu-DSM
23 Aprili, 2013


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. Baba askofu Kitula wakilisha AIC baba

    ReplyDelete
  2. amani ndiyo lulu pekee inayng'aa idumishwapo. Nchi ya tanzania inabahati kubwa kuliko nchi nyingine ulimwenguni kote hivyo lazima tujivunie kwa zawadi hiyo pekee tuliyoruzukiwa na muumba. Unaweza ukapoteza simu na ukanua nyingine kariakoo au laini ukairenew namba ile lakini katika vitu ambavyo ni Ghali kuvipata ukivipoteza, ni AMANI. Sitaki turudi nyuma tuanze kunyoosheana vidole huyu kafanya hili na huyu lile maana tutakosa kuelewana na tukikosa kuelewana huenda tukakosa AMANI. Chakufanya ni kwamba tufanye tunavyofanya tuhakikishe Amani tuliyonayo inadumu na sikupotea hata kwa bahati au kwa kujisahau. Mwenzemungu tunakuomba uibariki tanzania na watu wake bila ya kujali Madhehebu na dini za watu wake. Aaamiyn!

    ReplyDelete
  3. Amani haipatikani kwa kutumiliwa viongozi wa dini pekee. Ni haki na wajibu kwa serikali kuu na za mitaa kushajihisha amani kwa vitendo kwa kuwatendea haki watu wote kwa usawa na uadilifu.Bila kusahau uwajibikaji kwa kila jamii na taasisi mbalimbali.

    Vyama pia vinanafasi kubwa sana kusimamia amani kwani ndio vyenye muamsho wa kasi sana kulinganisha na dini.

    kwamtazamo huu sinashaka amani itadumu.

    ReplyDelete
  4. Kwa hy ma shekhe na ma ustadhi wao hawana maana? au mabubu? Jifikilie nyie.mxiuuuuuuuu viongozi wa ndo mnaoleta udini.Mungu awalaani wale wote wanaopiga vita waislam na uislam.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...