Mchezaji wa timu ya Azam FC ya jijini Dar es Salaam Shomary
Kapombe jana amekabidhiwa kitita cha shilingi Milioni 1/- kutokana na
kuibuka kuwa mchezaji bora wa ligi ya soka ya VPL inayoendelea kwa
kipindi cha mwezi Januari mwaka huu.
Kapombe amekabidhiwa kitita hicho kutoka kwa mdhamini wa waligi
hiyo Vodacom Tanzania katika uwanja wa klabu anayoichezea uliopo
maeneo ya Chamanzi,jijini Dar es Salaam.
Akiongea muda mfupi baada ya kukabidhiwa zawadi hiyo ikiwa ni tuzo
ya uchezaji bora,Kapombe alisema amefurahia kuwa miongoni mwa
wachezaji waliopata tuzo tuzo na kuongeza kuwa imezidi kumtia moyo
na bidii ya kujituma zaidi.
“Nashukuru Vodacom kwa kuwapatia zawadi wachezaji wanaofanya
vizuri kwa kuwa inawazidishia kasi ya kujituma zaidi,pia nawashukuru
wachezaji wenzangu wote wa Azam maana bila jitihada za pamoja sio
rahisi mchezaji mmoja ukaibuka na kuonekana bora kwa kuwa katika
mchezo wa soka sote tunategemeana”.Alisema.
Kwa upande wake Meneja Uhusiano wa Vodacom Tanzania,Matina
Nkurlu aliyeambatana na Ofisa wa Bodi ya Ligi, Joel Balisidya pamoja
na Ofisa Udhamini na Matukio wa kampuni hiyo, Ibrahim Kaude katika
kumkabidhi zawadi hiyo alimpongeza mchezaji huyo na kuongeza
kusema kuwa Vodacom inajivunia mafanikio yanayoendelea kupatikana
katika ligi hiyo na ina mpango wa kushirikiana na wadau wengine wa
soka kuzidi kuiboresha zaidi.
Kapombe alitwaa tuzo mwezi Januari uliokuwa na raundi tatu, alicheza
dakika zote 180 za mechi mbili za timu yake dhidi ya African Sports na
Mgambo Shooting.
Mechi ya tatu ya Azam FC katika raundi hiyo dhidi ya Tanzania Prisons
ilikuwa kiporo, na ilichezwa Februari 24, 2016.
Kapombe alifunga mabao yote mawili kwenye ushindi wa mabao 2-1 wa
timu yake dhidi ya Mgambo Shooting. Pia alisaidia kupatikana bao la
Azam kwenye mechi dhidi ya African Sports iliyomalizika kwa sare ya
bao 1-1, na mara nyingi mashambulizi ya timu yake yalianzia upande
wake.
Washindani wa Kapombe kwenye kinyang'anyiro hicho katika mwezi
huo walikuwa mshambuliaji wa Tanzania Prisons ya Mbeya, Jeremiah
Juma na beki wa Coastal Union ya Tanga, Miraji Adam.
Beki wa Azam FC, Shomari Kapombe (kushoto) akiwa ameshikilia hundi
yenye thamani ya Sh. Milioni 1/- kama tuzo ya mchezaji bora wa mwezi
Januari wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) jana katika
mazoezi ya timu yake,Kutoka kulia ni Ofisa wa Bodi ya Ligi (TPLB), Joel
Balisidya, Ofisa Matukio na Udhamini wa Vodacom, Ibrahim Kaude
pamoja na Meneja wa kikosi hicho, Luckson Kakolaki.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...