Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimsikiliza Balozi wa China hapa nchini Dkt. Lu Youqing Ikulu jijini Dar es Salaam. Balozi Dkt. Lu alifika Ikulu jijini Dar es Salaam kwa ajili ya  kuzungumza masuala mbalimbali ya kimaendeleo na Rais Dkt. Magufuli. 
 Balozi wa China hapa nchini Dkt. Lu Youqing akimkabidhi Rais Dkt. John Pombe Magufuli ujumbe wa barua ya kumpongeza kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  kutoka kwa Rais wa China Xi Jinping Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha na Balozi wa China hapa nchini Dkt. Lu Youqing wanne kutoka kushoto, Waziri wa Ujenzi Profesa Makame Mbarawa wapili kutoka kulia pamoja na maafisa wengine kutoka nchini na Ubalozi wa China.
Picha na IKULU.
KWA PICHA ZAIDI BOFYA HAPA.

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU

CHINA imekubali kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa reli ya kati yenye urefu wa kilometa 2,561 kwa kiwango cha kisasa yaani "Standard Gauge" ambao zabuni za ujenzi zinatarajiwa kutangazwa hivi karibuni.
Balozi wa China hapa nchini Mheshimiwa Dkt. Lu Youqing ametoa kauli hiyo leo tarehe 25 Aprili, 2016 Ikulu Jijini Dar es salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ambapo pia amemkabidhi barua yenye ujumbe kutoka kwa Rais wa China Mheshimiwa Xi Jinping.

Katika Mazungumzo hayo Rais Magufuli amemweleza Balozi Lu kuwa Tanzania imedhamiria kuanza ujenzi wa Reli ya kati haraka iwezekanavyo na tayari imetenga fedha kiasi cha shilingi Trilioni 1 katika bajeti yake ijayo kwa ajili ya kuanza awamu ya kwanza ya ujenzi huo.
"Tuna imani kuwa mradi huu utasaidia kuleta mapinduzi makubwa ya uchumi katika nchi yetu na katika nchi nyingine za Afrika Mashariki na kati zikiwemo Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ndio maana hatutaki kupoteza muda kwa mazungumzo marefu, tunataka kazi ianze na watu waanze kunufaika" Amesisitiza Rais Magufuli.
Kwa upande wake Balozi China hapa nchini Dkt. Lu Youqing amempongeza Rais Magufuli na serikali yake kwa kujiandaa kwa fedha, vifaa na rasilimali watu kwa ajili ya kutekeleza mradi huu mkubwa na kwamba Serikali ya China, Taasisi za fedha za China na Makampuni mbalimbali yatatoa ushirikiano wote katika utekelezaji wa mradi huu.

"Kama ambavyo Prof. Mbarawa amefanya mazungumzo na Serikali ya China, Taasisi za fedha za China na Makampuni, naahidi kuwa tutaanza kazi kama ambavyo taratibu na viwango vya ujenzi vimewekwa, tutafanya kazi kwa kujali muda, ubora na gharama nafuu" Amesema Balozi Lu.
Mradi mzima wa ujenzi wa reli ya kati unatarajiwa kugharimu Dola za Kimarekani bilioni 6.8 na umepangwa kutekelezwa kwa awamu ambapo awamu ya kwanza itahusisha ujenzi wa kilometa 1,216 za kutoka Dar es salaam - Tabora - Isaka - Mwanza na itajengwa kwa ushirikiano wa Tanzania na China.
Tayari Rais Magufuli amemtuma Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa Mnyaa kwenda nchini China kukamilisha mazungumzo juu ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ukiwemo wa ujenzi wa reli ya kati, ambapo Prof. Mbarawa anasema hatua inayofuata sasa ni kutangaza zabuni ya ujenzi wa reli hiyo kwa uwazi, ili makampuni mbalimbali ya ujenzi yaombe na hatimaye kupata washindi watakaoanza kazi mara moja.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
25 Aprili, 2016.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. The mdudu, Asante sana rais wetu mpendwa John Pombe Magufuli hakuna mchezo#hapakazi2

    ReplyDelete
  2. Hii ni zaidi ya safi. Safi sana tena sana. Hakuna kupoteza muda. Nakubali kwa asilimia mia kujenga vipande vipande. Mbele ya safari wawekezaji kwa mfumo wa PPP watajitokeza tu. Safi sana Rais wetu. Mungu akulinde.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...