Katika kuadhimisha siku arobaini za maombolezo, familia ya Marehemu Jessie Mgeni Chiume (pichani) inapenda kuwataarifu na kuwakaribisha ndugu, jamaa, marafiki na wanajumuiya wote kwa ujumla katika shughuli ya kutoa shukrani, kukumbuka na kusherehekea maisha ya Dada yetu mpendwa aliyetangulia mbele ya haki tarehe 24 Februari mwaka huu.
Shughuli hiyo itafanyika nyumbani kwa mdogo wake Marehemu, Fair Lawn, New Jersey siku ya Jumamosi tarehe 9 Aprili, 2016:
Anuani ya shughuli:
3-11 Linden Lane
Fair Lawn, NJ 07410
Muda: Saa 8 Alasiri - Saa 12 Jioni (2pm-6pm)
Kwa mara nyingine tena familia ya Mzee Kanyama Chiume (RIP), inapenda kutanguliza shukrani zake za dhati kwa ndugu na marafiki popote pale mlipo, hususan Marekani, Tanzania na Malawi, kwa ushirikiano mkubwa mliotupa tangu siku msiba wa Dada yetu Jessie ulipotufika ghafla. Tumefarijika sana na sala zenu na maombi yenu kwetu pamoja na salamu nyingi za pole mlizotuma. Tunawashukuru kwa kila aina ya msaada mliotupa na kwa kutuonyesha upendo wa kweli katika kipindi hichi kigumu kwetu. Ni dhahiri msiba huu haukuwa wetu peke yetu, ulikuwa wetu sote. Tumeona ushuhuda wa jinsi gani ambavyo wengi wenu mlivyoishi kwa upendo na Dada Jessie, na jinsi yeye alivyoishi kwa upendo na nyie. Msaada wenu mkubwa mlioutoa ulifanikisha mipango ya mazishi na kuwezesha familia kumsindikiza nyumbani Tanzania dada yetu mpendwa na kumhifadhi katika nyumba yake ya milele katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam mnamo tarehe 5 Machi.
Familia inawashukuru pia viongozi na wanajumuia wote wa NY, NJ, CT na PA pamoja na States zingine kwa kuacha shughuli zao muhimu na kuwa nasi katika maombolezo. Vile vile tunamshukuru sana Balozi Tuvako Manongi na Ofisi ya Ubalozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, NY kwa kuwa pamoja nasi na kwa msaada wao mkubwa waliotupatia katika kukamilisha taratibu za safari. Tunaishukuru pia Wizara ya Mambo ya Nje kwa ujumbe rasmi wa rambirambi kupitia Balozi Ramadhani Mwinyi, pamoja na Idara ya Diaspora, kwa mapokezi yao Uwanja wa ndege wa Dar es Salaam na kwa kushiriki kwao mazishi kupitia wawakilishi wao, Balozi Modest Mero na Balozi Liberata Mulamula.
Shukrani pia zimfikie aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue na Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Wilson Masilingi kwa salamu zao za pole. Vile vile tunamshukuru Balozi wa Malawi katika Umoja wa Mataifa NY, Brian Bowler kwa salamu za pole na pia Balozi Mdogo wa Malawi nchini Tanzania, Kwacha Chisiza kwa kuhudhuria mazishi. Shukrani zetu pia ziwafikie Wachungaji Mama Perucy Butiku na Carol Fryer wa NY pamoja na Mchungaji Prudence Chuwa wa Usharika wa Kilutheri wa Azania Front, Dar es Salaam kwa uongozi wao wa kiroho. Tunashukuru pia Kanisa la Holy Trinity Lutheran Church na Flynn Memorial Home za Yonkers, NY kwa msaada mkubwa waliotupatia.
Tunamshukuru pia Tumaini Kaisi-Katule kwa kuongoza vizuri shughuli iliyofanyika Yonkers, NY. Kwavile hatuwezi kuwataja wote mmoja mmoja, tunaomba mpokee shukurani zetu kupitia ujumbe huu kama ishara ya kutambua uwepo wenu na msaada wenu mkubwa kwetu ambao sio rahisi kuulipa. Tunasema ahsanteni sana.



Kwa taarifa zaidi wasiliana na:
Michael Chiume  646-662-6999
Chris Lutinwa 614-592-6231
Nathan Chiume 646-552-6347
Hajji Khamis 347-623-8965

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...