Zikiwa zimebaki siku chache kabla ya kuanza kwa kipindi cha mpito cha mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), watumiaji wa vyombo vya usafiri wametakiwa kutotumia njia maalum za mradi huo.
Mradi huo unatarajiwa kuanza kufanya kazi tarehe 10 Mwezi ujao na kuendeshwa na kampuni  ya UDA Rapid Transit (UDA-RT).
Msemaji wa Kampuni ya UDA-RT, Bw. Sabri Maburuki amesema jana kuwa “Wananchi waheshimu njia za mabasi hayo kwani itasaidia kuepukana na ajali na wepesi wa kuendesha mradi huo.”
Kwa sasa madereva wa mabasi ya mradi huo wanafanya mazoezi tayari kwa kuanza kwa mradi huo.
Alisema pamoja na kupigwa marufuku, bado kuna baadhi ya vyombo vya usafiri kama magari, bodaboda, bajaji na maguta yanapita katika barabara hizo huku mabasi yakiwa yanafanya mazoezi.
Alisema miundombinu ya mradi huo imejengwa kulingana na mahitaji, hivyo kila chombo cha usafiri kipite na waenda kwa miguu wapite katika njia zilizotengwa.
Akitoa mfano wa kutoheshimu taratibu alisema tayari mabasi manne ya mradi huo yameshakwanguliwa na vyombo vingine katika kipindi hiki cha mazoezi.
“Sheria za mabasi haya ni kama treni, yule aliyegongwa au kagonga basi ndiye mwenye kosa,” alisema.
Alisema tayari mabasi yana madereva waliofuzu, yamekatiwa bima na nauli zinatarajiwa kutangazwa hivi karibuni na Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA).
Alisema katika kudhibiti ulinzi wa vituo na mabasi, wamefunga kamera kwa ajili ya kubaini watu wenye nia mbaya ya kuhujumu miundombinu hiyo.
Mradi wa BRT unatarajiwa kupunguza kwa kiwango kikubwa tatizo la usafiri katika jiji la Dar es Salaam linalokadiriwa kuwa na watu milioni tano.
Msemaji wa Kampuni inayotarajiwa kuendesha mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) katika kipindi cha mpito, UDA-RT, Bw. Sabri Maburuki akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuhusu kuheshimiwa kwa njia za mabasi hayo ili kusaidia kuepukana na ajali na wepesi wa kuendesha mradi huo unaotarajiwa kuanza tarehe 10 mwezi ujao.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. Watanzania wengi ni vichwa maji. Kazi yao kulalamika tu kwenye vyombo vya habari. Wakiwekewa mifumo mipya wanaiharibu. Ni aibu sana kutoipenda nchi yako.

    ReplyDelete
  2. KItu muhimu kwa Serikali ni ku-wapiga faini kubwa, kwa wale wanao bainika na makosa ambayo tayari Serikali imesha-ainisha. na wale wasioweza kulipa vyombo vyao, viondolewe barabarani mpaka walipe hizo faini. na Serikali ijiandae kwa sehemu maalum kwa ijiri ya kuyayusha vyuma chakavu, kama magari, pikipiki, baiskeli, n.k

    Wakipata hasara za kutosha' Watafuata Sheria !

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...