Jeshi la Ulinzi
la Wananchi wa Tanzania linapenda kutoa taarifa ya ufunguzi wa mashindano
ya kombe la Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF
CUP) ambayo yanatarajiwa kufunguliwa rasmi tarehe 24 Mei 2016 katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam. Mgeni
rasmi katika ufunguzi huo anatarajiwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo, Mhe. Nape Nnauye.
Mashindano haya yalianzishwa mwaka 2014, awali
JWTZ lilikuwa likiteua wanamichezo wa kushiriki michezo ya kimataifa kupitia
timu teule za Jeshi hali iliyopelekea kutovumbuliwa kwa vipaji vipya katika
michezo, ikaonekana upo umuhimu wa kubadili mfumo wa uteuzi. Hivyo kuanzisha
mashindano ya Kombe la Mkuu wa Majeshi (CDF CUP) ambayo huanzia ngazi za
vikosi hadi kufikia ngazi za brigedi.
lengo la mashindano
haya ni kudumisha mshikamano, kuvumbua na kukuza vipaji, pia mashindano hayo
yatatumika katika kuteua kombaini ya timu ya JWTZ itakayoliwakilisha Jeshi na Taifa
kwa ujumla katika mashindano ya michezo ya majeshi na utamaduni kwa nchi za
Jumuiya ya Afrika Mashariki yanayotarajiwa kufanyika nchini Rwanda mwezi wa
nane mwaka huu.
Kauli Mbiu ya
mashindano haya ni “Michezo ni Ulinzi na
Umoja Daima”
Timu zinazoshiriki
mashindano haya ni Ngome (Makao Makuu JWTZ), Kamandi ya Jeshi la nchi kavu ikiwakilishwa
na timu za Tembo, Faru, Nyuki, Mbuni na Chui, Kamandi ya Jeshi la Anga, Kamandi
ya Jeshi la Wanamaji pamoja na Jeshi la Kujenga Taifa(JKT).
Mashindano haya yatahusisha michezo
ifuatayo, Mpira wa miguu kwa wanaume, Mpira wa kikapu kwa wanaume, Mpira wa mikono kwa wanaume, Mpira wa
pete kwa wanawake na Mbio za nyika kwa wanaume na wanawake.Michezo hii
itafanyika katika viwanja vya Twalipo vilivyopo Mgulani pamoja na uwanja wa
Uhuru jijini Dar es salaam.
Mashindano haya yanatarajiwa
kufungwa rasmi tarehe 06 Juni 2016. Mgeni
rasmi katika ufungwaji wa mashindano haya anatarajiwa kuwa Mkuu wa Majeshi ya
Ulinzi Tanzania Jenerali Davis Mwamunyange.
Wananchi wote wanakaribishwa. Hakuna
kiingilio.
Imetolewa na Kurugenzi
ya Habari na Uhusiano
Makao Makuu ya Jeshi, Upanga
S.L.P 9203, Dar
es Salaam, Tanzania.
Kwa Mawasiliano zaidi: 0756716085/
0713506757
Ni aibu kubwa kwa jeshi la ulinzi wa nchi yetu kutuimia anwani ya baruapepe ya yahoo.co.uk/ ambayo ni ya bure na huku likiwa na tovuti yake kamili.
ReplyDelete