Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi amekabidhi hati miliki za
ardhi 1,361 kwa wakazi wa vijiji vya Hembeti na Dihombo wilayani Mvomero mkoani
Morogoro.
Waziri Lukuvi amegawa
hati hizo na kuwasisitiza wananchi wa wilaya ya Mvomero kuhakikisha wanapata
hati za umiliki wa ardhi pamoja na kuwataka viongozi wa vijiji kote nchini kuhakikisha
wanakuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi ili kuepusha migogoro ya wakulima
na wafugaji kuendelea katika maeneo yao.
Pia amesema ili mwananchi
aweze kujikimu kimaisha ahakikishe anazitumia hati miliki hizo za kimila
kujiletea maendeleo na anaweza kuomba mkopo benki kwa kutumia hati hiyo ili
kuendesha shughuli zake za kujipatia kipato kupitia eneo analomiliki kisheria.
Nae Mkuu wa Mkoa wa
Morogoro Dkt. Stephen Kebwe amewataka wananchi kuzitunza hati hizo walizokabidhiwa
na kuyatumia mashamba yao waliyomilikishwa kwa kuyalima na sio kuyauza au
kukodisha kwa watu wengine na wao kubaki masikini.
Waziri Lukuvi pia alimtaka
Mkuu wa mkoa wa Morogoro ayaainishe mashamba mengine makubwa yasiyoendelezwa na
kugeuka kuwa mashamba pori ili amshauri Rais kuyafutia umiliki wa mashamba hayo
na kurudishwa kwao ili kuweza kuwapa kaya maskini ambazo zinaishi katika maeneo
ya hayo.
Kazi hii ya upimaji wa
maeneo na kutoa hati kwa wananchi ni katika mpango wa nchi wa matumizi bora ya
ardhi,ambapo serikali imechangua Mkoa wa Morogoro kuwa wa Mfano katika upimaji
wa ardhi na utahusisha nchi nzima kwa wapimaji wa ardhi kutumia vipimo vya
kisasa zaidi ambavyo kwa kiasi kikubwa vipimo hivyo vitaweza kupima ardhi kwa
kipindi kifupi na kila mtu kumiliki kipande cha eneo lake.
Lukuvi alisema kuwa wakati
wa kampeni mwaka 2015,Rais Dkt. John Magufuli alihaidi wazi kuwa kipindi cha
miaka 10 kutakuwa na upimaji katika maeneo yote ya nchi kwa utaratibu wa mpango
mzuri na wa kisasa, na kwa miaka mitano takribani vijiji 7,500 vitapimwa kwa kupangwa kila halmashauri 25
ambapo na kila mwaka vitapimwa vijiji 1,500 na kutoa hati. Alisema kuwa zoezi
la upimaji linaloendelea hivi sasa ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya Chama
cha Mapinduzi (CCM)kwa wananchi katika kuondoa migogoro inayojitokeza.
Na Hassan Mabuye (Kitengo cha Mawasiliano Serikalini - Wizara ya Ardhi).
Mzee Ali Juma mkazi wa kijiji cha Hembeti
wilayani Mvomero mkoani Morogoro akimshukuru Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi kumuwezesha kupata hati ya kumuliki
ardhi yake ambayo amekuwa nayo kwa miaka mingi bila kupewa hati hiyo, kushoto
ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Stephen Kebwe na kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa
Tume ya Taifa ya Mipango na Matumizi ya Ardhi (NLUPC), Dkt. Stephen Nindi anayemsaidia
kwa kumshika mkono.
Bi. Zaina Hussein mkazi wa kijiji cha Dihombo
wilayani Mvomero mkoani Morogoro akipokea hati ya kumuliki ardhi kutoka kwa Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi, kushoto ni Mkuu wa
Mkoa wa Morogoro Dkt. Stephen Kebwe.
Bibi. Magret Hamis mkazi wa kijiji cha Hembeti
akipokea hati ya kumuliki ardhi kutoka kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi Mhe. William Lukuvi, kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Stephen
Kebwe.
Baadhi wa wakazi wa vijiji vya Hembeti
na Dihombo wilayani Mvomero mkoani Morogoro wakiwa hati zao za kumuliki ardhi
mbele Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi na Mkuu
wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Stephen Kebwe.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...