MAAFISA Habari na Mawasiliano Serikalini wametakiwa kutoa taarifa kwa haraka zaidi kwa kutumia njia za kisasa za mawasiliano ikiwemo tovuti na mitandao ya kijamii ili kusaidia kutangaza Mafanikio ya Serikali katika maeneo yao ya kazi.
Hayo yamesemwa jana Mkoani Dodoma na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi, alipokuwa akizungumza na maafisa habari na TEHAMA katika mafunzo elekezi ya uwekaji wa taarifa katika tovuti yanayofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID) na kusimamiwa na Ofisi ya Rais- TAMISEMI na Wakala ya Serikali Mtandao (EGA).
Dkt. Abbas alisema kuwa mara baada ya tovuti kuzinduliwa rasmi, Maafisa Habari wana wajibu wa kuweka taarifa mpya zinazozingatia muda na wakati kwa kuwa malengo ya tovuti hizo ni kumsaidia mwananchi kuweza kupata taarifa mbalimbali za Serikali.
“Tukifungua tovuti hizi tunapaswa kuona taarifa mpya, kwa sasa suala la upashanaji wa habari na taarifa za miradi ya Serikali isisubiri tena michakato, isipokuwa kama kutatokea suala kubwa ambalo litahitaji ufafanuzi kutoka katika ngazi za juu katika maeneo yenu ya kazi” alisema Dkt. Abbasi
Aliongeza kuwa, taaluma ya habari katika zama za sasa inahitaji ubunifu mkubwa katika kuisemea Serikali kwa kutafuta njia mbalimbali za kubaharisha umma badala ya kutumia njia za kawaida na za kila siku.
“Katika maeneo yetu ya kazi tuna vituo vya redio na televisheni ambazo zinawahitaji Viongozi wetu kufanya nao mahojiano maalum kuhusu masuala mbalimbali ya Serikali, ni wajibu wetu kutumia fursa hizo kuhakikisha tunaisemea Serikali” alisema Dkt. Abbasi.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...