Imeelezwa kuwa kukamilika kwa ukarabati wa meli ya MV Umoja kutarudisha huduma ya usafirishaji wa mizigo katika kanda ya ziwa kupitia bandari ya Kemondo iliyopo mkoani Kagera.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, wakati akikagua Bandari hiyo kuangalia maendeleo yake, na kuitaka Mamlaka ya Bandari Nchini (TPA), Shirika la Reli Nchini (TRL), na Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), kuanza kuandaa Mfumo mmoja wa kutoa Stakabadhi ili kuwarahisishia wateja wake huduma za usafirishaji wa mizigo.
Aidha, Waziri Mbarawa ameitaka TRL kukarabati njia za reli bandarini hapo haraka iwezekanavyo ili kuruhusu mizigo itakayokuja ikiwa kwenye mabehewa kwa njia ya meli iweze kupakuliwa pindi Meli hiyo itaposhusha.
“Serikali imefanya ukarabati wa meli ya MV Umoja ambayo itabeba mizigo ikiwa kwenye mabehewa na reli hii inahitaji ukarabati mapema ipasavyo nawaagiza TRL kufanya ukarabati wa reli ili kusiwepo usumbufu wowote wakati wa kushusha na kupakia mizigo hiyo” , amesema Profesa Mbarawa.
Ameiagiza Mamlaka hiyo kuanza kutafuta tena wateja ambao kwa muda mrefu walikuwa wamepotea kutokana na bandari hiyo kusuasua kutoa huduma zake kwa muda mrefu.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (katikati), akielekea kukagua Bandari ya Kemondo mkoani Kagera ili kujionea utendaji kazi wake. Kulia ni Meneja wa Bandari Kanda ya Ziwa, Bw. Abel Moyo.
Muonekano wa gati ya meli katika Bandari ya Kemondo, mkoani Kagera.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa Kaimu Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), mkoani Kagera Eng. Zephrine Bahyona, alipotembelea na kukagua kivuko cha Kyanyabasa kinachotoa huduma katika mto Kyanyabasa, mkoani Kagera.
Muonekeano wa kivuko cha Kyanyabasa kinachotoa huduma katika mto Kyanyabasa, mkoani Kagera. Kivuko hicho kina uwezo wa kubeba watu sitini au magari mawili madogo kwa wakati mmoja.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...