Makamo
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewagiza wasomi nchini kwa
kushirikiana na wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuzifanyia tathmini za
kitaalamu mara kwa mara skuli walizosoma kwa lengo la kuzisaidia kupata
maendeleo endelevu ya elimu.
Balozi
Seif ameyasema hayo wakati akiwahutubia wananchi wa Nungwi wakati wa
kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Skuli ya Nungwi ambayo aliwahi kuwa
mwalimu Mkuu wa kwanza.
Makamo
wa Pili amesema tathmini ni nyenzo muhimu ya kielimu itakayozisaidia Skuli na
wataalamu wa Elimu nchini kurekebisha mapungufu yaliyopo kwenye Skuli
hizo kwa wakati pamoja na kujipangia mikakati mipya ya kurekebisha mapungufu
hayo.
Amesema
utoaji wa elimu na tathmini ni vitu vinavyokwenda sambamba na kwa kuanzia
amewagiza wasomi wa Nungwi kumpatia tathmini ya kitaalamu ya Skuli yao ndani ya
wiki tatu.
Akizungumzia
elimu kwa jumla katika kijiji cha Nungwi balozi Seif amewahimiza wanafunzi wa
Skuli hiyo kupania katika masomo yao ili kuendelea na masomo ya juu.
Amesema
Nungwi imebarikiwa na mazingira mazuri yanayowavutia wageni kuwekeza katika
sekta ya utalii jambo ambalo linatoa fursa nyingi za ajira kwa vijana.
Hata hivyo Balozi Seif amesema fursa hizo hazitopatikana kwa wanaNungwi ikiwa
hawatajibiidisha katika masomo yao.
Amesema
fahari ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuona hoteli zote za Nungwi
zinaendeshwa na vijana wa Nungwi, kwa hivyo amewataka vijana hao kujiunga na
vyuo vya utalii nchini kwa wingi kwa mafunzo ya shahada ya utalii.
Wakati
wa sherehe hizo za miaka 50 ya kuanzishwa Skuli ya Nungwi Makamo wa pili wa
rais Balozi Seif Ali Iddi alipata nafasi kuweka
jiwe la msingi la ukumbi wa kufanyia mitihani mradi ambao unaendeshwa
kwa nguvu za wananchi na wafadhili mbali mbali chini ya usimamizi wa Taasisi ya
Maendeleo ya Elimu ya Kijiji cha Nungwi (TAMEN)
Akimkaribisha
Makamo wa Pili wa Rais, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mhe. Riziki Pembe
Juma amewataka wananchi wa Nungwi kushikiana kwa hali na mali katika miradi
mbali mbali ya skuli ikiwemo ujenzi wa ukumbi wa kufanyia mitihani, ujenzi wa
mabanda ya madarasa na ujenzi wa ukuta ambao utakuwa ni uzio wa eneo
linalozunguka skuli.
Amesema
maendeleo ya elimu hayawezi kupatikana bila ya mashirikiano ya wanajamii na
kuwasihi wanaNungwi kushikamana katika kuwasomesha vijana wao.
Aidha
Waziri huyo wa Elimu amezitaka skuli zote nchini kuimba wimbo wa sisi sote
wakati wa paredi kama ilivyokuwa zamani
na kusisitiza kuwa skuli itakayoshindwa kutii amri hiyo itachukuliwa hatua.
Makamo wa pili wa rais Balozi Seif Ali Iddi akiweka jiwe la msingi la ukumbi wa kufanyia mitihani ikiwa ni kumbukumbu ya Skuli ya Nungwi kutimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. Makamo wa Pili alikuwa mwalimu Mkuu wa kwanza kusomesha skuli hiyo
Kikundi cha Sarakasi cha vijana wa Nungwi kikitoa burudani kwa mgeni rasmi na wageni waalikwa
wanafunzi wa Nungwi waliofurika kusherehekea miaka 50 ya skuli yao tangu kuanzishwa
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...