RAIS wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Pierre Nkurunziza ametembelea maonyesho ya kwanza ya biashara ya Tanzania nchini hapa yanayolenga kuangalia soko pana la bidhaa zinazotengenezwa na wajasiriamali kutoka Tanzania na kusifu ubora wa bidhaa hizo. 
Maonyesho hayo yaliyofanyika katika viwanja vya Tempete vilivyopo jijini Bujumbura, yalianza Septemba 28 mwaka huu na yamekamilika leo Oktoba 1, mwaka huu yameandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kwa lengo la kuongeza fursa za kibiashara katika nchi za ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati. 
“Hii ni ishara ya kukomaa kwa udugu kati ya Tanzania na Burundi, wananchi wa Burundi walikuwa wakisafiri umbali mrefu kufuata bidhaa hadi Dar es Salaam, lakini sasa wameletewa mlangoni. 
"Kwa muda mrefu tumekuwa tukifurahia bidhaa aina hii lakini bei zilikua kubwa kutokana na gharama za usafiri, kwa sasa mambo yamekua mazuri,” alisema Rais Nkurunziza. 
Rais Nkurunziza aliongeza kuwa: “Uhusiano wetu unazidi kuimarika, naaminiile dhana ya utangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki inatekelezwa kivitendo. Naahidi kuunga mkono juhudi zote za kuimarika kiuchumi kati ya nchi mbili hizi.” 
Aidha, ubalozi wa Tanzania nchini Burundi kwa kiasi kikubwa umeshiriki kufanikisha maonyesho haya chini ya Balozi Rajabu Gamaha ambaye ndiye aliyewashawishi maofisa wa TanTrade kuwa na maonyesho aina hii kutokana na maombi ya kupata bidhaa kutoka Tanzania kuwa mengi ofisini kwake. 
Awali katika hotuba yake ya ufunguzi Septemba 27 mwaka huu, Makamu wa Pili wa Rais nchini hapa, Dkt. Joseph Bitore alisema biashara ni kitu kinachounganisha mataifa mawili kiuchumi hivyo watachukulia maonyesho hayo kujifunza lakini pia kutanua wigo wa mahusiano ya kiuchumi kati ya Tanzania na Burundi. 
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TanTrade, Mhandisi Christopher Chiza alisema, uamuzi wa kupeleka bidhaa Burundi ulipofika mezani kwake hakutaka kusita kwa sababu alijua hiyo ni njia pekee ya kufikisha mbali bidhaa za kitanzania. 
“Tunapofanikiwa kufika Burundi maana yake tunalenga soko pana la ukanda huu, tunatarajia kufikia soko la Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa sababu hata wao tumearifiwa kuwa wananunua bidhaa kutoka Burundi. “Kwa muda mrefu kama alivyoeleza mheshimiwa Rais Nkurunziza, wajasiriamali kutoka Burundi wamekuwa wakifuata bidhaa za vyakula hasa nafaka na mavazi kutoka pembezoni mwa mikoa ya Tanzania, lakini na wao walikuwa wakipeleka bidhaa hizo Mashariki ya Kongo. Hivyo tunalenga soko pana la takriban watu milioni 20, si jambo dogo.” 
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Bwana Edwin Rutageruka aliahidi kuendeleza biashara kati ya Tanzania na Burundi hata baada ya kumalizika kwa maonyesho hayo ya siku nne: “Huu ni mwanzo, tayari wafanyabiashara tulioongozana nao wamechukua mawasiliano ya wateja wao na watawauliza wanahitaji nini ili baadaye walete.” Kwa muda mrefu sasa TanTrade wamekuwa katika harakati za kuondoa dhana kuwa maonyesho ya biashara yanafanyika jijini Dar es Salaam tu, hivyo wametanua mipaka ambapo wiki kadhaa zilizopita yalifanyika maoneyesho makubwa ya kibiashara mkoani Kigoma na bado maonyesho mengine yanaandaliwa katika mikoa ya pembezoni ili kuwafikia watanzania wengi zaidi.
Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi akiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) Mhandisi Chistopher Chiza, Balozi wa Tanzania nchini Burundi Rajabu Gamaha pamoja na Kaimu Mkurugenzi Mkuu TanTrade, Edwin Rutageruka kuelekea kwenye banda la Tanzania katika maonyesho ya kimataifa ya biashara yanayoendelea katika viwanja vya Tempete jijini Bujumbura mwisho mwa wiki.
 Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi akipatiwa maelezo kuhusu bidhaa za Tanzania kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu TanTrade, Edwin Rutageruka alipotembelea banda la Tanzania katika maonyesho ya kimataifa ya biashara yanayoendelea katika viwanja vya Tempete jijini Bujumbura mwisho mwa wiki.
Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi akifurahia jambo kuhusu bidhaa za Tanzania alipotembelea banda la Tanzania katika maonyesho ya kimataifa ya biashara yanayoendelea katika viwanja vya Tempete jijini Bujumbura mwisho mwa wiki.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...