Na Said Mwishehe,Globu ya jamii
SHIRIKA la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) Mkoa wa Temeke jijini Dar es Salaam limetoa mashine za kupima shinikizo la damu 12 zenye thamani ya Sh.5,000,000 kwa Hospitali ya Wilaya ya Temeke kwa lengo la kuboresha utoaji huduma hospitali hapo.
NSSF imesema vifaa tiba hivyo vitatumika kwa Watanzania wote watakaofika kupata tiba Hospitali ya Wilaya ya Temeke.Pia vitatumika kutoa huduma kwa wanachama wao wapatao 4000 ambao wanatibiwa hapo.
Akizungumza leo katika hosptali hiyo baada ya kukabidhi mashine hizo Kaimu Meneja Kiongozi wa NSSF Mkoa wa Temeke Barnabas Ndunguru amesema wametoa msaada huo kutokana na maombi ya hospitali hiyo.
Pia amesema msaada huo ni moja ya jukumu la NSSF katika kurudisha fadhila kwa jamii ikiwa ni jitihada za kuisaidia Serikali katika juhudi za kuboresha sekta ya afya nchini.
Amefafanua NSSF Mkoa wa Temeke idadi ya wanachama wake wanaopatiwa huduma katika hospitali hiyo ni 4000 na kwa mwezi wanatoa fedha Sh.milioni 42 kwa ajili ya kulipia matibabu hayo."Hivyo tunaamini kutoa msaada huu wa BP Mobile Machine utasaidia katika kuwatibu wanachama wetu pamoja na wananchi wote ambao watakwenda kupata tiba,"amesisitiza.
Ameongeza msaada huo si mwisho na kuahidi kuendelea kusaidia kadri watakavyoweza kulingana na nafasi yao na kueleza wamekuwa wakisaidia jamii katika maeneo mbalimbali.Pia Ndunguru amesema NSSF wanalo fao la matibabu na kinachofurahisha zaidi wanachama wao wamekuwa wakipata huduma za afya za magonjwa yote isipokuwa TB na Ukimwi ambayo hayo huduma zake Serikali inatoa bure.

Kaimu Meneja Kiongozi wa NSSF Mkoa wa Temeke jijini Dar es Salaam Barnabas Ndunguru (wa pili kulia) akimkabidhi Ofisa Muuguzi wa Hosptali ya Temeke,Deodata Msoma vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni tano

Picha ya pamoja

Kaimu Meneja Kiongozi wa NSSF Mkoa wa Temeke jijini Dar es Salaam Barnabas Ndunguru (kulia) akizungumza na waandishi wa habari katika hafla ya kukabidhi vifaatiba kwenye Hosptal ya Wilaya ya Temeke vyenye thamani ya shilingi Milioni tano .(Picha na Emmanuel Massaka wa Globu ya jamii)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...