Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro akiimba wimbo pamoja na
Askari wakati wa kikao chake na Askari wanafunzi katika Chuo cha Polisi
Zanzibar wakati wa ziara yake. Kulia kwake ni Kamishna wa Polisi
Zanzibar Mohamed Hassan Haji na kushoto ni Mkuu wa Utawala na Fedha
Kamisheni ya Polisi Zanzibar Faustine Shilogile.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro akisalimiana na Maofisa
wa Polisi Kamisheni ya Zanzibar wakati wa Ziara yake inayoendelea katika
Vyuo vya Polisi hapa nchini kwa lengo la kuboresha elimu inayotolewa na
vyuo hivyo
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro akizungumza na Mafundi
wa Nguo za Polisi waliopo katika Kiwanda cha Polisi cha kushona nguo
Kamisheni ya Polisi Zanzibar wakati wa Ziara yake inayoendelea katika
Vyuo vya Polisi hapa nchini kwa lengo la kuboresha elimu inayotolewa na
vyuo hivyo (Picha na Jeshi la Polisi).
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro amewataka Wakufunzi wa
Vyuo vya Polisi vya Dar es Salaam na Zanzibar kuhakikisha
wanawafundisha Askari Polisi Wanafunzi waliopo katika vyuo hivyo kwa
kuzingatia mitaala iliyotolewa ili wanapotoka waweze kuwatumikia
Wananchi na kupunguza uhalifu hapa nchini.
IGP Sirro ameyasema hayo kwa nyakati tofauti wakati wa ziara yake
katika vyuo hivyo ambapo alizungumza na Wakufunzi pamoja na Askari
wanafunzi wanaosomea vyeo mbalimbali ambapo lengo la ziara hiyo ni
kukagua muenendo wa mafunzo katika vyuo vya Polisi.
Amesema lengo la mafunzo yanayotolewa katika vyuo hivyo yanapaswa
kutolewa kwa weledi ili kila Askari anayehitimu aweze kupata maarifa
ambayo yatawezesha kufanya kazi za Polisi vyema jambo ambalo
litaendelea kupunguza uhalifu hapa nchini.
“Kila mkufunzi anapaswa ahakikishe lile somo analolifundisha wanafunzi
wake wanalielewa ili kusudi kama ni Ofisa, Mkaguzi na Kiongozi mdogo
ndani ya Jeshi la Polisi anafanya kazi kwa kufuata ile misingi iliyopo”
Alisema Sirro.
Kwa Upande wake Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam
Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Anthony Rutta amesema lengo la
mafunzo katika Chuo hicho ni kuhakikisha kila Askari anayatambua
majukumu yake ili kupunguza uhalifu hapa nchini na watahakikisha
ukakamavu na nidhamu inazingatiwa ili kuwa na Jeshi lenye kufuata kanuni
na taratibu zilizopo.
Naye Mkuu wa Chuo cha Polisi Zanzibar Naibu Kamishna wa Polisi (DCP)
Geofrey Kamwela amesema Chuo hicho kinakabiliwa na Changamoto
mbalimbali zikiwemo za uchakavu wa miundombinu yakiwemo majengo na
bwalo la Chakula ambapo IGP Sirro aliahidi kutuma fedha za awali kwa ajili
ya ujenzi wa bwalo la kulia chakula chuoni hapo.
Kamwela alisema hivi sasa wanaendelea kutekeleza mradi wa kuweka
mfumo wa Tehama ambao utawezesha wanafunzi kujisomea na kupata
matokeo yao kwa njia ya mtandao jambo ambalo litawafanya kwenda
kisasa katika utoaji wa elimu chuoni hapo.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini yupo katika ziara ya kukagua mafunzo
yanayoendelea katika vyuo vya Polisi hapa nchini ili kuhakikisha kuwa
mafunzo yanayotolewa yanawajenga Maofisa na Askari kufikia malengo
yaliyokusudiwa ya kupunguza uhalifu hapa nchini.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...