Na Karama Kenyunko,  blogu ya jamii
MWALIMU Mkuu wa  shule  ya  msingi ya Kimataifa  ya Hazina iliyopo Magomeni jijini Dar Es salaam na walimu  wake wanne leo  Septemba  26.2018  wamepandishwa katika kizimba cha Mahakama ya  Hakimu  Mkazi  Kisutu  kujibu  tuhuma za kupata  mitihani ya Taifa ya darasa la saba na kufanya mawasiliano ya maudhui yake na watahiniwa wa shule hiyo isivyo halali. 

Mwalimu Mkuu huyo Patrick Cheche (43) Wa shule hiyo ambayo mara kwa mara imekuwa ikitangazwa kufanya vizuri katika mitihani ya Taifa ya darasa la nne na la saba na walimu wenzake wamesomewa mashtaka yao leo mbele  ya  Hakimu  Mkazi  Mfawidhi Huruma  Shahidi.

Mbali na Cheche (43), anayeishi Mpinga Bagamoyo, washtakiwa wengine ni Laurence Ochien (30), Justus James (32), Nasri Mohamed (32) na Mambo Idd (32), ambao wote wakazi wa Dar es Salaam.

Akisoma hati  ya  mashtaka Wakili wa Serikali Mwandamizi  Mutalemwa Kishenyi  akisaidiana na Wakili wa Serikali, Mwanaamina Kombakono amedai washitakiwa hao Septemba 4, mwaka huu, katika Jiji na Mkoa wa  Dar es Salaam kwa pamoja walikula njama  ya kutenda kosa la kuingilia mitihani ya Taifa ya darasa la saba isivyo halali.

Washtakiwa katika Shtaka hilo la  kula njama wanashtakiwa chini ya Sheria ya Kanuni za adhabu.

Katika shtaka la pili ambao washtakiwa hao wanashitakiwa chini ya Sheria ya Baraza la Mitihani la Taifa, wanadaiwa Septemba 5 mwaka huu katika shule hiyo ya Hazina, iliyoko Magomeni, kujibu, kinyume cha sheria walipata uwezo wa kupata mitihani wa taifa wa darasa la saba na kuonesha maudhui yake kwa watahiniwa waliosajiliwa Katina shule hiyo.

Pia imedaiwa Katika shtaka la tatu, Septemba 5 mwaka huu katika shule hiyo washtakiwa hao kwa makusudi walitoa mitihani kwa watahiniwa waliosajiliwa katika shule hiyo wakati hawakustahili kufanya hivyo.Hata hivyo washtakiwa wote wamekana kutenda kosa hilo  na wako  nje kwa dhamana.

 Kwa Mujibu wa  upande wa mashtaka upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.Akisoma masharti ya dhamana,  Hakimu Shaidi amesema ili washtakiwa wawe nje kwa dhamana, kila mmoja anatakiwa awe na wadhamini wawili wenye barua za utambulisho, vitambulisho na mmoja kati ya wadhamini hao awe anatambulika katika taasisi yoyote.

Pia kila mdhamini anatakiwa kusaini bondi ya Sh.milioni sita na mshtakiwa wa kwanza na wa pili watatakiwa kuwasilisha hati zao za kusafiria kwani wao ni raia wa Kenya.Hata hivyo washtakiwa hao walifanikiwa kukamilisha masharti hayo ya dhamana kasoro mshtakiwa wa pili  ambaye alipelekwa rumande baada ya kushindwa kukamilisha masharti hayo ya dhamana.

Kesi imeahirishwa hadi Oktoba 10, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama laa.

 Mwalimu Mkuu wa  Shule  ya  Msingi ya Kimataifa  ya Hazina iliyopo Magomeni jijini Dar es Salaam na walimu  wake wanne wakipandishwa katika kizimba cha Mahakama ya  Hakimu  Mkazi  Kisutu mapema leo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...