Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH),kuanzia Novemba 12 hadi 16, 2018 inatarajia kufanya upasuaji wa kupandikiza vifaa vya usikivu kwa watoto 10 ambao wana matatizo ya kusikia baada ya kukamilika kwa maandalizi ya mwisho. 

Watoto hao watapandikizwa vifaa vya usikivu baada ya wataalam kuwafanyia uchunguzi wa kina pamoja na wazazi kupatiwa ushauri wa kitaalamu. Baada ya watoto hao 10 kupandikizwa vifaa vya usikivu, jumla ya watoto watakaokuwa wamepandikizwa vifaa hivyo itafikia 21 tangu kuanza kwa upasuaji huu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH). 

Daktari Bingwa wa upasuaji wa Masikio, Pua na Koo wa hospitali hiyo Dkt. Edwin Liyombo amesema maandalizi kwa ajili ya kupandikiza vifaa vya usikivu kwa watoto hao yamekamilika. Dkt. Liyombo amesema kwamba leo wamefanya kikao cha pamoja na wazazi wa watoto hao kwa ajili ya kuwaandaa na kuwapatia maelekezo jinsi ya kuwa karibu zaidi na watoto hao ili waweze kusikia vizuri na kuzungumza baada ya kupandikizwa vifaa vya usikivu. 

“Wazazi wanatakiwa kuwafutilia kwa karibu watoto baada ya kupandikizwa vifaa vya usikivu. Zinahitajika nguvu za ziada ili watoto waweze kuzungumza vizuri na kusikia,” amesema Dkt. Liyombo. Katika mkutano huo wazazi wa watoto hao wameonyesha imani kunbwa kwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa za kuhakikisha Watanzania wanapatiwa huduma bora za kibingwa. 

Upandikizaji wa vifaa hivyo utafanywa na timu ya wataalam 10 wa Muhimbili na wataalam wawili kutoka Misri akiwamo Prof. Lobna El Fiky, Mohamed El Disouky.
Mmoja wa wazazi akiwa kwenye kikao leo cha mwisho katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) cha maandalizi ya kupandikiza vifaa vya usikivu kwa watoto 10 wenye matatizo ya kusikia. 
Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Masikio, Pua na Koo kutoka nchini Misri, Prof. Lobna El Fiky akijadili jambo kwenye kikao cha maandalizi ya kupandikiza vifaa vya usikivu kwa watoto wenye matatizo ya kusikia. 
Kulia ni Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Masikio, Pua na Koo wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Shaban Mawalla akitoa taarifa ya mmoja wa watoto wenye tatizo la usikivu kwenye kikao hicho. Katikati ni Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Masikio, Pua na Mkoo wa Muhimbili, Dkt. Edwin Liyombo, mtaalam wa usikivu, Fayaz Jaffer na kushoto ni wazazi wakiwa kwenye kikao hicho leo. 
Wataalam wakiwa katika picha ya pamoja na wazazi wa watoto ambao watafanyiwa upasuaji wa kupandikizwa vifaa vya usikivu kuanzia Novemba 12 hadi 16, 2018 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...