ZAIDI ya Sh milioni 302.6 zimekusanywa katika kilele cha mashindano ya baiskeli ya ACACIA Imara Pamoja Cycle Challenge, ambayo lengo kuu ni kuchangisha fedha kutekeleza miradi itakayoboresha upatikanaji wa elimu kwa jamii zinazozunguka migodi kampuni Acacia kanda ya ziwa.
Mashindano hayo yaliyoandaliwa na Kampuni ya Uchimbaji Madini –ACACIA kwa kushirikiana na Taasisi binafsi kutoka nchini Canada (CanEducate), yameshirikisha wanaume katika mbio za Kilomita 140 na wanawake km 87.
Mzunguko wa mashindano hayo yaliyofanyika leo jijini Mwanza ulianza na kumalizikia katika Hoteli ya Malaika Resort kwa kupitia maeneo ya Kibandani, Igombe, Sangabuye, Kayenze, Nyanguge na Usagara, Buhongwa.
Akizungumza katika kilele cha mashindano hayo, Meneja Uboreshaji tija wa kampuni hiyo, Janet Reuben alisema jumla ya washiriki 211 wameshiriki katika mbio hizo. Alisema kila mwaka ACACIA imekua ikidhamini mashindano ya baiskeli ya kanda ya ziwa chini ya jina la Acacia Tufanikiwe Pamoja Cycle Challenge.
“Hata hivyo, mwaka huu mashindano hayo yamepewa jina Acacia Imara Pamoja Cycle Challenge ili kuakisi dira mpya ya kampuni inayolenga kujenga mahusiano imara zaidi na jamii na wadau wetu. “Pia uamuzi huu wa kubadili jina unatokana na kuongezeka kwa kipengele cha uchangishaji fedha katika mashindano ya mwaka huu kwa ajili ya kusaidia sekta ya elimu.
“Kwa niaba ya uongozi wa Acacia kwa kupitia migodi yetu ya dhahabu ya Bulyanhulu, Buzwagi na North Mara, wadau wetu CanEducate na kamati ya maandalizi, nipende kuwashukuru kwa uwepo wenu leo, pia nawapongeza washindi na washiriki wote kwa kumaliza mbio hizi salama,” alisema.
Meneja Uboreshaji Tija kutoka ACACIA, Janet
Reuben akizungumza katika mashindano mbio za baiskeli yaliyopewa jina la Acacia
Imara Pamoja Cycle Challenge. Jumla ya Sh milioni 302.6 zimekusanywa katika
mashindano hayo yaliyofanyika leo jijini Mwanza.
Baadhi ya washiriki wa mashindano mbio za baiskeli
yaliyopewa jina Acacia Imara Pamoja Cycle Challenge wakiwakata upepo katika
mashindano hayo yaliyofanyika jijini Mwanza. Jumla ya washiriki 211 wametimua
mbio katika mashindano hayo.
Mshindi wa mashindano ya mbio za baiskeli yaliyopewa jina Acacia Imara Pamoja Cycle Challenge, Masunga Duba akishangilia kuibuka mshindi na kujinyakulia Sh milioni 1.2, wa pili Gerald Konda (sh 900,000) na watatu Mungu Ataleta (Sh 500,000).
Baadhi ya washiriki wa mashindano wakikata utepe
kuanza mashindano hayo yaliyofanyika leo jijini Mwanza. Jumla ya washiriki 211
wametimua mbio katika mashindano hayo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...