MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF)mkoa wa Ruvuma,umekutana na wanachama na viongozi wa vyama viwili vya msingi vya ushirika vinavyojihusisha na kilimo cha zao la korosho katika wilaya ya Tunduru.
Lengo ni kuhamasisha wanachama na viongozi wa vyama hivyo kujiunga na mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa ajili ya kupata huduma za matibabu pindi wanapoumwa kwa kuwa shughuli za kilimo zinahitaji mtu mwenye afya njema ambayo itamruhusu kuendelea na majukumu yake katika kipindi cha msimu wa kilimo.
Wanachama hao ni kutoka vyama vya Naluwale na Mumsasichema kata ya Muhwesi ambayo ni maarufu kwa uzalishaji mkubwa wa korosho wilayani hapa.Akizungumza na Wanachama hao kaimu Meneja wa mfuko huo Antony Mgima alisema, mpango huo unalenga kutoa huduma kwa mwanachi mmoja kwa gharama ya shilingi 78,600 ambapo mwanachama atapata fursa ya kuhudumiwa kuanzia ngazi ya zahanati,kituo cha Afya na Hospitali zote Nchini.
Alisema, mpango huu wa sasa utasaidia sana kila mmoja kunufaika nao tofauti na hapo awali ambapo ni watumishi wa umma pekee yao ambayo walikuwa na sifa ya kuwepo katika mpango wa huduma za matibabu.
Kwa mujibu wake, mwanachama wa NHIF ana hiari ya kumlipia fedha kama michango kwa mtu yoyote ambaye anaona anastahili kuwemo katika mpango hasa ikizingatia kuwa, kwa sasa mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya umeboresha sana huduma zake .
Mkuu wa wilaya ya Tunduru Juma Homera,ameitaka NHIF kuhakikisha wanawashirikisha viongozi wa vijiji na kata katika kuhamasisha wananchi wengi zaidi ili nao waweze kujiunga na mfuko huo badala ya kulenga wanachama na viongozi wa vyama vya ushirika.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...