Na Karama Kenyunko, Blogu ya Jamii

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imesema uamuzi wa Mahakama ya rufaa dhidi dhamana ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko utatolewa na Mahakama ya Rufaa.

Hakimu Mkazi Mfawidhi, Kelvin Mhina amesema hayo leo Februari 14, 2019 wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa mahakamani hapo ambapo amesema mpaka sasa kesi hiyo haijaaanza kusikilizwa, mpaka watakapopata majalada ya maamuzi kutoka Mahakama ya Rufaa.

Mapema,  Wakili wa Serikali, Ester Martin amedai kesi hiyo leo imekuja kwa ajili ya kutajwa na kwamba wanasubiri uamuzi wa Mahakama ya Rufaa. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 28, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa wakati wakisubiri Rufaa  yao Ambayo tasikilizwa Februari 18, mwaka huu.Novemba 23, mwaka jana,Jaji Mashauri akiwa Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, alifuta dhamana kwa Mbowe na Matiko kutokana na kukiuka  masharti ya dhamana.

Baada ya uamuzi huo , washitakiwa hao wakiwakilishwa na Wakili Peter Kibatala walikata rufaa Mahakama Kuu kupinga maamuzi ya mahakama hiyo ya kufuta dhamana.Hata hivyo, baada ya mahakama Kuu chini ya Jaji Sam Rumanyika kusikiliza mapingamizi ya pande zote iliamua kuanza usikilizaji wa rufaa hiyo.

Upande wa Serikali ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi alidai kuwa wamekata rufaa katika Mahakama ya Rufani kupinga maamuzi yaliyotolewa na kuiomba mahakama hiyo kuacha kuendelea kusikiliza rufaa hiyo kwa sababu haina mamlaka.

Hata hivyo, baada ya upande wa serikali kuwasilisha rufaa yao,  kuliibuka malumbano ya kisheria baina ya mawakili wa pande zote, huku mawakili wa kina Mbowe wakiongozwa na Wakili Peter Kibatala, walipinga uhalali wa taarifa ya serikali ya kusudio la kukata rufaa kwa madai hawajafahamishwa na Msajili wa Mahakama Kuu kuhusu kuwepo kwa taarifa hiyo.

Jaji Rumanyika alisema kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP) anapewa mamlaka ya kukata rufaa kwa uamuzi mdogo chini ya kifungu cha 6 cha Sheria ya Mamlaka ya Rufaa na kwamba kunapokuwepo taarifa ya kusudio la kukata rufaa Mahakama ya Rufani, mahakama ya chini haiwezi kuendelea na shauri.

Jaji  Rumanyika alisema mahakama yake imefungwa mikono hivyo anasitisha usikilizwaji wa rufani hiyo hadi hapo itakapotolewa uamuzi katika Mahakama ya Rufani.Mbali na Mbowe na Matiko, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mbunge wa Iringa mjini, Peter Msigwa, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Katibu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji, Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu ambao wote walikuwepo mahakamani.

Katika kesi ya msingi, washitakiwa wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari Mosi na 16, mwaka  2018 maeneo ya Dar es Salaam.



Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko wakitoka kwenye viunga vya mahakama leo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...