Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, (DPP) Biswalo Mganga ameziasa benki zote nchini, zilizotumika kuweka sh. Bilioni 14 za kampuni ya kusimamia shughuli za upatu (DECI), kwa mtindo wa kupanda mbegu na kuvuna fedha kutozigusa fedha zozote zilizoamriwa kutaifishwa na mahakama na wakibainika kufanya hivyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yao ikiwemo kupelekwa mahakamani

DPP amesema hayo leo Mei 8, 2019 alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari ofisini kwake kufuatia amri ya Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam iliyotolewa jana na kuamuru mali zote za Deci zitaifishwe na kuwa mali ya serikali.

Amesema, mameneja wa benki hizo wanapaswa kuwa makini na kutambua kuwa mahakama tayari imeshatoa agizo na wasiruhusu kurubuniwa kuzihamisha kwenda kwenye akaunti nyingine.

Akieleza sababu za kutoa onyo hilo, Dpp amesema, Januari 10, mwaka huu kulikuwa na kesi inayowahusu wakurugenzi wa Kampuni ya Rifaro Afrika ambayo inajihusisha na kuchezesha upatu ambao walikiri makosa na mahakama iliwaamuru fedha zilizokuwa benki ya biashara ya Kenya (KCB) sh milioni 149 zitaifishwe na kuwa mali ya serikali.

Amesema, hatua hiyo ilikuja baada ya mahakama kuwaachiwa kwa kulipa faini ya zaidi ya Sh milioni 204, ambapo baada ya kulipa faini hiyo, fedha zilizokuwemo kwenye account KCB, benki walihamisha Sh milioni 109 na kuziweka kwenye akaunti maalum na kuacha Sh milioni 40 pekee.

Amesema kufuatia kitendo hicho, ameshatoa maagizo kwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) kufanya uchunguzi kwa meneja wa benki hiyo ya KCB na wahakikishe kwamba fedha hizo zinarudi mapema iwezekanavyo na waende mahakamani akaeleze kwa nini fedha hizo walieza kuziamisha kutoka kwenye akaunti husika huku wakijua zilikuwa zimezuiwa kwa amri ya mahakama kwa kutaifishwa.

Aimezitaja mali zilizotokana na DECI ambazo ni nyumba nne, viwanja vitano na magari 11 na fedha hizo zilizoko kwenye akaunti za Benki ya NMB, DCB na KCB, ambazo Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam iliamuru mali hizo zitaifishwe na kuwa za serikali.

Aidha DPP amewaasa wananchi wanaojishughulisha na upatu kuacha mara moja kwa sababu ni kosa la jinai na kwamba watakapokamatwa watashitakiwa na watapoteza mali na fedha zao kwa sababu zitataifishwa.

"Ninafahamu kuna watu ambao bado wanajishughulisha na upatu, niwaombe waache, tulianza na Deci 2009, ikaja Rifaro ambayo tayari fedha zao zimetaifishwa na zote huko wataendelea kupoteza fedha, ninafahamu kuna watu walijiingiza kwenye upatu katika kampuni nyingine tuko kwenye upelelezi muda ukifika tutasema, lakini yeyote anayejiingiza kwenye upatu kwa kutafuta fedha za haraka haraka atapoteza fedha sake"amesema Mganga.

Amesema watu watafute biashara halali ya kufanya uwekezaji kuliko kujiingiza kwenye upatu. Kwani sheria inasema yeyote anayejiingiza kwenye upatu anafanya kosa la jinai na akikamatwa atashtakiwa.

Mganga alizitaja mali ambazo zimetaifishwa kuwa ni nyumba namba UKMMD/1237 iliyoko Mwembe Madafu, Ukonga, Dar es Salaam, kiwanja namba 651, kitalu ‘M’ kilichopo Forest area, Mbeya, nyumba iliyoko kiwanja namba 7, kitalu ‘P’ ikiwa na hati namba 033004/23 kilichopo mtaa wa Rufiji, Manispaa ya Mwanza.

Pia mali nyingine ni kiwanja namba 2/283/2 kitalu “E” Mabibo, Kinondoni, Dar es Salaam, kipande cha ardhi ambacho hakijapimwa kilichopo kijiji cha Manyinga, Turiani, Mvomero, Morogoro, kiwanja namba 467 kilichopo kitalu “H” kikiwa na hati ya usajil;i namba 48170 kilichopo eneo la Tegeta, Dar es Salaam, nyumba iliyoko kiwanja namba MM/19/P kilichopo Manzese karibu na barabara ya Morogoro, Dar es Salaam na nyumba iliyoko katika kiwanja namba KND/MXS/MNM/Z ikiwa na leseni ya makazi namba KND 008337 Kinondoni, Dar es Salaam.

Magari yaliyotaifishwa ni Toyota Premio lenye namba T 132 AWJ, Toyota Land Cruiser namba T 480 AUP, Toyota Rav 4 namba T 274 ATQ, Toyota Mark II namba T 676 AYP, Subaru Legacy namba T 682 AUT, Toyota Ipsum namba T 850 AXY, Toyota Ipsum T455 ADM, Toyota Mark II T 186 AYX, Mitsubishi Pajero T 852 AAV, Toyota Land Cruiser T 789 AUX, Nissan Terrano namba T 899 AYU.

Aidha, Mganga alisema fedha zilizotaifishwa na kuwa mali za serikali ni Sh 12,503,068,647.89 zilizopo NMB, tawi la Msasani, Sh 1,457,700,462.49 zilizoko benki ya Dar es Salaam Community Bank (DCB), tawi la Uhuru na Sh 57,933,304.10 zilizoko KCB, tawi la Samora, Dar es Salaam.

Alisisitiza kuwa mahakama hiyo iliamuru magari hayo yabadilishwe umiliki na kubadilishwa matumizi kwa namna serikali itakavyopenda na kiwanja ambacho hakijapimwa kinatakiwa kusajiliwa kwa jina la Katibu Mkuu hazina.

Pia mahakama iliagiza DPP kupeleka maombi mahakamani hapo kuomba watu wanaoishi kwenye nyumba hizo watolewe kupitia kampuni ya udalali.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...