Muonekano wa eneo lililobuniwa na
TAWA kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya KARIBU KILIFAIR 2019
jijini Arusha linaloakisi Pori la Akiba la Selous.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu akizungumzia mikakati ambayo Serikali imeipanga ya namna ya kushirikiana na Wadau wa sekta ya utalii mara baada ya kufungua Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya KARIBU KILIFAIR 2019 jijini Arusha.(Picha na Wizara ya Maliasili na Utalii)

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu (katikati)wakiwa na waandaaji wa maonesho hayo ya Kimataifa ya Utalii ya KARIBU KILIFAIR 2019, Bw.Dominick Shoo (kulia) akiwa Mwenyekiti wa Kampuni ya Kilifair Promotion, Tom Kunkler (kushoto). na kwenye mfano wa kilele cha Mlima Kilimanjaro mara baada ya kufungua Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya KARIBU KILIFAIR 2019 jijini Arusha.(Picha na Wizara ya Maliasili na Utalii)

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu wakati akizungumza kwenye ufunguzi wa Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya KARIBU KILIFAIR 2019 jijini Arusha.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na waaandaji na waalikwa walioshiriki kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya KARIBU KILIFAIR 2019

Naibu Waziri wa Maliasili na
Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja
na Watumishi wa Benki ya NMB ambao ni wadhamini wakubwa wa kwa mwaka
huu kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya KARIBU KILIFAIR 2019

Naibu Waziri wa Maliasili na
Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu (wa pili kushoto) akiwa kwenye picha ya
pamoja na baadhi ya washiriki kwenye nembo ya Maonesho ya Kimataifa ya
Utalii ya KARIBU KILIFAIR 2019

Naibu Waziri wa Maliasili na
Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu akiwa pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya
Utalii Tanzania (TTB), Jaji Mstaafu Thomas Mihayo wakipewa maelezo na
Wily hida kuhusu uimara wa gari maalum ya kubeba watalii jinis
inavyoweza kuhimili hali zote pindi ikiwa mbugani na watalii mara baadfa
ya kufungua Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya KARIBU KILIFAIR 2019
jijini Arusha. (Picha na Wizara ya Maliasili na Utalii)
*********************************
WMU – ARUSHA
Serikali imesema kuwa itaendelea
kushirikiana na wadau wa sekta binafsi waliowekeza katika Sekta ya
Utalii na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazowakabili kwa lengo la
kuimarisha sekta hiyo na kuvutia wawekezaji wengi zaidi.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu wakati
akifungua Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya KARIBU KILIFAIR 2019 jijini
Arusha.
Amesema ushirikiano huo unalenga
kuifanya sekta ya utalii iwe zao namba moja na chanzo kikuu cha mapato
nchini na kuongeza kuwa Tanzania inaendelea kuwekeza kwenye miundombinu
ya barabara na viwanja vya ndege kwa lengo la kufungua shughuli za
utalii katika maeneo yote yenye vivutio vya utalii.
Mhe.Kanyasu amesema kufanyika kwa
maonesho hayo ambayo ni makubwa mara mbili ya yale yaliyofanyika mwaka
jana ni ishara ya kukua kwa sekta ya utalii na kueleza kuwa washiriki
kutoka nchi 40 za ndani na nje Afrika na mashariki ya nje yameshiriki.
“Maonesho haya yana sura ya
Kimataifa hili linatambulika kwa kuona washiriki hao sisi kama nchi
tumepata bahati, tungeweza kutumia gharama kubwa kuwaleta hawa watoa
huduma za utalii huko kwenye nchi zao, hawa wamekuja wenyewe na hii
imesaidia kampuni za Tanzania badala ya kwenda nje kuuza biashara zao
wamekutana na kampuni za kimataifa hapa hapa Tanzania” Amesema Mhe.
Kanyasu.
Amesema onesho la KARIBU KILIFAIR
linasaidia kukuza utalii nchini kutokana na umuhimu wake wa kuuza
huduma na bidhaa za utalii kwa kutangaza fursa mbalimbali zilizopo hapa
nchini na kuongeza kuwa ili utalii uweze kukua ni lazima kazi ya
kutambulisha na kuuza bidhaa za utalii ifanyike.
Mhe. Kanyasu amezitaka taasisi za
uhifadhi zilizo chini ya Wizara ambazo zinashiriki maonesho hayo
zikiwemo TANAPA, Ngorongoro, TAWA, Bodi ya Utalii Tanzania na Wakala wa
Misitu Tanzania (TFS) zifikiri kibiashara na kutafuta wawekezaji wapya
watakaowekeza na kufanya biashara kwenye Mapori ya Akiba, Misitu ya
Asili na hifadhi za Taifa ambazo bado hazijapata wawekezaji ili nazo
zichangie katika pato la Taifa.
“Tunataka taasisi zote wakati
zinashiriki uhifadhi zifikiri kibiashara, tunataka tuondokane na mfumo
wa kizamani wa kufikiri kuhifadhi bila kufikiri kibiashara, tuna mapori
mengi ambayo ambayo hayaingizi fedha, tunataka taasisi za usimamizi wa
mapori haya watafute wawekezaji kwa kuainisha fursa za uwekezaji
zilizopo” Amesisitiza Mhe. Kanyasu.
Amesema kuwa Serikali
inaendelea kuboresha miundombinu ya ukanda wa kusini ikiwemo barabara,
ununuzi wa ndege kubwa za kisasa na kuboresha viwanja vya ndege ili
kufungua Utalii wa ukanda wa Kusini na kuongeza shughuli za utalii
katika hifadhi za ukanda huo zikiwemo Ruaha Selous, Mikumi na
Udzungwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Jaji Mstaafu Thomas Mihayo akizungumzia
maonesho hayo amesema kuwa mwaka huu Tanzania imepata wageni wengi
walioshiriki maonesho hayo kutoka ndani na nje ya Afrika.
Amesema ujio wa washiriki hao
utasaidia kwa kiwango kikubwa kuitangaza Tanzania kimataifa na kusaidia
kukuza na kuongeza idadi ya watalii wanaoitembelea Tanzania.
Kwa upande wake Mjumbe wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii ambaye na Mbuge
wa Iringa mjini, Mhe. Peter Msigwa ameeleza kuwa ushiriki wa makampuni
mengi ya utalii ya ndani na nje ya Tanzania unaeleta chachu katika dhana
nzima ya kukuza utalii nchini.
“Hili ni jambo jema na lenye
heri ambalo kwa kufanya maonesho haya yanasababisha tujulikane, biashara
ni matangazo tunapokuwa tunajulikana ndani ya nchi na kimataifa
inasaidia sana kukuza utalii” Amesema Mhe. Msigwa.
Mhe. Msigwa amesema
ushirikiano wa sekta binafsi na Serikali ni muhimu katika kukuza utalii
nchini akibainisha kuwa hilo litaiwezesha serikali kuendelea kukusanya
kodi kutoka sekta binafsi kwa lengo la kuendesha nchi.
Naye Mkurugenzi wa kampuni ya
KILIFAIR ambao ni waandaaji wa maonesho hayo ya Kimataifa ya Utalii ya
KARIBU KILIFAIR 2019, Bw.Dominick Shoo ameeleza kuwa maonesho hayo kwa
mwaka huu yamewahusisha washiriki zaidi ya 450 kutoka ndani na nje ya
Tanzania.
Bw. Shoo ameishukuru Serikali
kwa ushirikiano inaoutoa kwa sekta binafsi na kazi kubwa kazi kubwa
inayoendelea kufanyika ya kufungua vituo vipya vya utalii katika mikoa
ya Kanda ya ziwa na kueleza kuwa wao kama wadau wa sekta binafsi
wataendelea kuvitangaza vivutio hivyo kwa nguvu kubwa.
“ Ninaishukuru Serikali kwa
kuweka msukumo mkubwa katika uanzishaji wa vituo vipya vya utalii na
kazi kubwa inayoendelea ya kuboresha miundombinu, ninaamini utalii wa
Tanzania utakua kwa kasi na hii inaashiria kwamba ushirikiano tunaoupata
kutoka Serikalini utalii utakua kwa kasi kubwa na tutapata watalii
wengi zaidi” Amesisitiza Bw. Dominick.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...