Na Karama Kenyunko, Michuzi Tv

MAHAKAMA Kuu Kitengo cha Makosa ya Rushwa na Uhujumu uchumi maarufu kama Mahakama ya Mafisadi imepokea barua mbili za uthibitisho kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, kwamba washitakiwa Benason Shallanda na Alfred Misana waliteuliwa kuwa makamishna katika Idara ya Sera.

Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu kutoka Wizara hiyo, Grace Sheshunga (52), amezitoa barua hizo leo Julai 11,2019 mahakamani hapo mbele ya Jaji Immaculata Banza wakati akitoa ushahidi wake dhidi ya kesi ya utakatishaji inayomkabili Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake.

Mbali na hao, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Ofisa wa Benki ya Stanbic, Shose Sinare na Sio Salomon ambao kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 58 yakiwemo 49 ya utakatishaji fedha.

Akiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Hashimu Ngole, kutoa ushahidi wake shahidi Sheshunga amedai Oktoba Mosi, 2010 Shallanda aliteuliwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi wakati huo, Ramadhan Kija kuwa Kamishna wa Sera na kudai kuwa, barua ya kupandishwa cheo kwa Shallanda ilielekeza kwamba atalipwa Sh 2,062,000 bila nyongeza na kwamba atakuwa kwenye majaribio kwa miezi sita na endapo atashindwa kazi hiyo atatolewa.

Amedai kuwa, barua hiyo pia ilielekeza kwamba serikali itamdhamini mshitakiwa huyo kwa kumkopesha gari ndogo ya usafiri aina ya Sallon kwa ajili ya safari za kwenda kazini na kurudi nyumbani, nyumba ya kuishi na kumlipia gharama za umeme ya fedha isiyozidi Sh 205,000 na simu Sh 180,000 kwa mwezi huku majukumu yake kwa nafasi hiyo yakiwemo ya kuandaa sera za madeni na kupokea maombi mbalimbali ya mikopo ya fedha.

Aidha amedai, Agosti Mosi, 2013 mshitakiwa Misana ambaye alikuwa Mchumi Mkuu daraja II, aliteuliwa kuwa Kamishna Msaidizi wa Madeni katika Idara ya Sera huku akiongeza kuwa mamlaka iliyomteua mshitakiwa Misana ni aliyekuwa Katibu Mkuu, Dk Servacius 

Likwelile ambaye alielekeza kwamba mshahara ulioainishwa katika barua hiyo ni Sh 2,900,000.

Pia alielekeza mshitakiwa atafanya kazi kwa majaribio kwa miezi sita na endapo atashindwa kumudu majukumu hayo makubwa yanayohusu madeni ataondolewa kwenye nafasi hiyo kwa mujibu wa sheria. Na barua yake ya kupandishwa cheo ilielekeza kuwa serikali itamdhamini mshitakiwa huyo kukopa gari, kumpatia nyumba, kumlipia umeme usiozidi Sh 205,000 na simu Sh 180,000.

Baada ya kueleza hayo, shahidi aliiomba mahakama kupokea barua hizo kama kielelezo na upande wa utetezi haukuwa na pingamizi.

Shahidi huyo amedai majukumu yake ni kutunza nyaraka mbalimbali za mawasiliano ya ndani na nje ya wizara kwenye masijala zao na kwamba Januari Mosi, 2016 alipokea hati kutoka Takukuru ikimuelekeza kuwasilisha nyaraka zinazohusu muhtasari wa kikao cha 61 cha Kamati ya Kitaalamu ya Usimamizi wa Madeni (TDMC) na kuiwasilisha.

Hata hivyo, baada ya shahidi huyo kuomba mahakama kupokea nyaraka hiyo, Wakili wa Utetezi, Majura Magafu alipinga kupokelewa kwa sababu nyaraka hiyo haijaambatana na muhtasari wa kikao kama shahidi alivyoelekeza huku Wakili Alex Mgongolwa na Jeremiah Ntobesya walipinga pia kwa madai kuwa barua iliyowasilishwa ni ya siri kinyume na Sheria ya Usalama wa taifa pia inaonekana hakuna nyaraka iliyopelekwa Takukuru kwa sababu katika vielelezo hivyo havioneshwi.

Wakili Ngole, amedai hoja zilizowasilishwa hazina mashiko nakuomba mahakama kuzitupilia mbali kwani upande wa utetezi hawapaswi kuwapangia namna ya kuwasilisha ushahidi wao kwani nyaraka zilizowasilishwa zina maana kwenye shauri hilo na zinaonesha namna shahidi alivyohusika kutoa nyaraka aliyoombwa.

Kesi hiyo itaendelea kesho.

Washitakiwa katika kesi hiyo wanakabiliwa na mashitaka matatu ya kughushi, moja la kuongoza uhalifu, 49 ya utakatishaji fedha, mawili ya kutoa nyaraka za uongo, kujipatia fedha kwa njia ya udanyanyifu moja na la kutoa nyaraka kwa nia ya kumdanganya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...