Moureen Rogath, Kigoma
Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso, amemuagiza Naibu katibu Mkuu wa wizara ya maji mhandisi Emmanuel Kalobelo, kuwasimamisha kazi wahandisi wawili wa Wakala wa Maji na usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).
Akizungumza leo katika mkutano wa saba wa Mwaka wa bodi za maji za mabonde, uliofanyika mjini hapa mkoani Kigoma, wahandisi hao ni Elinathan Elisha wa wilaya ya Kakonko na Godfrey Mbuza wilaya ya Kasulu.
Amesema wahandisi hao wamekuwa sababu ya kukwamisha miradi ya maji katika wilaya hiyo hali iliyosababisha wananchi kushindwa kupata huduma za maji katika maeneo yao.
"Serikali imekuwa ikitumia gharama kubwa katika miradi mbalimbali ya maji nchini lakini wapo baadhi ambao wamekuwa wakikwamisha jitihada hizo hali na kuwaumiza wananchi," amesema Aweso.
Aweso amesema zaidi ya kampuni 30 zilizojenga miradi ya maji chini ya kiwango nchini zitabainishwa na hawatapewa miradi yoyote ya maji ili iwe fundisho kwa kampuni nyingine zinazojenga miradi chini ya kiwango.
Amewataka ofisi za mabonde kuhakikisha inakomesha vitendo vya uchafuzi wa rasilimali na vyanzo vya maji katika mabonde na hasa kudhibiti viwanda vinavyotiririsha uchafu kwenye vyanzo vya maji.Naibu katibu mkuu wa wizara ya maji, Mhandisi Emanuel Kalobelo alisema usimamizi wa rasilimali za maji bado ni changamoto kubwa katika wizara hiyo.
Mkuu wa mkoa wa Kigoma Brigedia Generali mstaafu Emanuel Maganga amewataka wavuvi wanaovua ziwa Tanganyika kuacha kutumia sumu kupata samaki kwani ni hatari kwa watumaji wa maji.
Ameagiza ofisi za bonde kutoa elimu kwa wananchi juu ya utaratibu wa kuchimba visima na mabwawa kwa kufuata utaratibu ikiwa ni pamoja na kupata vibali kutoka ofisi za bonde katika eneo wanapoishi.
Mkutano huo wa siku mbili utajadili masuala ya rasilimali za maji na kutoa maazimio yatakayosaidia kuboresha miundombinu na rasilimali za maji ili kuwa endelevu.

Wadau wa maji wakiwa katika mkutano wa saba wa mwaka wa bodi za mabonde ,uliofanyika mjini Kigoma leo .
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...