Na EmanuelMadafa,MichuziMbeya .
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi mkoa wa Mbeya imewahukumu kwenda jela miaka mitatu raia watatu wa kigeni ama kulipa faini ya shilingi milioni kumi kila mmoja baada ya kukiri kukutwa na madini ya dhahabu gramu 1043 sawa na kilo 1.33 kinyume cha sheria ya madini No. 14 ya mwaka 2010.
Julai mwaka huu watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani hapo wakikabiliwa na shitaka moja la uhjumu uchumi ambalo ni kumiliki na kusafirisha Madini yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 98.5.
Washitakiwa hao ambao ni Clive Rooney (62) raia wa Ireland, na wenzake wawili Ross Stephen Harris 34 na Robert Charles Wheedon (59) raia wa Uingeza wamekutwa na madini hayo katika Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Songwe mkoani Mbeya julai 3 mwaka huu.
Hukumu hiyo imetolewa na Kaimu Hakimu Mfawidhi Venance Mulingi baada ya washtakiwa kukiri mashitaka yanayowakabili.Na kisha Mahakama hiyo ikaamuru madini hayo yataifishwe na yakabidhiwe Benki kuu ya Tanzania (BoT) hadi serikali itakavyoamua vinginevyo.
Mapema mwendesha mashtaka wa serikali Jacqueline Nyantori ameieleza mahakama kuwa washtakiwa walimwandikia barua Mkurugenzi wa Mashtaka nchini DPP wakiomba kupewa nafasi ya kukiri kosa.
Katika barua hiyo washtakiwa wamemwomba DPP kutoa kibali ili kesi yao ishuke kutoka mahakama kuu hadi mahakama ya wilaya na kueleza kuwa wako tayari kulipa faini ama kupewa adhabu yoyote ikiwemo kurejesha madini.Kabla ya hukumu kutolewa wakili wa upande wa utetezi James Kyando ameiomba Mahakama kuwapunguzia adhabu wateja wake kwa kuwa ni wageni na pengine wamefanya hivyo bila kujua kuwa ni makosa.
Hata hivyo upande wa Jamhuri ukiongozwa Jaqueline Nyntori umepinga vikali madai hayo na kueleza sababu kuu tatu za kuitaka mahakama itoe adhabu kali ili iwe funzo kwa wengine kutokna na serikali kuwa kwenye vita kali ya kiuchumi na kwamba walikuwa wnakwepa kulipa kodi.
Baada ya maelezo ya mawakili wa pande zote mbili Washitakiwa hao wamekiri kosa kukubali kulipa faini ya shilingi milioni 10 kila mmoja huku wakikwepa kwenda Jela kutumikia kifungo cha miaka mitatu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...