*Yasema kwa kuwa mtuhumiwa alitenda kosa Kisarawe  basi atafikishwa Mahakama ya Mkoa wa Pwani

*Yatoa onyo kwa wote wenye tabia ya kufanya vitendo vya kitapeli kwani TAKUKURU iko  macho, itawanasa


Na Humphrey Shao, Michuzi Tv Dar es Salaam

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ofisi ya Dar es Salaam inamshikilia mkazi wa Chamazi Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, kwa tuhuma za kujifanya Ofisa wa Serikali – kutoka ofisi ya Usalama wa Taifa na kutaka kumtapeli Mkuu wa Wilaya Kisarawe mkoani Pwani.

Hata hivyo TAKUKURU imesema kwa kuwa watuhumiwa huyo alitaka kufanya UTAPELI katika Wilaya ya Kisarawe basi atafikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Pwani ili sheria ichukue mondo wake.

Taarifa ya Kaimu Mkurugenzi wa TAKUKURU Ali Mfuru kwa vyombo vya habari aliyoitoa leo Julai 10,2019 amefafanua kuwa mtuhumiwa huyo anayejulikana kwa jina la Omari Khamis Chuma( 55), alikamatwa na maofisa wa TAKUKURU baada ya kupokea taarifa kuwa mtuhumiwa huyo alifika katika Ofisi zaMkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo kwa nia ya kumtapeli kwa kujifanya kuwa yeye ni Ofisa wa Serikali kutoka Usalama wa Taifa – IKULU.

Amesema baada ya kupokea taarifa hizo pamoja na taarifa kutoka katika vyanzo mbalimbali, TAKUKURU ilianzisha uchunguzi dhidi ya mtuhumiwa huyu na kuthibitisha makosa chini ya sheria zifuatazo ikiwemo Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007:

Amesema makosa hayo ni kujifanya Ofisa wa Serikali kinyume na kifungu Na 100 (b) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code) Sura ya 16 marejeo ya mwaka 2002 pamoja na kuomba, kushawishi au kujaribu kujipatia au kujipatia rushwa kinyume na Kifungu Na. 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na 11/2007

"Hatua ya kumkamata tapeli huyu imefikiwa takriban wiki tatu tu tangu TAKUKURU iutangazie umma kuhusu kukamatwa kwa matapeli wengine sita waliokuwa wakishirikiana kufanya utapeli. Kati ya watuhumiwa wale – Wanne kati yao walijifanya kuwa ni maofisa wa TAKUKURU pamoja na maofisa wa byombo vingine vya Dola na wawili kati yao walitoka katika kampuni ya Simu.

"Uchunguzi wetu umebaini kuwa matapeli hawa wana mtandao unaojumuisha watu kutoka maeneo na ofisi mbalimbali zikiwemo za Serikali na wamekuwa wakiwafuatilia watumishi au viongozi ambao kwa njia moja au nyingine wanaweza kuwa na tuhuma na hivyo kuwadai fedha rushwa  huku wakijifanya wao ni maofisa kutoka TAKUKURU au Usalama wa Taifa"amesema Mfuru.

Hata hivyo ametoa agizo kupitia vyombo vya habari kuwataka matapeli kuacha mchezo huo mara moja kwani TAKUKURU iko macho na inayo mamlaka kisheria ya kuwachukulia hatua wale wote wanaojihusisha na vitendo vya utapeli.

Kuhusu wapi mtuhumiwa aliyekata kumtapeli DC Mwegelo, amesema kuwa "Kwa kuwa mtuhumiwa huyu alitenda makosa haya katika Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, basi atafikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi - Mkoa wa Pwani leo Jumatano Julai 10, 2019 ili kujibu mashitaka yanayomkabili,"amesema.

Pia anaendelea kutoa tahadhari kwa jamii na kuwataka kuwa makini na kutokubali kurubuniwa kwa njia hizo wanazozitumia matapeli wa aina hiyo kujinufaisha na kuongeza anaendelea kuwahimiza wananchi kutupatia taarifa sahihi za matapeli wa aina hiyo au yeyote anayejihusisha na vitendo vya Rushwa ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa bila kumwonea mtu au kumpendelea yeyote.

"Taarifa hizi zinaweza kutumwa kwetu kupitia mfumo rasmi wa mawasiliano lakini pia wanaweza kuwatumia Viongozi wa Dini au chombo chochote cha Dola na taarifa hizo zitatufikia.Tunatoa shukrani kwa wananchi ambao wamekuwa ni msaada mkubwa katika kutupatia taarifa ikiwa ni pamoja na wadau mbalimbali tunaoshirikiana nao katika kueneza elimu dhidi ya rushwa kwa jamii yetu,"amesema.
 Kaimu Mkurugenzi wa Uchunguzi wa TAKUKURU, Ali.S.Mfuru Kulia akiwa na Mtuhumiwa anayejifanya usalama wa Taifa ndugu Omar Chuma mbele ya Waandishi wa Habari katika mkutano uliofanyika makao makuu ya Tasisi hiyo jijini Dar es Salaam 
 Kaimu Mkurugenzi wa uchunguzi TAKUKURU Ali.S.Mfuru akizungumza na Waandishi wa habari juu ya kumkamata tapeli aliyejifanya usalama wa Taifa

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...