Baadhi ya vifaa vyenye thamani ya
Tshs Milioni 70 vilivyotolewa kwa Taasisi ya Uvuvi nchini (TAFIRI) kwa
ajili ya kuendeleza tafiti za sekta ya uvuvi nchini

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na
Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah (mstari wa mbele katikati) akiwa
katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo.

Washiriki wa mafunzo wakiwa katika
hatua za mwisho za mafunzo kabla ya mafunzo hayo kuhitimishwa na Katibu
Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah.
****************
Na. Edward Kondela
Katibu Wizara ya Mifugo na Uvuvi
anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah amesema wizara hiyo kupitia
Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi nchini (TAFIRI) imeweka mikakati ya kufanya
tafiti ikiwa ni moja ya vipaumbele katika kukuza sekta ya uvuvi nchini
katika mwaka wa fedha 2019/2020.
Akizungumza jijini Dar es Salaam
wakati wa kufunga mafunzo hayo yaliyokuwa yakiendeshwa kwenye makao
makuu ya TAFIRI, Dkt. Tamatamah amesema mafunzo hayo yaliyofadhiliwa na
Serikali ya Watu wa China kupitia Sino-Africa Joint Research Centre
(SAJOREC) na East African Great Lakes Urban Ecology (EAGLU) kwa
kushirikiana na TAFIRI yana lenga kuhakikisha washiriki wa mafunzo hayo
ya siku sita ya uelewa wa ufuatiliaji wa ubora na unadhifu wa maji na
mazingira, wanafanya tafiti ili kuleta matokeo chanya katika ukanda wa
Bahari ya Hindi, maziwa na mito iliyopo nchini.
Dkt. Tamatamah amesema pia
washiriki wamepata mafunzo kupitia mihadhara iliyotolewa na wakufunzi
wabobezi kutoka China na Tanzania pamoja na kukusanya takwimu kutoka
katika mito iliyopo Mkoani Dar es Salaam na kuchakata takwimu hizo
katika maabara ya TAFIRI.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi
Mkuu TAFIRI Dkt. Semvua Mzighani amesema kupitia mafunzo hayo Serikali
ya Watu wa China, SAJOREC na EAGLU wametoa vifaa vya utafiti vyenye
thamani ya Tshs Milioni 70 ambavyo vitatumika kwa tafiti za kuangalia
ubora na unadhifu wa maji na mazingira kwa ujumla.
Amesema mafunzo hayo yatawasaidia
washiriki kuwafundisha wenzao katika sekta ya uvuvi ili kuhakikisha
viumbe vinavyotegemea maji katika maisha yao ya kila siku, vinapata maji
safi na salama kutokana na tafiti zitakazokuwa zikifanywa na kutafuta
njia mbadala za kuhakikisha maji yanaendelea kuwa salama na kudhibiti
mabadiliko ya tabia nchi kuathiri usalama wa maji.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo
hayo wamesema mafunzo yatawezesha taasisi mbalimbali zinazohusika na
usalama wa maji kufanya tafiti zenye matokeo chanya ili maji ya Bahari
ya Hindi, maziwa na mito katika Ukanda wa Afrika kuwa salama na kupata
suluhu namna ya kukabiliana na mabadiliko yoyote ya tabia nchi ambayo
yanaweza kusababisha athari katika maji hayo.
Mafunzo hayo yameshirikisha
washiriki kutoka nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na
Ethiopia pia walikuwepo waendesha mafunzo hayo kutoka China.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...