NA SEIF MANGWANGI ARUSHA
TANZANIA imeibuka mshindi wa kwanza katika bara la Afrika wa tuzo ya Kimataifa ya KAIZEN katika viwanda bora na vinavyofanyakazi kwa ufanisi kupitia kiwanda cha A TO Z Textile Mills kilichopo Kisongo Jijini Arusha.
Tuzo hiyo ya Kimataifa ambayo hushirikisha sekta mbalimbali ikiwemo viwanda vya kati na vikubwa zilizofanyika katika mji wa Tunis nchini Tunisia, hutolewa na shirika la kimataifa la misaada la JAPAN (JICA), kwa taasisi hizo kutekeleza majukumu yao kwa kufuata dhana ya KAIZEN ambayo ni kuzalisha kwa tija, ubora, kupunguza gharama.
Kabla ya kuibuka na ushindi huo, A to Z iliibuka kidedea dhidi ya viwanda vyote vya Tanzania katika mashindano ya Tanzania Kaizen Award, yaliyoandaliwa na wizara ya Viwanda na Biashara kupitia kitengo cha Kaizen Tanzania (TKU), yaliyofanyika Machi 1, 2019 Jijini Dar es salaam na kuchaguliwa kwenda kuiwakilisha Tanzania katika ngazi ya Afrika.
Mkurugenzi wa uzalishaji wa kiwanda cha A to Z Textile Mills, Binesh Haria alisema Kampuni 16 kutoka katika nchi za Kenya, Ghana, Ethiopia, Afrika Kusini, Zambia, Cameroon na DRC Congo na Tanzania zilishiriki kwenye tuzo hizo na A to Z kuibuka mshindi wa kwanza kwa kuwa kiwanda bora Afrika.
Mmoja wa wasimamizi wa kitengo cha Kaizen katika kiwanda cha A to Z, na ambaye ndiye aliyewasilisha utekelezaji wa dhana ya KAIZEN katika mkutano huo nchini Tunisia alisema katika uwasilishaji huo ambao hutokana na taarifa ya waangalizi wa tuzo hizo ambazo huzichukua awali baada ya kutembelea viwanda hivyo, Tanzania ilionekana kufanya vizuri zaidi kuliko nchi zingine.
Lyanga alisema baada ya tuzo hiyo, Agosti mwaka huu A TO Z itashiriki kwenye mkutano wa Kimataifa unaojulikana kama TICAD7 utakaoshirikisha wakuu mbalimbali wa nchi kwa lengo la kuzungumzia maendeleo ya Afrika katika sekta tofauti ikiwemo sekta ya viwanda ambapo pia katika mkutano huo, washindi wa tuzo ya KAIZEN watapata fursa ya kueleza utekelezaji wake na mafanikio waliyopata.
Akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa A TO Z, Kalpesh Shah, Meneja wa biashara za nje, Sylvester Kazi alisema tuzo hiyo ya kwanza kutolewa Afrika ni zawadi ya watanzania hasa kupitia Serikali ya wamu ya tano chini ya Rais Dkt John Magufuli.Alisema ni kweli kiwanda cha A to Z kimeibuka mshindi lakini anayestahili kupewa hongera na pongezi nyingi ni Rais Dkt Magufuli kwa kuwa amekuwa akihamasisha uanzishwaji wa viwanda mbalimbali tangu alipoingia madarakani.
Kazi alimuomba Rais Magufuli kuipokea Tuzo hiyo yeye mwenyewe au kupitia kwa kiongozi wa chini yake ambaye ataagiza apatiwe ili kuonyesha ishara ya uwajibikaji na utekelezaji wa malengo ya Serikali ya awamu ya tano ya kuanzishwa kwa viwanda na kutoa ajira nyingi kwa watanzania.
“Sisi kama kiwanda tumefurahi sana na tunafanya utaratibu wa kumfikishia Tuzo hii, Rais wetu Dkt John Pombe Magufuli ili aiweke Ikulu na kuonyesha jitihada zake zinapelekea za kuifanya Tanzania kuwa ya viwanda, tutajitahidi kuwasiliana nae kama itampendeza tutamfikishia Ikulu,”alisema Kazi.
“Pia kiwanda kinapenda kutoa shukrani zake kwa shirika la viwanda vidogo SIDO Mkoa wa Arusha, kitengo cha Kaizen nchini (TKU), shirika la Kimataifa la Ushirikiano wa kimaendeleo la watu wa Japan (JICA) na wizara ya viwanda kwa mchango wao mkubwa wa kufanikisha mafanikio iliyofikia hivi sasa A to Z.
Wawakilishi wa kiwanda cha A to Z, Reuben Lyanga pamoja na Marco Alphay wakiwa katika picha ya pamoja na waandaaji wa tuzo ya Kimataifa ya KAIZEN mara baada ya Tanzania kutangazwa mshindi wa tuzo hiyo katika hafla iliyofanyika katika mji wa Tunis nchini Tunisia
Mwenyekiti wa taasisi ya Lean Institute na mmoja wa majaji wa tuzo ya KAIZEN, Profesa Norman Faull akishuhudiwa mwakilishi wa kiwanda cha A TO Z Reuben Lyanga akivishwa bendera ya Tanzania baada ya kumtangaza kuwa mshindi wa kwanza wa tuzo za KAIZEN 2019.
Tuzo walizokabidhiwa kiwanda cha A to Z baada ya kuiwakilisha vyema Tanzania
Wawakilishi wa A TO Z Reuben Lyanga wa pili kushoto na Marko Aphayo wakiwa wameshikilia tuzo bora ya Afrika ya kaizen 2019 katika picha ya pamoja na Makamu wa Rais wa taasisi ya kimataifa ya Grips na waandaaji wa tuzo hiyo, Professa Tetsushi Sonobe.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...