Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limetoa mwito kwa wafanyabiashara wanaotaka kufanya shughuli zao kwenye nchini za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kufika kwenye ofisi za shirika hilo ili kupata elimu kuhusiana na namna ya kufanya biashara na nchi hizo bila vikwazo vyovyote.
Ushauri huo umetolewa jijini Dar es Salaam na Ofisa Mwandamizi Uhakiki Ubora wa TBS, Stella Mrosso, wakati akizungumza na kwenye Maonesho ya Nne ya Wiki ya Viwanda SADC yaliyomalizika jana (ALHAMISI) katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jana.
Akieleza faida za wafanyabiashara kupata elimu TBS kabla ya kupeleka biashara zao kwenye soko la nchi za SADC, Mrossa alisema hatua hiyo inawasaidia kujua taratibu za kufuata, ambazo zinawasaidia kuepukana na vikwazo mbalimbali.
"Hii inarahisishia biarasha kuliko wale wanaopita juu kwa juu, kwani wanaweza kufika mipakani wakazuiwa kupeleka bidhaa zao kwenye nchi walizokusudia na hivyo kujikuta wakipata hasara kubwa," alisema.
Alisema TBS ni mdau mkubwa kwenye nchi za SADC hasa katika suala zima la umahiri, hivyo kwa ajili ya kuwasaidia. "Sisi tupo kwa ajili yao, kwa hiyo wakipita kwetu na kupatiwa elimu watafanyabiashara vizuri na kukuza uchumi wao na wa nchi kwa ujumla,"alisema.
Pia, aliwataka wafabiashara kufika kwenye ofisi za shirika hilo kuthibitisha ubora wa bidhaa zao, kwani shirika hilo lina maabara zenye umahiri uliothibitishwa kimataifa.
Alifafanua kwamba bidhaa ikishapimwa kwenye maabara zenye umahiri, haiwezi kupimwa tena, kwani matokeo yake yanakuwa yanaaminika.
Alitaja baadhi ya maabara za shirika hilo zenye umahiri kuwa ni maabara ya nguo, maabara ya kemia, maabara ya ujenzi, maabara ya umeme. "Bidhaa zikishapimwa kwenye maabara hizi kwenye soko la SADC haziwezi kupimwa tena," alisema.
Alizidi kufafanua kwamba Tanzania ina maabara 31 zenye umahiri, hivyo kuwa miongoni mwa nchi tatu bora kwenye ukanda wa nchi za SADC zenye maabara nyingi zenye umahiri.
Mrosso, alitaja hatua nyingine ambazo zinachukuliwa na nchi za SADC kuondoa vikwazo vya kibiashara kwa nchi wanachama kuwa ni pamoja na kuoanishwa viwango.
"Sisi kama TBS tuna wajibu mkubwa wa kuoanisha viwango ambavyo vitasaidia wafanyabiashara kuondokana na vikwazo vya kibiashara,"alisema Mrosso na kuongeza kwamba kwenye kuoanisha viwango wanawezesha ufanyikaji biashara bila vikwazo.
Alisema kwenye nchi za SADC viwango ambavyo tayari vimeoanishwa vinafanyakazi kulingana na mahitaji ya wafanyabiashara wa Tanzania.
Alipoulizwa wametujiaje fursa ya kushiriki maonesho ya SADC, Mrosso, alisema wameweza kutoa elimu ya huduma zitolewazo na shirika hilo pamoja na kuwataka wajasiriamali kujitokeza kwa wingi kwenda kuthibitisha bidhaa zao kwani huduma hiyo inatolewa bure.
Mrosso, alisema lengo la hatua hiyo kuwawezesha kufanya biashara, kukuza uchumi wao na wa nchi kwa ujumla. "Pia tunatoa elimu ili kuwawezesha kuzalisha bishaa zenye ubora," alisema.
Ofisa Mwandamizi Uhakiki Ubora wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Stella Mrosso, akizungumza na baadhi wananchi waliotembelea banda la shirika hilo na kwenye Maonesho ya Nne ya Wiki ya Viwanda ya nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) yaliyomalizika jana kuhusiana na shirika hilo linavyowezesha wafanyabiashara kufanya shughuli zao kwenye nchi za SADC bila vikwazo vyovyote. Maonesho yalifanyika katika kwenye kituo cha Mikutano wa Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...