Na Karama Kenyunko, Globu ya jamii

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Agosti 19, mwaka 2019 imeangalia ushahidi wa video uliowasilishwa na shahidi namba sita, Koplo Charles, katika kesi ya jinai namba 112/2019 inayowakabili viongozi wa tisa wa Chadema, akiwemo Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe.

Mawakili wa pande zote mbili na watu mbalimbali wamepata kushuhudia video hiyo iliyooneshwa katika ukumbi wa Chuo cha Mafunzo cha Mahakama kilichopo mahakamani hapo kwa kutumia Projector mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba.

Hata hivyo katika video hiyo inayodaiwa ni ya mkutano uliofanywa na viongozi hao, hakuna mahali popote ambapo palipomuonesha Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko akihutubia katika mkutano huo. 

Pia video hiyo haijaonesha watu wakirusha mawe wala viongozi hao wa Chadema wakiwa katika maandamano bali imeonesha baadhi ya viongozi hao wakihutubia katika mkutano wa kumnadi aliyekuwa mgombea wa ubunge jimbo la Kinondoni Salum Mwalimu na mwisho wafuasi wa chama hicho wakiandamana.

Mapema kabla ya kuangalia ushahidi huo wa video Hakimu Simba alisoma uamuzi na kuruhusu video hiyo kuoneshwa na kutupilia mbali mapingamizi ya upande wa utetezi waliokuwa wakiponga ushahidi huo kuoneshwa mahakamani hapo wakidai kuwa, upande wa mashtaka hawakuwasilisha vifaa vya kusaidia kuonekana kwa video hiyo

Awali, upande wa mashitaka kupitia kwa shahidi wake namba sita uliiomba mahakama hiyo ikubali kuonyeshwa ushahidi wa video kutoka katika kamera ya Koplo Charles kwa kutumia vifaa vya nje.

Akisoma uamuazi huo, Hakimu aliridhia video hiyo kuoneshwa kwa kutumia vifaa vya nje (external device).

Katika zoezi hilo, shahidi namba sita, Koplo Charles alisaidiwa na mtaalamu wa IT Nazari Moshi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuunganisha kamera yake na vifaa vya nje vya mahakama hiyo kwa ajili ya kuonesha video hiyo aliyoigawa mara mbili (Min div 1 &2).

Koplo Carles alionesha video ya kwanza aliyoipa jina la Mkutano wa Chadema wa mwaka 2018 iliyoonesha baadhi ya viongozi na wabunge wa chadema wakiongozwa na Freeman Mbowe, Mwenyekiti Chadema Taifa na Dk. Vicent Mashinji, Katibu Mkuu wa Chadema, wakimnadi Salum Mwalimu aliyekuwa Mgombea wa Jimbo la Kinondoni katika uchaguzi wa marudio wa mwaka huo.

Video hiyo ya kwanza yenye dakika 56 na sekunde 37 ilionesha wabunge kadhaa wa Chadema akiwemo, John heche (Tarime Mjini), Cecil Mwambe (Ndanda), Halima Mdee (Kawe) Ester Bulaya (Bunda Mjini) Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini) wakitoa hotuba zao za kumnadi Mwalimu.

Video ya kwanza ilikwisha, ikawekwa ya pili yenye urefu wa dakika 25 na sekunde 55 ambayo nayo ilimuonyesha Mbowe akihutubia kisha kuhamasisha wananchi kuelekea ofisi ya msimamizi wa uchaguzi wilaya ya Kinondoni.

kwa ajili ya kupata barua ya utambulisho za mawakala wao katika uchaguzi huo wa marudio.Kesi hiyo imeahirishwa hadi kesho

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...