Na Karama Kenyunko, Michuzi TV,
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewaachia huru washitakiwa watano waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka ya kujiunganishia isivyo halali bomba la mafuta mali ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).
Hatua hiyo imekuja baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kuwasilisha hati mahakamani hapo kuonesha kuwa hana nia ya kuendelea na mashtaka dhidi ya washtakiwa na anaondoa kesi hiyo chini ya kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ( CPA), sura ya 20 , iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon amedai kuwa kesi hiyo leo ilikuja kwa ajili ya kutajwa, lakini DPP hana nia ya kuendelea na kesi hiyo dhidi ya washitakiwa hao.Baada ya kueleza hayo, Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba alisema kupitia kifungu hicho, mahakama imewafutia mashitaka washitakiwa wote na inawaachia huru.
Washitakiwa walioachiwa katika kesi hiyo ni Audai Ismail (43) ambaye ni mkazi wa Kibaha, Chibony Emmanuel, Roman Abdon, Amina Shaban na Zubery Ally.
Washitakiwa wote kwa pamoja walikuwa wanakabiliwa na mashitaka matatu likiwemo la kujiunganishia isivyo halali bomba la mafuta, mali ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kinyume cha sheria.
Katika mashitaka ya kwanza, inadaiwa kati ya mwaka 2015 hadi Januari 8, mwaka huu katika eneo la Tungi Muungano wilaya ya Kigamboni, washitakiwa kwa pamoja wanadaiwa kujiunganishia bomba la mafuta ya dizeli lenye upana wa inchi moja kutoa katika bomba lenye upana wa inchi 24, bila kuwa na kibali kutoka TPA.
Pia wanadaiwa kuharibu miundo mbinu ambapo wanadaiwa kutoboa bomba la hilo, ambalo lilikuwa likitumika kusafirisha mafuta, mali TPA.
Inadaiwa washitakiwa waliharibu bomba la mafuta mazito lenye upana wa inchi 28, ambalo lilikuwa likitumika kusafirisha mafuta ghafi, mali TPA.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...