Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na Maendeleo, Freiman Mbowe akisalimiana na Naibu katibu Mkuu Tanzania bara na Mbunge wa jimbo la Kibamba,John Mnyika leo akiwa katika mahaka ya mkazi kisutu jijini Dar es Salaam.

 Viongozi wa chama cha Demokrasia na maendeleo wakiwa katika mahakama ya hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo.

Na Karama Kenyunko, Michuzi TV
MAHAKAMA ya Hakimu ya Hakimu Mkazi Kisutu imetupilia mbali maombi ya Katibu Mkuu wa Chadema, Dr. Vicent Mashinji na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko waliokuwa wanaiomba mahakama hiyo kusafiri kwenda nje ya nchi kwa nyakati tofauti. 

Pia mahakama imewataka washitakiwa hao bila kujali nyadhifa zao kuwepo mahakamani kama washitakiwa wengine.

Imeelezwa kuwa, washitakiwa hao sasa watatakiwa kujitetea kwa siku  tano mfululizo kuanzia Oktoba 7 hadi 11,2019 na mahakama inategemea kuwa hakutakuwepo na sababu zingine zozote zitakazosababisha kesi hiyo isianze kusikilizwa.

Akisoma uamuzi huo, Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba amesema, safari hizo ni mambo yao wenyewe na hayahusiani na ratiba ya mahakama.

Amesema kuwa, iwapo mahakama itaruhusu maombi ya washtakiwa hao kusafiri, itakuwa imefungua mwanya kwa washtakiwa wengine kwani tukiruhusu haya leo hatutaweza kukataa kwa mwingine ukizingatia kuwa washtakiwa hawa wote ni wabunge.

"Maombi haya hayana msingi, hii kesi sasa hivi haiko kwenye hatua ya kutajwa, washtakiwa walikutwa na kesi ya kujibu na sasa wanatakiwa kujitetea" amesema Hakimu Simba.

Ameongeza kuwa, kesi hiyo ni ya muda mrefu, inalalamikiwa sana, inatakiwa kusikilizwa na kufika mwisho na Profesa Safari alisema wanamashahidi wengi sana hivyo kesi hii inahitaji kupangwa mara kwa mara kwa ajili ya kusikilizwa upande wa utetezi.

Jana, Wakili Profesa Abdallah Safari aliwasilisha maombi mawili mahakamani hapo ya kuahirisha  kesi hiyo hadi Oktoba 7 na 8 mwaka huu kwa sababu wanahitaji kupata muda wa kutosha kujiandaa na utetezi.

Amedai kuwa wanahitaji muda wa kutosha wa kujiandaa na utetezi kwa kuwa wana mashahidi wengi ambao wanahitajika kutafutwa na kuandaliwa. 

Pia ameomba ruhusa ya kusafiri kwa mshtakiwa Mashinji  kuanzia Septemba 26 mpaka Oktoba 6 mwaka huu kwenda Uingereza huku mshitakiwa Ester Matiko, Mbunge wa Tarime Mjini, kuanzia Septemba 25 hadi 28, mwaka huu anatakiwa kwenda Kigali nchini Rwanda na Oktoba 13 hadi 18 atakwenda kuiwakilisha nchi barani Ulaya. 

Hata hivyo, upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili wa wa Serikali Mkuu Faraja Nchimbi walipinga maombi hayo yote kwa kuwasilisha hoja mbali mbali. 

Barua ya maombi ya kusafiri Mashinji haijitoshelezi kwani haielezi anakwenda huko kufanya nini na kwanini aende mshitakiwa huyo ambaye tarehe hizo shauri lake litatajwa mahakamani, " alidai Nchimbi. 

Kuhusu mshitakiwa Matiko,  Nchimbi alidai barua ya mshitakiwa huyo inaonesha imetoka Chama cha Wanasheria Wanawake (Tawla)  kwenda kwa Katibu wa Bunge wakiomba uwakilishi wa wabunge sita nchini Kigali. 

Ameidai hayo yanabaki kuwa maombi ambayo yanaweza kukubaliwa au kukataliwa na kuongeza kuwa hakuna sababu ya mshitakiwa huyo kwenda safari hiyo kwa kuwa kuna uwakilishi wa wabunge wengine watano. 

"Ni vema ikafahamika kwamba mtuhumiwa anapokuwa na kesi mahakamani ni wazi ratiba yake kiasi fulani itaingiliwa na taratibu za mahakama,  kama itakuwa kila mshtakiwa akijisikia kusafiri anapatiwa ruhusa kwa vyovyote vile shauri hili halitafikia mwisho," alidai Nchimbi. 

Mbali na Mashinji na Matiko,  washitakiwa wengine ni Mwenyekiti wa Chadema,  Freeman Mbowe, Mbunge wa Iringa mjini, Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu Taifa, Zanzibar, Salum Mwalimu,  Mbunge wa Kibamba, John Mnyika,  Mbunge wa Kawe  Halima Mdee, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya.

Washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka 13 likiwemo la kula njama, ambapo wote wanadaiwa kuwa, Februari Mosi na 16, mwaka jana, Dar es Salaam walikuĺa njama ya kutenda kosa la kufanya mkusanyiko usio halali na kukiuka tamko kutawanyika.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...