Na Karama Kenyunko, Michuzi Tv

RAIA wa Sri Lanka AbdulAzeez Amaan (26) amemuandikia barua Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kuomba kukiri kosa la kusafirisha madini yaliyokuwa na thamani zaidi ya Sh.milioni 36 kinyume na sheria.
Amaan ambaye ni mwanafunzi amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Septemba 26,mwaka 2019 akikabiliwa na shtaka moja la kusafirisha madini hayo bila ya kuwa na kibali wala leseni.
Mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi Wankyo Simon amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba kuwa, Septemba 21 mwaka huu, katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Ambapo mshtakiwa huyo alikutwa akisafirisha madini aina ya Scapolite yenye uzito wa gramu 996.50, Sperssartite gramu 487, Tanzanite gramu 44, Quarts gramu 126, Citrine gramu 174, blue agate gramu 101.80, Toumarine gramu 16, Aquamarine gramu 14.30 na Supphire gramu 5.04 yote kwa pamoja yakiwa na jumla ya Sh.milioni 36.5 bila ya kuwa na kibali.
Hata hivyo baada ya kusomewa shtaka lake Hakimu Simba alimtaka mshtakiwa huyo kutojibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo aina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo  hadi pale itakapopata kibali kutoka kwa DPP.
Wakili wa Utetezi Shabani Mlembe alidai mteja wake amekwishaandika barua kwa DPP la kukiri kosa hilo, hivyo wanaomba tarehe ya karibu ili kufanya utaratibu unaotakiwa kwa mujibu wa sheria.
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, upelelezi wa shauri hilo umekamilika na hawana pingamizi na maelezo hayo ya upande wa utetezi.

Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi kesho itakapokuja kwa ajili ya kutajwa na kukamilisha taratibu.
Wakati huo huo, Hassan Azizi (33),Hassan Shaban (30) na William Daraja wamefikishwa katika Mahakama hiyo wakikabiliwa tuhuma za Uhujumu Uchumi ikiwamo kusafirisha gramu 983.5 za dawa za kulevya aina heroine.
Washtakiwa hao walisomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Vick Mwaikambo.
Upande wa Jamhuri ulidai Septemba 4, mwaka huu eneo la Tegeta Nyaishozi Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam washtakiwa walikutwa na dawa hizo za kulevya
Hakimu alisema washtakiwa hawatakiwi kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Washtakiwa kwa nyakati tofauti walidai kwamba wamekaa mahabusu ya polisi zaidi ya siku 14 na kwamba wamepigwa sana makofi kiasi hawana uwezo wa kusikia vizuri.

Hakimu Mwaikambo amesema kwa sababu wanakwenda mahabusu magereza wana utaratibu wao wa kuwapa matibabu.
Upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika. Hakimu alisema kesi hiyo itatajwa Oktoba 10,mwaka huu na washtakiwa wapelekwe mahabusu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...