Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akizungumza jambo na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwenye moja ya hafla hivi karibuni jijini Dar.


Na Said Mwishehe,Michuzi TV 

SITAKI kukupotezea muda msomaji wa makala haya, naomba tu uelewe mapema leo hii nimeamua kujikita kuzungumzia muunganiko wa kazi kati ya Rais Dk.John Magufuli na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa. 

Ndio kuna kitu nataka kuzungmza kuhusu viongozi wangu hawa wawili ambao nawapenda kwa nafasi sawa huku nikitambua kila mmoja na nafasi yake na mamlaka yake kwa mujibu wa Katiba ya Nchi yetu. 

Nikiri ni mara kadhaa nimeandika makala au chambuzi kuhusu utendaji kazi wa Rais Dk.John Magufuli.Nimeandika sana kuhusu Rais wetu. 

Nimeandika kuhusu mambo ya msingi ambayo anayasimamia katika kuhakikisha Taifa la Tanzania linasonga mbele.Niahidi kadri nitakavyopata nafasi na uhai nitaandika tu.Nasisitiza nitaandika kuhusu Rais wangu, kikubwa nifuate sheria na taratibu zilizopo. 

Kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa nikiri kwamba sijawahi kuandika chochote tangu amekuwa katika nafasi hiyo.Nazugumzia kuandika makala au uchambuzi kuhusu Waziri Mkuu.Kweli sijawahi. 

Hata hivyo kwa kuandika habari zinazohusu Waziri Mkuu, namshukuru Mungu kwani kazi hiyo nimekuwa nikiifanya sana tena kwa nyakati tofauti.Kuna tofauti kati ya kuandika habari na makala au kuandika habari na uchambuzi. 

Kwa leo naomba niandike kuhusu Waziri Mkuu.Navutiwa na utendaji wake wa kazi, navutiwa na namna ambavyo anatimiza majukumu yake kwa nafasi yake ya Waziri Mkuu. 

Ukweli Waziri Mkuu Kassim Majaliwa unajua namna ya kufanya kazi zako, unajua kutekeleza majukumu yako, unajua kuwasimamia walio chini yako.Waziri Mkuu wewe ni jembe.Tena ni jembe la kazi. 

Tangu Rais Dk.Magufuli alivyokuteua nafasi hiyo umekuwa makini kwa kila ambacho unakifanya.Unajua namna ya kuhakikisha Serikali ya Awamu ya Tano inakwenda vizuri.Kweli Waziri Mkuu uko vizuri. 

Nimekuwa nikifuatilia ziara zako, nimekuwa nikifuatilia maagizo yako na kubwa zaidi nimekuwa nikifuatilia misimamo yako.Kuna wakati huwa najifikirisha ujinga. 

Ndio nafikiri ujinga kwasababu kadri navyokutafakari nakosa majibu ya moja kwa moja wewe ni wa aina gani.Hata hivyo jibu langu la moja kwa moja nalipata kuwa wewe unastahili kuwa Waziri Mkuu na Rais wetu mpendwa hakukosea kukuteua katika nafasi hiyo. 

Kwa kuwa nimeamua kuandika kuhusu wewe, leo nataka nikuambie jambo.Iko hivi baada ya Rais Magufuli kushinda uchaguzi Mkuu na kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzaia, kitendawili kikabaki nani atakuwa Waziri Mkuu wake. 

Kila Mtanzania alitaka kufahamu nani atakuwa Waziri Mkuu.Tunafahamu Dk.Magufuli akiwa katika harakati za kuutaka urais hakuwa na makundi, hivyo haikuwa rahisi kujua nani atakuwa nani baada ya kushinda kiti cha urais. 

Wakati tunasubiri nani atakuwa Waziri Mkuu, nakumbuka nilipata nafasi ya kwenda mkoani Mbeya na nilifikia wilayani Mbalali katika mji mdogo wa chimala. 

Sikumbi tarehe, wala mwezi ila nakumbuka nilikuwa na rafiki yangu ambaye ni Mwandishi Mwandamizi wa gazeti la Majira.Anaitwa David John. 

Nimeamua kumtaja mwandishi huyu si kwasababu ya kutaka kumpa sifa au umaarufu.Hana sifa ya kuwa maarufu au kuwa na sifa ila anabaki kuwa mwandishi makini na anayejua kutimiza majukumu yake. 

Tukiwa Mbeya tunaendelea na majukumu yetu, tukapata nafasi ya kusikia Rais atatangaza jina la Waziri Mkuu ambalo litapelekwa bungeni kwa ajili ya kupigiwa kura na wabunge. 

Hivyo wakati tukisubiri nani atapendekezwa katika nafasi hiyo , tukiwa katika moja ya mgawa,baadhi ya wananchi waliamua kutaja baadhi ya wabunge ambao wanadhani wangeweza kupendekezwa na Rais kushika nafasi hiyo ya Waziri Mkuu. 

Binafsi nilitaja jina la Kassim Majaliwa.Baada ya kutaja jina hilo kukaibuka mjadala.Huyu mwandishi wa Majira David John akawa anakubaliana nami kuhusu Kassim Majaliwa lakini akawa ananiambia hataiweza nafasi hiyo kwasababu ni mpole.Ndivyo alivyokuwa anamtafsiri kwa wakati huo. 

Nadhan alikuwa anaangalia haina ya Kassim Majaliwa ambaye kimuonekano ni mpole lakini kiutendaji yuko makini na mkali. 

Nilimwambia David John , sawa Kassim Majaliwa anaweza kuwa mpole lakini nafasi ya Waziri Mkuu inaweza kumbadilisha na akaimudu vema. 

Hicho ndicho ambacho kimenifanya leo hii niandike makala haya.Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameimudu nafasi hiyo.Nimekuwa nikimfuatilia hatua kwa hatua.Yuko vizuri sana. 

Hata hivyo nimekuwa nikijiuliza Rais Magufuli alifikiria nini hadi kuamua Kassim Majaliwa awe Waziri Mkuu wake. Aliona mbali sana.Rais Magufuli wewe uliona mbali sana kuamua kumchagua Kassim Majaliwa. 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa sasa yuko mkoani Morogoro katika ziara ya kikazi.Watendani na viongozi wazembe wanaipata freshi.Wanakiona cha mtema kuni. 

Tayari Mkurugenzi na Mkuu wa Wilaya ya Malinyi wako pembeni.Madudu ambayo amekutana nayo Waziri Mkuu aliamua kuchukua hatua kwa nafasi yake kimamlaka na mengine akaacha kwa Rais.Kama unavyojua tena Rais Magufuli hana muda wa kuvumilia mambo ya hovyo.Ametengua nafasi za viongozi hao. 

Kama kuna muungano mzuri na wenye tija katika kutenda kazi ya kuwatumikia Watanzania basi ni huu unaoneshwa na Rais pamoja na Waziri Mkuu.Katika soka huwa nawafananisha na wachezaji maalufu duniani ambao ni Christiano Ronaldo na Lionel Mess.Wachezaji hao kila mmoja anakuwa uwanjani acha kabisa.Ni mafundi wanaojua kutafuta ushindi kwa ajili ya timu zao. 

Hadi leo ni ngumu kujua nani zaidi kati ya Mess na Ronaldo.Kwa utendaji kazi wa Rais Magufuli na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa hawana tofauti na wachezaji hao. 

Wanajua wanachokifanya kuhakikisha Tanzania inashinda katika mapambano ya kiuchumi na hatimaye kuwa na maendeleo.Wanahakikisha wanashinda katika kurudisha nidhamu kwa watendani wa umma. 

Ingekuwa ni wanasoka basi ningesema Rais ni Mess na Waziri Mkuu ni Ronaldo.Sio mfano mzuri kwa wazee wangu hawa lakini nia yangu ni kujaribu kuwaelezea kwa namna ambavyo huenda watu wakanielewa.Niombe msamaha kwa kutoa mfano huo.Sina nia mbaya. 

Pia najua baada ya Rais Magufuli kuamua kuwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa vyovyote vile kuna mambo walizungumza na kukubaliana.Sina hakika walizungumza nini lakini leo hii naomba nieleze kitu.Nataka kuwaza kile ambacho walikubaliana. 

Huenda hawakuzungumza mambo mengi lakini moyo wangu eti unaniaminisha kuwa Rais Magufuli na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa walipokutana kwa mara ya kwanza baada ya mazungumzo yao ya kuhusu Tanzania mpya wakamalizia na wimbo huu;Tuimbe wote tena mkono ukiwa umeweka kifuani na itapendeza ukiwa upande unaokaa moyo. 

Tuanze kuimba; 


KIITIKIO(1) 

Tanzania Tanzania nakupenda kwa moyo wote 
Nchi yangu Tanzania jina lako ni tamu sana 
Nilalapo nakuota wewe 
niamkapo ni heri mama we! 
Tanzania Tanzania nakupenda kwa moyo wote 

UBETI WA KWANZA 

Tanzania Tanzania ninapokwenda safirini kutazama maajabu, biashara nayo makazi 
Sitaweza kusahau mimi mambo mema ya kwetu kabisa 
Tanzania Tanzania nakupenda kwa moyo wote 


KIITIKIO(MARA 1) 

Tanzania Tanzania nakupenda kwa moyo wote 
Nchi yangu Tanzania jina lako ni tamu sana 
Nilalapo nakuota wewe 
niamkapo ni heri mama we! 
Tanzania Tanzania nakupenda kwa moyo wote 


UBETI WA PILI 

Tanzania Tanzania watu wako ni wema sana, 
Nchi nyingi zakuota nuru yako hakuna tena, 
Nawageni wakukimbilia ngome yako imara kweli we, 
Tanzania Tanzania heri yako ni kwa mataifa 

KIITIKIO 

Tanzania Tanzania nakupenda kwa moyo wote, 
Nchi yangu Tanzania jina lako ni tamu sana, 
Nilalapo nakuota wewe, 
niamkapo ni heri mama we! 
Tanzania Tanzania nakupenda kwa moyo wote, 


UBETI WA TATU 

Nchi nzuri Tanzania, karibu wasio kwao, 
Wenye shida na taabu hukimbizwa na walowezi, 
Tanzania yawakaribisha mpigane kiume chema we, 
Tanzania Tanzania mola awe nawe daima. 

Nimeamua kuweka mashairi wa wimbo huo nikiamini mengi ambayo yanafanywa na viongozi hao utaona yanauhusiano mkubwa na yaliyomo katika mashairi ya wimbo huo.Ndio.Soma beti moja baada ya nyingine.Kisha changanua kisha tafsri matendo ya viongozi hao katika kuwatumikia Watanzania.Inatosha kwa leo. 

KWA HERUFI KUBWA KAMA VIPI TUWASILIANE KWA 0713833822

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...