Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama baadhi ya vifaa tiba vilivyopatikana kutokana na juhudi za mbunge wa Geita vijijini, Joseph Msukuma (kulia) kwa ajili ya hospitali ya wilaya ya Geita iliyopo katika kijiji cha Nzela, wakati alipokagua ujenzi wa hospitali hiyo na kuzungumza na wananchi Septemba 21, 2019. Wa pili kulia ni Mganga Mkuu wa wilya ya Geita, Deo Kisaka.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Vijana wa kijiji cha Nzela katika jimbo la Geita Vijijini wakimshangilia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza na wananchi baada ya kuakagua ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Geita, Septemba 21, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi baada ya kukagua ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Geita katika kijiji cha Nzela, Septemba 21, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

…………………………………………………
*Yaonesha kutoridhika na kasi, Waziri Mkuu atoa maagizo kwa NIDA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameitaka Mamlaka ya Usajili wa Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ihakikishe wananchi hasa walioko vijijini wanapata angalau namba za utambulisho wa usajili wao kabla ya muda wa usajili wa laini za simu haujamalizika.

Ametoa agizo hilo jana (Jumamosi, Septemba 21, 2019) wakati alizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa hospitali ya wilaya ya Geita iliyopo kwenye Kijiji cha Nzela.

Alisema kitendo cha kuwapatia namba za utambulisho wa usajili wananchi ambao hawajapata vitambulisho vya uraia kitawezesha kuingia kwenye orodha ya wale wanosubiri kusajiliwa hata kama muda wa usajili utakuwa umeisha. Mwisho wa muda wa usajili ni Desemba mwaka huu.

Waziri Mkuu alisema Serikali imewapatia NIDA vifaa vya kisasa vya kielektroniki ili wafanye kazi zao kwa haraka na ufanisi, lakini hali hairidhishi kwa sababu wananchi wengo bado hawajapata vitambulisho na kasi ya usajili wa laini za simu inalalamikiwa katika meneo mengi.

“NIDA mnalalamikiwa, nimeenda Morogoro Vijijini NIDA mnalalamikiwa hivi utendaji wenu uko je? Kwanini mnachelewa ?” Waziri Mkuu alimuuliza Afisa Msajili wa NIDA wa wilaya ya Geita, Paschal Saro ambaye alijitetea kwamba wamesajili laini za simu 340 na tayari namba za usajili 330 zimeshatolewa.

Saro alimwambia Waziri Mkuu kuwa suala la utata wa uraia kwa baadhi ya wananachi wanaoomba vitambulisho vya NIDA ni moja ya sababu zinazochelewesha usajili wa vitambulisho vya uraia.

Waziri Mkuu aliwasihi wananchi wote kuwa walinzi wa nchi yao kwa kutoa taarifa za watu ambao wanaomba viutambulisho vya uraia wa Tanzania wakati si raia na aliwataka watoe taarifa mara moja kwenye vyombo vya dola pale wanapogundua kuwa kuna raia wa nje anafanya mchakato wa kuapata vitambulisho hivyo.

Alisema katika baadhi ya mikoa ya mipakani ambayo ina wakimbizi Serikali imekamata silaha ambazo raia hawasurusiwi kuzimiliki na zinasadikiwa kuwa zimepenyezwa nchini na raia wa nje wasiowaaminifu.

Awali,Waziri Mkuu, alikagua ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Geita iliyopo katika kijiji cha Nzera mkoani Geita na kufurahishwa na hatua ya Mbunge wa jimbo wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma ambaye amewezesha upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa kwa ajili ya hospitali hiyo.

Waziri Mkuu alimpongeza Musukuma kwa moyo wa upendo alionao kwa wapiga kura wake. Vifaa hivyo ni vya kisasa na vinastahili kuwa katika hospitali za rufaa za mikoa lakini mbunge huyo ameamua kuwapelekea wapiga kura wake kwenye hospitali ya wilaya lengo likiwa ni kuboresha huduma.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...