Muonekano wa hatua za ujenzi wa Daraja la Magara lenye urefu wa mita 84
ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 75, utagharimu zaidi ya shilingi Bilioni 12
na unatarajiwa kukamilika mwezi Februari 2020, Mkoani Manyara.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya
Ujenzi) Arch. Elius Mwakalinga, ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa Daraja
la Magara lenye urefu wa mita 84 na barabara za maingilio KM 4.
Katibu Mkuu Mwakalinga, amesema kuwa daraja hilo linajengwa na
mkandarasi M/s China Railway Seventh Group kwa muda wa miezi ishirini
na sita (26) na kuongeza kuwa daraja hilo ni kiungo muhimu kwani
litaunganisha Wilaya ya Mbulu na Makao Makuu ya Mkoa wa Manyara.
Amefafanua pia daraja hilo litaunganisha hifadhi ya Taifa ya Manyara na
Tarangire kupitia Mayoka pamoja na kuunganisha mashamba makubwa ya
mpunga na miwa yaliyopo ng'ambo ya pili ya Mto na masoko ya Babati,
Arusha na kwingineko kwa vipindi vyote vya mwaka.
Katibu Mkuu ameyazungumza hayo katika eneo la Magara, mkoani
Manyara ambapo pamoja na mambo mengine alipokea taarifa ya mradi
kutoka kwa Mshauri Elekezi M/S Crown Tech Consult na kukagua hatua za
ujenzi wa daraja hilo na kusisitiza kwa mkandarasi kukamilisha daraja hilo
kwa mujibu wa mkataba.
"Nimeridhishwa na kazi zilizofanyika mpaka sasa, naomba Meneja wa
TANROADS endelea kusimamia daraja hili likamilike kwa muda
uliopangwa", amesisitiza Arch. Mwakalinga.
Ameongeza kuwa ujenzi wa daraja hilo la Magara utachochea ukuaji wa
utalii na uchumi katika mkoa wa Manyara na Taifa kwa ujumla.
Arch. Mwakalinga, ametoa wito kwa wananchi wa Magara kuendelea kutoa
ushirikiano kwa mkandarasi ikiwa ni pamoja na kutojihusisha na vitendo
vya wizi wa vifaa vinavyotumika katika ujenzi wa Daraja.
"Nitoe wito kwa wananchi wa maeneo haya kuwa daraja pamoja na
miundombinu yake ni mali ya umma hivyo ni jukumu la wananchi kuilinda
na kuitunza", amesema Arch. Mwakalinga.
Naye Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Manyara
Eng. Bashiri Rwesingisa, amemueleza Katibu Mkuu huyo kuwa ujenzi wa
daraja hilo unatarajia kukamilika mwezi Februari mwakani na unagharimu
kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 12.
Eng. Rwesingisa ameendelea kueleza kuwa hatua za mradi mpaka sasa
zimefikia asilimia 75 na kazi nyingi zimefanyika ikiwemo kuweka mihimili ya
chuma kwa ajili ya kubeba zege la juu la Daraja limekamilika asilimia 100.
Ameongeza kuwa katika mradi huo mkandarasi atatakiwa kuhakikisha
mazingira ya Mto Magara yanakuwa salama hii ikiwa ni pamoja na
kupanda miti ili kuufanya mto huo usihame.
Daraja la Magara lipo umbali wa KM 21 kutoka Mbuyu wa Mjerumani katika
barabara kuu ya Babati - Arusha ili kuwezesha kuvuka mto Magara katika
barabara ya Mkoa ya Mbuyu wa Mjerumani - Mbulu yenye urefu wa KM 49.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Arch. Elius Mwakalinga, akitoa maelekezo kwa Mkandarasi wa Kampuni ya M/S China Railyway Seventh Group anayejenga Daraja la Magara lenye urefu wa mita 84 na barabara za maingilio KM 4 kwa kiwango cha lami, wakati alipotembelea na kukagua hatua za maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo, Mkoani Manyara.
Meneja wa Wakala wa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Manyara Eng. Bashiri Rwesingisa, akifafanua jambo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Arch. Elius Mwakalinga, wakati alipotembelea na kukagua hatua za maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Magara lenye urefu wa mita 84 na barabara za maingilio KM 4 kwa kiwango cha lami, Mkoani Manyara.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Arch. Elius Mwakalinga, akitoa maelekezo kwa Mshauri Elekezi kutoka Kampuni ya Crown Tech Consult anayesimamia ujenzi wa Daraja la Magara lenye urefu wa mita 84 na barabara za maingilio KM 4 kwa kiwango cha lami, wakati alipotembelea na kukagua hatua za maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo, Mkoani Manyara.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Arch. Elius Mwakalinga, akielekea kukagua hatua za ujenzi wa Daraja la Magara lenye urefu wa mita 84 na barabara za maingilio KM 4 kwa kiwango cha lami ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 75 na unatarajiwa kukamilika mwezi Februari 2020, Mkoani Manyara.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...